Na Allan Kitwe,Timesmajiraonline,Tabora
WAKAZI wa Kata ya Ukumbisiganga katika Halmashauri ya Wilaya ya Kaliua Mkoani Tabora kutoka vyama mbalimbali vya siasa wameungana na wana CCM kumpongeza Rais Dkt Samia Suluhu Hassan kwa mambo mazuri aliyowafanyia.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti na mwandishi wa mtandao huu aliyetembelea kata hiyo hivi karibuni walieleza kuwa Kata hiyo ilikuwa imesahaulika na kukosa huduma nyingi za kijamii lakini serikali ya awamu ya sita imewatendea haki.
Edson Kilegea mkazi wa Kijiji cha Usinga na Katibu Tawi wa CCM alisema kuwa wakazi wa Kijiji hicho na Kata nzima wana furaha kubwa kutokana na maboresho ya huduma za kijamii yaliyofanywa na Rais Samia katika kata yao.

Alisema kuwa Kijiji chao kiko umbali wa km 90 kutoka Makao Makuu ya Wilaya na miundombinu ya barabara ni shida sana hali inayopelekea kutofikika kirahisi hivyo kukosa huduma nyingi za kijamii.
‘Tunaishukuru sana serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia kwa kutuboreshea huduma za afya, maji, umeme na mawasiliano na kuacha wananchi waendelee kufanya shughuli zao za kiuchumi, pasipo bughudha yoyote’, alisema.
Mwanachama wa CUF Juma Hemed alieleza kuwa miaka ya nyuma walikuwa wanasumbuliwa sana na kufukuzwa mara kwa mara kwa kuwa Kata hiyo ipo ndani ya hifadhi lakini Rais Samia kwa uungwana wake hajawafukuza hadi sasa.
‘Tunaishi eneo hii tangu miaka ya 1970 hadi sasa, Rais Samia alituma Mawaziri 8 wakaja hapa kuangalia eneo lote, wakasema tuendelee kuishi wakati taratibu zingine zinaendelea kufanyika, katika hili tunamshukuru sana’, alisema.
Kada wa CHADEMA Boniface Nzengo alipongeza kazi nzuri iliyofanywa na Rais Samia katika kata hiyo na Wilaya nzima ya Kaliua na kuwataka wakazi wa Kata hiyo kumpa kura za kishindo kwa kuwa ni Kiongozi anayejali wananchi wake.
‘Hata wapinzani tunatambua kazi nzuri inayofanywa na Rais Samia, hapendi kuona wananchi wake wakiteseka, ameendelea kutambua wanaoishi kwenye maeneo ya hifadhi na kurasimisha makazi yao, naamini hata vijiji vyetu 2 vilivyobakia vya Usinga na Ukumbi Kakoko atavirasimisha’, alisema.
Mwenyekiti wa serikali ya Kijiji cha Usinga, Omari Kalomo alimpongeza Rais Samia kwa kuruhusu kaya zaidi ya 6000 zilizopo katika kata hiyo kuendelea kuishi kwa amani na utulivu, aliahidi kuwa Oktoba 29 watampa kura za kishindo.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako