March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Serikali yaipongeza Benki ya TCB kwa kuanzisha hatifungani ya Stawi

Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Dar

SERIKALI imeipongeza Benki ya TCB kwa kuwa benki ya kwanza ya Serikali kutoa hatifungani ya Stawi ambayo inalenga kuwahudumia wafanyabiashara ndogo ndogo na wakati hapa nchini na hatimaye watakapokuwa wanapata fedha kwenye benki kama hiyo wataweza kukuza biashara zao na hatimaye wataweza kuwa makampuni makubwa.

Pongezi hizo zilitolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Wizara ya Fedha, Elijah Mwandumbya, wakati wa uzinduzi wa Hatifungani ya Ustawi inayomilikiwa na Benki ya TCB.

Amesema iwapo watakuwa na makampuni wataweza kutoa ajira kwa watu wengine, lakini pia wataweza kulipa kodi na mambo mengine mbalimbali.

Mwandumbya amesema TCB ni benki inayomilikiwa na Serikali kwa asilimia 100, ambapo baada ya mapinduzi makubwa ya benki hiyo imeona ni vema ikaanzisha hatifungani maalum ya Stawi ambayo ina lengo la kuwakaribisha Watanzania na wawekezaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi waweze kushiriki katika uwekezaji kwenye hatifungani hiyo na hatimaye waweze kupata mapato kutokana na uwekezaji huo.

Mwandumbya amezidi kufafanua kuwa kupitia uwekezaji huo mwekezaji ataweza kupata riba ya asilimia 13.5, kama ataweka fedha isiyopungua sh. 500,000 kwenye bondi hiyo ambayo itasimamiwa na TCB.

Aidha, amefafanua kwamba lengo la Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Dkt. Samia Suluhu Hassan, ni kuhakikisha wananchi na wajasiriamali wanapata bidhaa na huduma hususan katika sekta ya fedha kwa gharama nafuu.

“Kwanza zinapatikana, lakini pia zinapatikana kwa gharama nafuu na kwa miaka hii minne Serikali imefanya kazi kubwa ya maboresho ya sera, sheria na kanuni mbalimbali za uwekezaji katika sekta ya fedha na uendeshaji wa biashara na ili kuhakikisha malengo haya yanatimia hatimaye leo hii tumeshuhudia TCB ikizindua hatifungani ya Stawi,” amesema Mwandumbya.

Akizungumza kwa niaba ya Menejimenti ya benki, Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu wa Benki ya TCB, Adam Mihayo, amesema ana furaha kubwa kushuhudia hatua hiyo muhimu wanapozindua rasmi hatifungani ya Stawi.

Amesema Hatifungani yenye Jina la Stawi inaashiria ukuaji na ustawi kwa jamii yetu ni awamu ya kwanza ya programu ya hatifungani ya miaka mitano yenye thamani ya sh. Bilioni 150 za Kitanzania.

“Toleo hili la kwanza linatoa fursa ya uwekezaji wa hadi kiasi cha sh.
Bilioni 50 za Kitanzania ambacho kitatolewa kulingana na vigezo vilivyoainishwa kwenye waraka wa toleo,” alisema.

Kwa mujibu wa Mihayo wawekezaji watanufaika na riba ya asilimia 13.5 ambayo italipwa kila baada ya miezi mitatu ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Amefafanua kuwa fedha itakayopatikana kutokana na hatifungani hii itafanya mambo yafuatayo;

“Itaimarisha mtaji wetu wa benki, itasaidia ukuaji wa vitabu vyetu vya mikopo, kuwezesha wafanyabiashara na wajasiriamali kwa kuwapatia mikopo itakayosaidia kukuza biashara ndogo na za kati na kuwapatia wafanyabiashara na wajasiriamali mtaji wa kuendeleza na kupanua
shughuli zao za kibiashara, na kuwezesha kurasimisha biashara ,” amesema Mihayo na kuongeza;

“Hii itawezesha kuongeza vipato vya Watanzania, na vivyo hivyo kuongeza pato la taifa. Na hii yote ni maendelezo ambayo Benki yetu inafanya kuzingatia Dira ya Taifa 2050 katika kusaidia Serikali ya Tanzania kwenye kukuza uchumi kupitia uwezeshaji kwa wafanyabiashara.

Akizungumza kwenye hafla hiyo ya uzinduzi wa Hatifungati ya Ustawi, Afisa Mtendaji Mkuu wa Soko la Hisa Dar es Salaam (DES), Peter Nalitolela, ametoa pongezi kwa Bodi ya Wakurugenzi na Menejimenti ya Benki ya TCB kwa uamuzi huo wa busara wa kutumia masoko ya mitaji na dhamana kuweza kuongeza mtaji na ukwasi ambao utaenda kuchangia katika ukuaji wa benki hiyo na ukuaji wa uchumi kwa ujumla.

Amesema hiyo ni kwa sababu fedha zitakazopatikana zitaenda kuwakopesha wajasiriamali, wafanyabiashara wadogo na wakubwa, wateja binafsi na kwa kiasi kikubwa itaenda kuyasaidia makundi ambayo yana ujumuishi mdogo kifedha ikiwemo akina mama, vijana, wakulima na wafanyabiashara wadogo.

“Uamuzi wa Benki ya TCB kutumia Masoko ya Mitaji ni mwitikio wa agizo la Rais, Dkt. Samia Suluhu Hassan wa kuzitaka taasisi kutumia DSE na masoko ya mitaji na dhamana kwa ujumla wake kupata mitaji na ya kuwekeza na kuendeleza shughuli zao,” alisema Nalitolela

Aidha, ametumia fursa hiyo kuipongeza Benki ya TCB kwani wamekuwa ni watumiaji wazuri, na washiriki wa Soko la Hisa la Dar es Salaam.

Alisema ilikuwa benki ya kwanza kuunganisha mfumo wake wa Kidijiti wa TCB Popote na mfumo wa DSE Hisa Kiganjani, hivyo kuwawezesha wateja wake kuwekeza katika Soko la Hisa moja kwa moja tokea katika mfumo wao wa Kibenki.

“Tunatarajia pia kuwa katika kipindi hiki cha IPO, wawekezaji wataweza kutumia TCB Popote na DSE Hisa Kiganjani kuwekeza katika TCB Stawi Bond.

Mabadiliko na maendeleo yote haya ni muendelezo wa mapinduzi chanya ambayo benki hii imekuwa ikipitia chini ya uongozi wa Mkurugenzi Mtendaji na Afisa Mtendaji Mkuu, Adam Charles Mihayo.

Imani yetu ni kuwa baada ya hatifungani hii, hatua itakayofuata ni kwa TCB kuuza hisa zake kwa umma na kuja kuorodheswa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam,” amesema.