*Yazindua kampeni mkoani Mwanza
*Yaahidi kuleta mabadiliko katika sekta mbalimbali
*Kuunda Serikali inayojitegemea
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Mwanza
CHAMA cha Wananchi (CUF), kimezindua kampeni za Urais kikiahidi kuleta mabadiliko katika sekta za afya, elimu, madini, maji, nishati ya umeme, kodi , ajira na kuondoa kikokotoo .
Pia, itaunda serikali inayojitegemea, itaboresha utawala bora ,huku ikisisitixa kuwa mara baada ya mgombea Urais kuapishwa mchakato wa mabadiliko ya katiba utaanza.

Ahadi hizo zimetolewa na mgombea Urais wa CUF, Gombo Samandito Gombo, Agosti 32,2025,wakati wa uzinduzi wa kampeni za chama hicho, uliofanyika katika uwanja wa Furahisha, Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza
Gombo amesema,endapo CUF ikifanikiwa kushika dola italeta mabadiliko makubwa katika sekta mbalimbali ambapo ili kuondokana na uhaba wa dawa na vifaa tiba, itajenga viwanda vya kuzalisha bidhaa hizo nchini , kwa kutumia rasilimali zilizopo.
Pia, ikipewa ridhaa ya na wananchi huduma za afya katika hospitali za umma zitatolewa bure , hata Mfuko wa Bima ya Afya wa Taifa, wataudhibiti utoe huduma bure kwa wananchi wote.
“Hata bima ya afya hatuitaki maana imekuwa uchochoro wa ufisadi, CUF tutadhibiti mfuko huo kwa kutoa huduma bure kwa wote.Tutajenga viwanda vya kuzalisha vifaa tiba na dawa kwa sababu uwezo tunao, badala ya kutegemea wafadhili,”amesema Gombo.
Kuhusu elimu, mgombea huyo wa Urais wa CUF amesema kuwa, itatolewa bure kuanzia shule za awali hadi chuo kikuu kwa kufuta mikopo ya elimu ya juu, wataimarisha elimu ya ufundi kwa vijana wasome masomo wanayoyahitaji bila kuwashurutisha ili baada ya kuhitimu wajitegemee.
Aidha,Gombo amesema haki ya huduma ya kuunganisha umeme na maji, itahakikisha wananchi wanaipata na itatolewa bure, ambapo watalipia kidogo kidogo, huku akieleza kuwa huduma mbalimbali zitaendeshwa kidijitali.
Pia amesema,huduma hizo zitatolewa bure mara baada ya serikali kujenga setelaiti na minara ya kutoa “WiFi”, ili wananchi wanufaike na huduma hiyo ikiwemo “internet” mijini na vijijini, bila malipo kwa sababu fedha zipo nyingi anafahamu mahali zilipo.
Akizungumzia sekta ya madini, Gombo amesema serikali itakayoundwa na CUF itaboresha sheria ya madini, haitatoa leseni kwa mtu asiye na hati ya umiliki wa ardhi, uchimbaji utafanywa na kampuni za serikali ili kuiwezesha kupata faida ya moja kwa moja.
“Tanzania ni nchi tajiri ya madini ya kipekee , tutabadilisha sheria ili serikali ichimbe madini na kupata faida, hatutafanya uthamini wa ardhi wala mtu ambaye hatakuwa na umiliki wa ardhi wakiwemo wawekezaji hawatarusiwa kuchimba madini,”amesema Gombo.
Vilevile amesema,serikali yake itajenga nyumba milioni mbili ili kuwapatia wananchi makazi bora, wakiwemo askari polisi, na mikopo midogo ya nyumba inayowasumbua watafutiwa wafanye kazi kwa weledi.

Aidha amesema CUF itafuta kikokotoo na kurejesha makato ya watumishi wa umma, watapata stahiki zao na itahakikisha maslahi yao yanaboreshwa ili kudhibiti ufisadi na wizi, endapo mtumishi atabainika kuiba mali ya umma anatalazimika kurejesha na kufukuzwa kazi.
Hata hivyo amesema,serikali atakayoiunda akipewa ridhaa itaziba mapengo ya uhaba wa watumishi kwa kutoa ajira kwa watu wenye ujuzi na taaluma, watapewa hati za viwanja vya kujenga nyumba.
Naye Mwenyekiti wa CUF Taifa, Profesa Ibrahim Lipumba, alidai nchi iko njia panda, imeathiriwa na ufisadi, hali ya maisha imekuwa ngumu, hivyo kutokana na mgombea wa chama hicho kufahamu matatizo ya Watanzania, itaimarisha utawala bora na kudhibit ufisadi.
“Gombo na Mgombea Mwenza Husna Abdallah, watahakikisha rasilimali za nchi zinatumika kuwaletea furaha Watanzania wote, wakiwemo wa Mkoa wa Mwanza,”amesema Lipumba.


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi