March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

DC Nyangh’wale avutiwa na hatua za BoT katika ununuzi na uhifadhi wa dhahabu

Na Joyce Kasiki, Timesmajira Online – Geita

MKUU wa Wilaya ya Nyang’hwale, Bi. Grace Kingalame, ameeleza kufurahishwa kwake na hatua kubwa iliyopigwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika ununuzi na uhifadhi wa dhahabu, huku akiwahamasisha wachimbaji wa wilaya yake kuendelea kuuza dhahabu yao kupitia njia halali na kwa serikali.

Akizungumza Septemba 24, 2025, baada ya kutembelea banda la BoT kwenye Maonyesho ya Nane ya Teknolojia ya Madini yanayoendelea katika viwanja vya Dkt. Samia Suluhu Hassan, Bombambili mkoani Geita, Bi. Kingalame ameema hadi sasa BoT imekusanya akiba ya dhahabu takribani tani 10, hatua aliyoitaja kuwa ya kihistoria na yenye mafanikio makubwa kwa Taifa.

“Ni jambo la msingi kumpongeza Rais wetu Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa nafasi kubwa ambayo Tanzania imefikia. Sasa tuko miongoni mwa nchi tano zinazozalisha dhahabu kwa wingi barani Afrika, na tumeweza kuwa na akiba ya dhahabu ya kutosha kupitia BoT,” amesema Bi. Kingalame.

Ameeleza kuwa serikali haijawabana wachimbaji kupeleka dhahabu yao nje ya nchi, lakini pia imeweka mazingira bora ya wao kuuza kwa serikali ili Taifa linufaike kupitia akiba na mapato yatokanayo na madini hayo.

“Hii ni nafasi kwa wachimbaji wa Nyang’hwale na maeneo mengine kuuza dhahabu kwa serikali ili nasi tuendelee kuwa na ‘reserve’ ya dhahabu inayoiimarisha nchi yetu kiuchumi na kifedha,” amesisitiza.

Bi. Kingalame amewataka wananchi na wadau mbalimbali wa madini kutembelea maonyesho hayo ili kujifunza kuhusu maendeleo ya teknolojia kwenye sekta ya madini, hususan katika uchimbaji, uchenjuaji na uchorongaji wa dhahabu.

“Nimefurahishwa sana kuona namna teknolojia inavyozidi kukua na kuleta tija katika shughuli za madini,hii ni fursa kwa wachimbaji wadogo na wa kati kuongeza maarifa yao na kufanya kazi kwa tija zaidi,” alisema.

Aidha, ameeleza kufurahishwa kwake na namna wajasiriamali walivyoshiriki maonyesho hayo, wakijipambanua kwa ubunifu, juhudi na mshikamano katika kujikwamua kiuchumi.

“Ni jambo la kufurahisha kuona wanawake na vijana wakiendesha shughuli zao kwa ubunifu mkubwa. Hili linaonesha kuwa dhamira ya Rais Samia ya uchumi shirikishi inatekelezwa kwa vitendo,” aliongeza.