March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wagombea Ubunge 16 wa vyama mbalimbali kuchuana  Ilemela 

*Huku wagombea 69 ngazi ya Udiwani kupeperusha bendera ya vyama vyao

Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Jumla ya wagombea 16  kutoka vyama mbalimbali wameteuliwa kugombea nafasi ya Ubunge  katika Jimbo la Ilemela mkoani Mwanza huku wagombea 69 wa ngazi ya Udiwani wakiteuliwa kushiriki katika kinyang’anyiro cha nafasi hiyo kwa Kata 19, zilizopo jimboni humo.

Ambapo vyama 16 vya siasa ambavyo wagombea wake wameteuliwa  ni  CCK, DP, NLD, AAFP, SAU, MAKINI, UMD, N.R.A, ACT, UPDP, UDP, CUF, NCCR-MAGEUZI, ADC,CCM na  CHAUMMA.

Akitoa taarifa  Agosti 28, 2025, ofisini kwake,Msimamizi wa Uchaguzi Jimbo la Ilemela,Herbert Bilia, amesema wagombea  17,walifanikiwa  kuchukua   fomu za uteuzi kwa ngazi ya Ubunge,kati yao 16 walifanikiwa kurejesha fomu hizo huku mmoja akishindwa kurejesha.

“Mmoja hakuteuliwa na hii imetokana na kuwa mgombea huyo kutoka chama cha  ADA -TADEA hadi kufika saa 10 jioni  Agosti 27, 2025 muda wa uteuzi hakuwa amerejesha fomu,hivyo kukosa sifa ya kuteuliwa,”amesema Bilia.

Bilia amesema,kwa upande wa ngazi ya Udiwani jumla ya wagombea 81 waliochukua fomu za uteuzi kati yao 69 walifanikiwa  kurejesha fomu  hizo na kuteuliwa kupeperusha bendera ya vyama vyao katika uchaguzi  mkuu kwa nafasi hiyo huku wagombea 12 wakishindwa kuteuliwa kutokana na sababu kuu mbili.

Ametaja sababu hizo kuwa  ni mgombea mmoja alikosa wadhamini huku wagombea 11 hawakuteuliwa kutokana na  kutokurejesha fomu hadi muda wa uteuzi ulipofika ambao ni saa 10 jioni   Agosti  27,2025.

Pia amesema,kwa mujibu wa kalenda ya uchaguzi mkuu wa Rais,Wabunge na Madiwani, Agosti 28,2025 kampeni zinaanza nchi nzima,hivyo amewahimiza  wananchi kujitokeza katika kampeni hizo ili kusikiliza sera za wagombea na kuweza kufanya maamuzi sahihi.Huku akiwasihi wagombea kufanya kampeni  kwa kufuata sheria, taratibu na kanuni kama ilivyoelekezwa.

“Kwani uchaguzi ni nyenzo muhimu ya kutupatia viongozi wa kutusaidia kudumisha amani,utulivu na kutuletea maendeleo,”amesema Bilia.