March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Vijana waaswa kutumia mfumo wa NeST 

*Ili waweze kunufaika na asilimia 30 ya zabuni za Serikali 

*PPRA yaeleza kuwa ni mfumo wenye uwazi

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online – Mwanza

Serikali kupitia Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2023, imeelekeza kuwa taasisi zote za umma zitenge asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya makundi maalumu ambayo ni pamoja na vijana, wanawake, wazee na watu wenye ulemavu.

Akizungumza na Timesmajira Online katika banda la Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA), kwenye kongamano la vijana lililofanyika uwanja wa Nyamh’ongolo, wilayani Ilemela mkoani Mwanza, Ofisa wa PPRA Kanda ya Ziwa, Jabiry Bane, amewahimiza vijana wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela na maeneo mengine nchini kuunda vikundi rasmi na kujisajili kupitia mfumo wa NeST ili waweze kunufaika na fursa hiyo ya asilimia 30.

Ofisa PPRA Kanda ya Ziwa Jabiry Bane

“Kikundi lazima kiwe na shughuli maalum,katiba na wanachama wasiopungua watano na wasiozidi ishirini. Baada ya kusajiliwa Halmashauri, taarifa ya kikundi itawasilishwa PPRA kwa ajili ya kusajiliwa rasmi kama kikundi maalum na hivyo kuanza kufaidika na asilimia 30 ya zabuni za Serikali,” amesema Bane.

Kwa mujibu wa Bane,mfumo wa NeST umeainisha mgawanyo wa asilimia 30 kwa makundi maalumu ambapo vijana wanapatiwa asilimia 10, wanawake asilimia 5, wazee asilimia 5, na watu wenye ulemavu asilimia 10.

“Kila taasisi ya umma inapaswa kutenga asilimia 10 ya bajeti ya ununuzi kwa ajili ya vijana.Hivyo  vijana tuamke, tusidanganywe kwamba tunaweza kupata zabuni bila kupitia NeST. Mfumo huu ndio unaoratibu mchakato mzima wa zabuni na hakuna upendeleo wowote,”amesisitiza Bane.

Bane amebainisha kuwa mfumo wa NeST umeainisha vipengele vinne vikuu ambavyo vijana na makundi maalumu wanaweza kujiunga navyo ili kushiriki kikamilifu katika zabuni  ikiwemo usambazaji wa bidhaa.

“Vijana wanaweza kujisajili kuuza au kusambaza bidhaa mbalimbali kama vifaa vya ujenzi,”.

 Pia vijana wanaweza kujusajili kwa ajili ya kutoa huduma mbalimbali kama vile chakula,usafi, ujenzi na huduma nyingine zinazotolewa na vikundi Huduma za ushauri elekezi  kwa  wataalamu waliobobea katika taaluma mbalimbali kama uandishi, usimamizi wa miradi na kadhalika pamoja na huduma za kiufundi na kitaalamu ikiwemo uandishi.

Ofisa PPRA Kanda ya Ziwa Jabiry Bane kulia akifafanua jambo kwa mmoja wa wananchi waliotembelea banda lao katika kongamano la vijana Nyamh’ongolo wilayani Ilemela mkoani Mwanza

Sanjari na hayo Bane,amesema mfumo wa NeST umeleta mabadiliko katika ununuzi wa umma kwa kuongeza uwazi, thamani ya fedha, na kupunguza mianya ya rushwa. Pia, umechangia katika kutatua changamoto ya ajira, kwani vijana wengi wameweza kujiajiri kupitia fursa hizo.

Kwa upande wake Ofisa Mtendaji mtaa wa Mtakuja Kata ya Nyamh’ongolo,Wilson Ntahondi,atawahamasisha wananchi WA mtaa huo hususani vijana kusajili vikundi vyao na kuweza kupata fursa ya kujiajiri kupitia mfumo wa NeST.

Ofisa Mtendaji WA mtaa wa Mtakuja Kata ya Nyamh’ongolo Wilson Ntahondi