Na Esther Macha,TimesMajiraOnline,Mbeya
MGOMBEA ubunge wa Jimbo la Uyole kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), ambaye pia ni Rais wa Umoja wa Mabunge Duniani (IPU), Dkt. Tulia Ackson, amesema ataendelea kulipia bima za afya kwa familia zenye mazingira magumu, ili kuhakikisha wananchi wote wanapata huduma bora za matibabu.
Akizungumza Oktoba 4, 2025, wakati wa mkutano wa kampeni katika Kata ya Mwansekwa,Dkt.Tulia amesema mpango huo utaimarishwa zaidi kutokana na ukubwa wa mahitaji na idadi ndogo ya kata katika Jimbo la Uyole.
“Ndugu zangu, Februari 2025 tulitoa zaidi ya bima za afya 9,000 kwa wananchi kutoka kata 36 za Jimbo la Mbeya Mjini. Sasa tupo katika kata 13 za Jimbo jipya la Uyole, hivyo msiwe na wasiwasi bima zitaendelea kutolewa kwa kaya zenye uhitaji, na zoezi hili litakuwa kubwa zaidi,” amesema Dkt. Tulia.
Ameongeza kuwa zoezi hilo litahusisha kata zote 13 na mitaa 60, hivyo idadi ya wananchi watakaonufaika itaongezeka maradufu.
“Mwakilishi wenu wa udiwani, Juma, ndiye atakayekusanya orodha ya majina ya wenye uhitaji katika mitaa yenu akileta taarifa hizo, mimi nitazifanyia kazi kwa kuwa ndiye mwakilishi wenu wa karibu,” amesema.
Akijibu changamoto zilizotolewa na wananchi, Dkt. Tulia ameahidi kushughulikia tatizo la paa la Zahanati ya Mwansekwa linalovuja, huku akieleza kuwa kipaumbele cha sasa katika sekta ya afya ni ujenzi wa jengo la mama na mtoto pamoja na ukarabati wa miundombinu ya zahanati hiyo.
Kwa upande wake, diwani wa kata hiyo, Juma, alimwomba Dkt. Tulia kusaidia ukarabati wa paa la zahanati, kuboresha miundombinu ya barabara na kuhakikisha wananchi wote wanapatiwa umeme kupitia mradi wa REA.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako