March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Kampeni ya ‘Kila hatua Mixx’ yazinduliwa Kanda ya Ziwa

Na Mwandshi Wetu, Timesmajira Online

KAMPENI mpya ya ‘Kila Hatua Mixx’ imetambulishwa rasmi kwa wakazi wa Kanda ya ziwa katika hafla iliyofanyika jijini Mwanza Septemba 9,2025.

Hiyo ikiwa ni hatua nyingine ya kampuni ya Mixx kuendeleza ujumuishwaji wa kifedha nchini.

Akizungumza katika hafla ya uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Yas kanda ya ziwa, Joseph Mutalemwa amesema kampeni hiyo inalenga kuhakikisha wananchi wa Kanda ya Ziwa, wanapata huduma bora za kifedha, kuimarisha biashara zao, na kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidigitali.

“Mixx imekuwa jukwaa muhimu kwa uchumi wetu kwa miaka 15 sasa, ikiwezesha zaidi ya watanzania milioni 20 kufanya miamala mbali mbali ya kifedha yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 6.

“Kupitia mtandao wetu wa mawakala zaidi ya 200,000, tumeweza kuunda ajira zisizo za moja kwa moja kwa maelfu ya vijana na kutoa suluhisho salama za malipo kwa wafanyabiashara zaidi ya 500,000,” amesema Mutalemwa.

Ameongeza kuwa, mixx ni zaidi ya huduma ya kifedha kwani wamekuwa mshirika wa kifedha mwenye suluhisho za moja kwa moja kwa changamoto za Watanzania.

Kupitia huduma zake bunifu kama Bustisha, Nivusheplus, Kibubu, Lipa kwa Simu, na zinginezo, wanakidhi mahitaji ya kifedha ya kila siku,ikiwemo mikopo ya dharura, uwekaji wa akiba, uwekezaji na malipo salama.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara wa Mixx, James Sumari, amesema:

“Tunapozindua kampeni ya ‘Kila Hatua Mixx’, tunahimiza kujenga mazingira ya kidigitali yenye usawa, salama na rahisi kutumia kwa kila Mtanzania.

“Hii ni safari ya pamoja ya kuyafikia makundi yaliyosahaulika kama wajasiriamali wadogo, wakulima, vijana na akina mama ili waweze kufanikisha malengo yao ya kimaisha na kibiashara,” amesema.

Kampeni ya ‘Kila Hatua Mixx’ inasisitiza umuhimu wa makundi maalim kama vijana na wanawake katika uchumi wa kidigitali, ikiwapa fursa ya kupata huduma za kifedha zinazorahisisha biashara, mikopo, akiba, uwekezaji, na bima.