March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

0-4064x3074-0-0#

Wafanyabiashara wa samaki,mama lishe waomba majiko makubwa ya nishati safi

*Walia na moshi kutokana na matumizi ya nishati ya kuni

*Waeleza namna moshi unavyofukuza wateja

*Wakazi wa Kitangiri,Kirumba waguswa na  kampeni ya Pika Smart, 

*Waeleza  kila siku wanatumia mkaa wa Tsh 15,000

*Wasisitiza elimu zaidi iwafikie wengi

Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza 

Wafanyabiashara wa samaki na mama ntilie( mama lishe),wa Kata za Kitangiri na Kirumba, wilayani Ilemela mkoani Mwanza,wameiomba  Serikali kuwatengenezea majiko makubwa ambayo yatapatikana kwa gharama nafuu yanayotumia nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme ili waweze kuyatumia katika biashara zao na kuepukana na changamoto ya moshi.

Hii ukiwa ni kuunga mkono mpango wa Serikali wa kuhakikisha ifikapo 2034, watanzania asilimia 80 wawe wanatumia nishati ya safi ya  kupikia huku wakiepuka madhara yanayotokana na matumizi ya nishati za kuni na mkaa.

Mhamasishaji wa nishati safi ya kupikia kutoka shirika la Nishati la Maendeleo TaTEDO-SESCom Dora Urio( kushoto), akitoa elimu ya nishati safi ya kupikia kupitia nishati ya umeme kwa mama ntilie wa mara wa Medical Research Kata ya Kitangiri Salome Marco,anayesonga ugali,kupitia kampeni ya pika smart

Wamebainisha hayo Agosti  21,2025,wakati  wa utoaji wa elimu na uhamasishaji  wananchi  juu ya matumizi   nishati ya safi ya kupikia ikiwemo  nishati ya umeme kwa Kata hizo mbili,kupitia kampeni ya pika smart,nishati safi ya kupikia oko maisha na mazingira  inayoratibiwa na Serikali ya Tanzania kupitia Wizara ya Nishati kwa kushirikiana na shirika la Modern Energy Cooking Services(MECS)   pamoja na shirika la kimataifa la Maendeleo  la Marekani(UK Internation Development).

Rose Zakaria mfanyabiashara  wa samaki soko la Kishimba Kata ya Kirumba wilayani Ilemela,amesema,wanatumia nishati ya kuni kukaanga samaki huku wakikabiliwa na changamoto ya moshi mwingi,unaowasababishia madhara ikiwemo macho na kuwapa usumbufu wateja wao.

“Moshi ni tatizo unachangia wateja kukimbia wengine wananuna,pia unatusababishia macho kuuma kuwa mekundu na kuvimba,na hofu yetu miaka ikienda tunaweza kuitwa wachawi na kukutwa na madhira waliokuwa wanapitia wazee ya kuitwa wachawi na kuuawa,” amesema Rose na kuongeza:

“Kutokana na kazi ninayofanya ya kungaa samaki kwa kutumia kuni moto wake unakuwa mkali hivyo  joto la mwili nalo linakuwa juu ukichanganya na moshi nalazimika kwa siku nakunywa  maji lita 5 ambayo ni ya baridi lakini yakiwa ya kawaida nalazimika kunywa maji lita 10 kwa siku,”.

Amesema,kwa sasa majiko yaliyopo ya umeme ni kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na siyo ya biashara hivyo,ameomba Serikali kuyaboresha na kuwaletea majiko hayo yakiwa mamkubwa ili wafanyabiashara  ikiwemo wanaokaanga samaki waweze kunufaika na nishati hiyo ya umeme na nishati nyingine  safi za kupikia.

Salome Marco ni mamantilie wa mtaa Medical Research,amesema,katika biashara hiyo kwa siku anatumia mkaa wa Tsh.15,000 na wakati mwingine fedha hiyo inazidi kwa sababu wanapika vyakula vingi kuanzia asubuhi hadi jioni,hivyo kupitia  elimu alioipata ameweza kutambua matumizi  ya nishati ya umeme ni nafuu kulingana na chakula wanachokipika pia inaokoa muda.

“Nimebandika sufuria la ugali saa nne asubuhi nakuja kuivisha saa sita mchana, kwenye umeme naweza kutumia saa moja kumaliza kila kitu na inawezekana isiishe.Changamoto hatuna uwezo wa kununua majiko hayo au kutumia nishati ya gesi,tunaiomba Serikali itusaidie kutupunguzia gharama au yatolewe kwa mkopo,”.

Naye Amina Jumanne mkazi wa Bwiru Bima,amesema huwezi kununua mkaa wa shilingi 1,000 ukapika makande yakaiva  lakini kwenye jiko hili unaweza kupika na yakaiva na bado ukawa kwenye matumizi mazuri ya fedha.

“Tunaiomba Serikali ituletee majiko haya na ipunguze bei ili na sisi wananchi wa hali ya chini tuweze kutumia japo kuwa sisi tunaweza kushirikiana na akina mama kwenye vikundi au majirani  tukachangiana na kucheza mchezo na baada ya muda mtu mmoja mmoja au wawili wawili wakapata jiko,”.

Maria Chacha, mfanyabiashara wa samaki soko la Kishimba Kata ya Kirumba,amesema majiko hayo ya nishati ya umeme yana faida nyingikwanu yanaokoa muda na gharama ukilinganisha na mkaa,hivyo ameomba Serikali ifanye jitihada ya kusambaza na kuitangaza huduma hiyo ili ifike maeneo mengi nchini hasa vijijini.

“Madhara tunayoyapata kutokana na matumizi ya kuni kwenye biashara zetu ni macho kuuma saa zote kutokana na moshi, na unapofika muda wa kulala ukifumba tu macho yanaanza kuuma yakishatoa machozi unapata unafuu kidogo,kwa sasa tuna pata madhara sana hatujui huko mbeleni yatakuwaje,”.

Emmanuel Bamba,mkazi wa Kitangiri,amesema  majiko yanayotumia nishati safi yanawasaidia  watu wenye kipato cha chini,hivyo elimu itolewa juu ya namna ya kutumia majiko hayo ili watu wawe na uelewa mpana na yasije sababisha   majanga.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa mtaa wa Medical Research Yudas  Hume,mwamko wa wananchi kuchangamkia fursa  ya  nishati safi ya kupikia ikiwemo  ya umeme upo,lakini changamoto ni ukosefu wa elimu na gharama za maisha,endapo majiko hayo  yatapatikana kwa  gharama nafuu matumaini yake kila mwananchi atapenda kutumia.

“Naishukuru Serikali  kwa hiki inachokifanya,wakati wa nyuma tulikuwa tunatumia kuni na mkaa lakini kwa ujio huu utaenda kutupunguzia gharama za maisha.Kwenye mtaa wangu nina kaya zaidi 800 na watu wasiopungua 22,000,elimu  tulioipata itatusaidia tuondokane na maisha duni,mama ntilie watafanya kazi zao vizuri huku wa kina mama wa nyumbani maisha yao yatakuwa bora,”.

Mmoja wafanyabiashara wa samaki soko la Kishimba Mwaloni akizungumza adha wanayoipata kutokana na matumizi ya nishati ya kuni

Mwenyekiti wa soko la Kishimba Mwaloni, Khalid Masesa,amesisitiza  zaidi elimu ya majiko ya nishati safi ya kupikia ikiwemo umeme na gesi itolewe kwa  wafanyabiashara ili kupunguza hatari ambayo imekuwa ikilikumba soko hilo kwa kuuungu baada ya mtu kuhisi amezima moto kumbe haujazimika.

Mhamasishaji wa nishati safi ya kupikia  kutoka shirika la  Nishati la Maendeleo TaTEDO-SESCom Dora Urio,amesema wapo Mwanza kwa ajili ya kampeni hiyo ili kuhakikisha wananchi wote waweze kutumia vifaa ambavyo vimeboreshwa na  vinatumia nishati safi.

Hali itakayosaidia  Serikali ya Tanzania kutimiza lengo la  ifikapo 2034 asilimia 80 ya watanzania wawewanatumia  nishati safi kupikia ambalo kwa sasa hivi ni asilimia 20  ya watanzania wanatumia nishati safi.

“Mwitikio Mwanza ni mkubwa kwa sababu watu wengi  wanafuatilia kujua zaidi,kwa siku tunaweza kuhamasisha watu zaidi ya 100,huku wengine wanaomba wanasema kama serikali inaweza kusaidia wakapewa kwa mkopo,

maoni ambayo inatakiwa tuyawakilishe ili yaweze kufanyiwa kazi kwa sababu wananchi wengi wanataka lakini wanaomba wapate kwa mkopo,hivyo Serikali inapaswa kuweka ruzuku kwenye majiko haya ili yauzwe kwa bei nafuu na kila mtu aweze kumudu gharama,”amesema Urio.

Urio amesema,mikakati yao  ni kutoa elimu kubadili mitazamo ya wananchi  ili watambue nishati ya  umeme ni rahisi na gharama nafuu.Kwani utafiti ambao wamefanya kwenye  majiko hayo  kwa  milo mitatu siku nzima mtu anaweza kutumia shilingi mia mbili mpaka mia saba,lakini wakati wanazunguka mtaani kutoa elimu wananchi wengi hususani wafanyabiashara waliwaekeza kuwa kwa siku wanaweza kutumia mkaa wa shilingi 15,000.

Mhamasishaji wa nishati safi ya kupikia kutoka shirika la Nishati la Maendeleo TaTEDO-SESCom Dora Urio,akitoa elimu juu ya namna majiko yanayotumia nishati ya umeme yanavyofanya kazi kwa baadhi ya wananchi walijitokeza katika kampeni ya pika smart soko la Kishimba Mwaloni