March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mkemia Mkuu ni muhimu kwa usalama wa matumizi ya kemikali 

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online 

MENEJA  wa Kanda ya Ziwa wa Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, John Faustine, amesema ofisi hiyo ina nafasi muhimu na ya kipekee katika kuhakikisha usalama na uendelevu wa matumizi ya kemikali, hasa kwenye sekta ya madini ambayo kwa kiasi kikubwa hutegemea kemikali katika uchimbaji na uchenjuaji wa madini.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati wa Maonesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Faustine amesema Mamlaka hiyo imekuwa ikitekeleza majukumu yake katika maeneo makuu mawili: usimamizi wa sheria na uchunguzi wa kimaabara.

“Tupo hapa kwenye maonesho kwa sababu sisi ni wadau wakuu wa sekta hii. Huwezi kupata dhahabu au madini mengine yoyote bila kutumia kemikali. Sisi kama Mkemia Mkuu wa Serikali tunahakikisha kemikali hizo zinasimamiwa kisheria na kimazingira ili ziwe salama kwa binadamu na mazingira,” alisema Faustine.

Ameeleza kuwa Mkemia Mkuu wa Serikali ndiye msajili wa kemikali zote nchini na hutoa vibali vya kuingiza, kusafirisha na kutumia kemikali kwa mujibu wa Sheria ya Udhibiti na Usimamizi wa Kemikali za Viwandani na Majumbani Na. 3 ya Mwaka 2003.

“Shughuli nyingi za binadamu zinahusisha kemikali, hivyo ni muhimu kuwa na miongozo ya matumizi salama. Tunashughulika pia na usajili wa wadau wote wa kemikali, maeneo wanayotumia, aina za kemikali wanazotumia, na kuhakikisha wanazingatia sheria,” aliongeza.

Kwa upande wa sekta ya madini, Faustine alieleza kuwa maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali hutoa huduma ya uchunguzi wa kimaabara kwa wachimbaji na wachenjuaji, hasa wanaofanya shughuli zao kwa kiwango kidogo.

“Wachimbaji wadogo wanapaswa kupeleka sampuli za udongo kwenye maabara zetu kabla ya kuanza uchenjuaji. Tunawasaidia kujua ni kiasi gani cha dhahabu kilichopo kwenye udongo huo, pamoja na kutambua uwepo wa madini shindani kama silva, kopa, na salfa ambayo huweza kuathiri upatikanaji wa dhahabu wakati wa uchenjuaji,” amefafanua.

Ameongeza kuwa kemikali zinapokuwa na ushindani na madini mengine, huathiri uwezo wa mchenjuaji kupata dhahabu kwa ufanisi, hivyo maarifa ya awali kutoka maabara ni muhimu sana kwa matokeo bora.

Ametumia nafasi hiyo kutoa wito  kwa watumiaji wote wa kemikali kufuata taratibu za  matumizi salama kwani kemikali ikitumika vibaya huweza kuathiri siyo tu mtumiaji, bali pia mazingira na jamii inayomzunguka na kwamba ifika ardhini, haina mpaka  inaweza kusambaa kwa mbali na kusababisha madhara makubwa.

Faustine amewakaribisha wananchi na wadau kutembelea banda la Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali katika maonesho hayo ili kupata elimu zaidi, kujifunza teknolojia mpya, na kutatuliwa changamoto mbalimbali zinazohusu kemikali na maabara.