Na Agnes Alcardo, Timesmajira Online-Dar
MGOMBEA Mwenza wa kiti cha Urais kwa tiketi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amesema, lengo la Serikali chini ya chama hicho ni kuhakikisha mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na halmashauri inawafikia walengwa waliokusudiwa, ambao ni wanawake,vijana.na watu wenye ulemavu.
Akizungumza na wananchi wa Wilaya ya Kinondoni Oktoba mosi,2025, kwenye uwanja wa Biafra, uliopo wilayani humo jijini Dar-es-Salaam,Dkt. Nchimbi amesema, mikopo hiyo inayotolewa na halmashauri zote nchini, lengo ni kuwasaidia wananchi wa kipato cha chini, ili waweze kujikwamua kiuchumi.

“Miaka mitano inayokuja Dkt.Samia amesema, mikopo ya asilimia 10,si kwa ajili ya matajiri ni kwa ajili ya vijana na wanawake wanaojitafuta.hivyo alipoona mfumo wa mwanzo unaleta upendeleo alisimamisha na sasa umetengenezewa mfumo mpya unaofuta upendeleo na ubaguzi, ambapo hivi sasa unawafikia walengwa,” amesema Dkt. Nchimbi.
Pia Dkt. Nchimbi ameahidi ujenzi wa barabara ya juu (flyover) katika makutano ya eneo la Mwenge, ikihusisha makutano ya barabara ya Ali Hassan Mwinyi na Kinondoni, Magomeni na ujenzi wa barabara ya mabasi ya mwendokasi kuunganisha barabara ya Mwai Kibaki na Kigogo.
Amesema Serikali itahakikisha biashara za wafanyabiashara wadogo wadogo zinapewa hadhi rasmi ili waweze kukopesheka na kushiriki kikamilifu kwenye mfumo wa fedha.
“Tunahitaji mfumo wa kodi rafiki, ambao si wa shuruti bali unampa mteja heshima. TRA lazima washirikiane na wafanyabiashara kama marafiki na si maadui,” amesema Dkt. Nchimbi.
Kwa upande wake mgombea Ubunge wa Jimbo la Ilala kupitia CCM, Mussa Azan Zungu, amesema Ilala ni kitovu cha biashara na ukusanyaji wa mapato kwa taifa, ambapo kwa sasa inakusanya shilingi bilioni 130 huku malengo mapya yakiwa ni kufikia shilingi bilioni 170.

Zungu pia amewataka watanzania kudumisha amani na mshikamano wa kitaifa akibainisha kuwa endapo amani itaharibiwa watakaohathirika zaidi ni watoto, wanawake na wazee.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako