Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Dar
NAIBU Katibu Mkuu wa Wizara ya Ujenzi, Dkt. Charles Msonde, ameipongeza Bodi ya usajili wa wahandisi (ERB) kwa kuandaa Jukwaa la wahandisi vijana 2025,ambalo ni muhimu kwa mshikamano na ubunifu wa mustakabali wa taifa.
Dkt Msonde ametoa pongezi hizo Jijini Dar-Sala,Septemba 23,2025 wakati akifunga Jukwaa la wahandisi vijana 2025,amesema limekuwa chachu ya kubadilishana uzoefu miongoni mwa wahandisi vijana, jambo linalojenga msingi imara wa maendeleo ya taifa.

“Nafahamu jukwaa hili limekusudiwa kutuweka pamoja. Tukiwa pamoja tunapata nafasi ya kushirikiana, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ubunifu kwa manufaa ya jamii na taifa zima,” amesema Dkt.Msonde.
Hivyo amewataka vijana hao kutumia vyema mifumo na programu mbalimbali zinazoratibiwa na ERB pamoja na AQRB, ambazo zimekuwa zikiwasaidia kukua kitaaluma kwa kasi.
Dkt. Msonde amesisitiza kuwa mafanikio katika uhandisi yanahitaji ujasiri, ubunifu na ushirikiano wa kimkakati, hivyo aliwasihi vijana hao kutumia maarifa waliyojifunza kutatua changamoto zinazokabili jamii.
“Mmesoma, mna ujuzi na maarifa ya kuwawezesha kupiga hatua.Msikate tamaa pale mawazo ya kibunifu yanaposhindwa kwani ni ishara ya safari ya kuelekea mafanikio,”.
Amesema mustakabali wa uhandisi nchini hautategemea wataalamu wa kigeni bali ubunifu wa vijana wa Kitanzania wenyewe.
Kwa upande wake, Kaimu Msajili wa ERB, Wakili Mercy Jilala amesema kupitia kongamano hilo wahandisi vijana 145 na wengine 85 walikuwa wakifuatilia mafunzo hayo kwa njia ya mtandao wamepata elimu ya kitaaluma na ujasiriamali pamoja na mafunzo ya namna ya kuanza maisha baada ya uhandisi bila kutegemea ajira.
“Lengo ni kuongeza uwezo wa vijana wahandisi ili waweze kujiajiri na kuwaajiri wengine,” amesema

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya ERB, Mhandisi Wakili Menye Mangu, amebainisha kuwa mafunzo kama hayo yataendelea kutolewa ili kuwawezesha vijana kujikwamua kiuchumi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Miongoni mwa washiriki, katika jukwaa hilo Vanessa William amesema mafunzo hayo yamemsaidia kujiandaa na kujikita kikamilifu katika sekta ya uhandisi, sambamba na kufanya kazi kwa ubunifu zaidi.
“Inabidi tutumie ubunifu na njia mahsusi zitakazotuwezesha kufanya kazi kwa ukubwa na kwa uhalisia,” amesema

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina