December 25, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Ofisa kutoka TASAF akizungumza na baadhi wanufaia namna ya kuanzisha miradi kutokana na fedha wanazopata hivi karibuni mkoani Dodoma.

Wanufaika wa TASAF waishukuru serikali kuwawezesha

Na Zuhura Zukheir,TimesMajira Online,Dodoma

WANUFAIKA wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF), wameishukuru Serikali kwa kuwawezesha kiuchumi kupitia ruzuku wanayopokea, hali iliyowaondolea umaskini uliokithiri katika kaya zao kutokana na kuwa na uhakika wa kuendesha maisha yao na ya familia zao.

Pia wamewashauri wanufaika wengine kuweka akiba, ili ruzuku hiyo iwaondoe kwenye umaskini kama serikali ilivyodhamiria.

Ofisa kutoka TASAF akizunguma na baadhi ya wanufaika kuzingatia fedha wanazopewa kwa kuanzisha miradi.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti,wanufaika hao wa TASAF kutoka Chamwino na Nala walisema awali kabla ya kuingizwa katika mpango huo, walikuwa na maisha magumu kutokana na kuishi katika nyumba za tende huku hali ya lishe na elimu kwa watoto ikiwa ni shida.

Winfrida Mbango ambaye ni mnufaika tangu mwaka 2014 alikiri kuwa TASAF, imemtoa katika umaskini baada ya kuanza ufugaji wa mifugo mbalimbali baada ya kuanza kupokea fedha za ruzuku kutoka katika mfuko huo, ambapo baada ya kuuza mifugo yake alipata zaidi ya sh. milioni 2 zilizomfanya ainuea nyumba ya vyumba viwili pamoja na kuingiza maji nyumbani kwake.

Amesema mafanikio mengine aliyoyapata kupitia TASAF ni pamoja na kufungua mradi wa duka, ufugaji wa kuku na kusuka umeme katika nyumba yake kutokana na fedha zilizopatikana, baada ya kuuza mifugo yake iliyotokana na ruzuku za TASAF.

Mkazi mwingine wa Kijiji cha Nala katika Halmashauri ya Jiji la Dodoma, Paulina Nzengo amesema baada ya kupata ruzuku kutoka TASAF alianza kufuga mbuzi baadaye aliwauza na kuanza ujenzi wa nyumba ambayo ndiyo anaishi kwa sasa.

Amesema mwanzoni alianza kupokea ruzuku isiyopungua 30,000, lakini kutokana na kuuchukia umaskini alilazimika kuziwekeza fedha hizo katika biashara ya viazi vya kukaanga na faida yake kuiweka kwenye kibubu na baada ya kupata ruzuku ya mara ya pili, alichanganya fedha hizo na kununua mbuzi wawili ambao ni jike na dume.

Mnufaika huyo amesema baada ya muda, mbuzi hao walizaliana na kisha kuwauza na ndipo alipoamua kuinunua nyumba ya vyumba vitatu pamoja, choo bora na kuwekeza katika chakula ambapo kwa sasa maisha yake, yameimarika kwa kuwa anaishi pazuri na ana uhakika wa kupata chakula.

Paulina amewataka wanufaika wengine wajitahidi kuweka akiba, ili wafanye mambo ya maana ili hata mradi utakapoisha wawe na miradi endelevu itakayowasaidia wao na jamii inayowazunguka.