Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Korogwe
MKUU wa Wilaya ya Korogwe mkoani Tanga William Mwakilema ameliomba Shirika la World Vision Tanzania kuwaongezea nguvu wananchi wa Kijiji cha Ubiri katika ujenzi wa zahanati yao.
Wananchi hao walimueleza Mkuu wa Wilaya kuwa wanapata shida ya kutafuta huduma za afya, ambapo ili mtu aweze kufika Hospitali ya Wilaya ya Korogwe, Magunga, inabidi alipe usafiri wa bodaboda sh. 30,000, na hiyo ni kutokana na ubovu wa barabara na milima kufika Korogwe mjini.
Amesema hayo Septemba Mosi, 2025 alipofika kuzindua Mradi wa vyoo vilivyojengwa na Shirika la World Vision, Mnyuzi AP, Kanda ya Mashariki kwenye Shule ya Msingi Mnyuzi iliyopo Kijiji cha Ubiri, Kata ya Kwagunda.

Mwakilema amesema anaujua mchango wa Shirika la World Vision, kwani pamoja na kujenga vyoo hivyo, pia ilijenga vyumba viwili vya madarasa na ofisi ya walimu kwenye shule hiyo, hivyo anaamini shirika hilo lina uwezo wa kuwasaidia wananchi hao kuweza kukamilisha zahanati yao ambayo kwa sasa ipo hatua ya uchimbaji wa msingi.
“Kwenye kijiji hiki kumekuwa na changamoto ya barabara, umeme kwa baadhi ya vitongoji, maji na zahanati. Lakini kwenye changamoto ya maji na zahanati, nipeleke ombi tena kwa World Vision. Najua wamekuwa wakitusaidia mambo mengi kwenye masuala ya elimu, afya na maji, na hata pale Mnyuzi wametujengea zahanati.
“Lakini kutokana na Kijiji cha Ubiri kuwa pembezoni mwa wilaya, basi muwape umuhimu wa pekee kuweza kuwasaidia ujenzi wa zahanati, ambapo itawapunguzia kwenda umbali mrefu kufuata huduma za afya” amesema Mwakilema, huku wananchi hao wakimpongeza kufika kijijini hapo, kwani tangu alipofika aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Korogwe, Margareth Ndaga mwaka 1995, hakuna mkuu wa wilaya mwingine alifika.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Korogwe Goodluck Mwangomango ambaye nae amefika kijijini hapo tangu Mkurugenzi wa mwisho kufika hapo mwaka 1997, amesema ataangalia uwezekano wa kuongeza walimu hasa wa kike baada ya kuelezwa walimu waliopo hapo ni wanne, huku mwalimu wa kike akiwa mmoja tu, na wakati huo shule ikiwa na wanafunzi 203, wavulana 112 na wasichana 91.
Mratibu wa Mnyuzi AP, Daniel Chuma amesema Kijiji cha Ubiri ni mojawapo ya vijiji vinufaika vilivyo ndani ya eneo la Mradi wa Mnyuzi AP. Kijiji hicho
chenye wakazi 877 na kaya 328, Mradi wa Mnyuzi AP umechangia maendeleo ya ustawi wa watoto katika nyanja mbali mbali katika muda wa uhai wa mradi. Kijiji kimenufaika katika miradi ya kilimo,uchumi,utunzaji wa mazingira, elimu ,afya ,lishe, utetezi na haki za watoto.

“Mojawapo ya miradi mikubwa iliyotekelezwa kwa siku za nyuma ni pamoja na madarasa mawili na ofisi katika Shule ya Msingi Ubiri uliotekelezwa mwaka 2017. Mradi wa Ujenzi wa Vyoo Shule ya Msingi Ubiri ulitokana na uhitaji na changamoto iliyoibuliwa na jamii ambayo ilikuwa ni upungufu wa matundu ya
vyoo katika Shule ya Msingi Ubiri.
Mradi ulianza utekelezaji wa ujenzi wa vyoo hivi Januari, 2025 hadi April 2025 chini ya Mkandarasi Okasseny Engineering Ltd. Baada ya kipindi cha
miezi mitatu ya uangalizi, mradi ulikaguliwa kwa mara ya mwisho na hati kutolewa mwishoni mwa mwezi
wa Agosti.

“Mradi umegharimu jumla ya sh 84,365,634 na kuwanufaisha jumla ya watoto 203 (91 wasichana,112 wavulana). Mradi umejumuisha ujenzi wa matundu manne (4) kwa watoto wa kike, choo cha walemavu na eneo la kujisitiri wakati wa hedhi. Pia mradi umejumuisha ujenzi wa matundu manne (4) kwa wavulana, choo cha walemavu na eneo la haja ndogo kwa wavulana. Miundombinu yote imezingatia makundi yote na haswa walemavu,”amesema Chuma.




More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina