Kila hatua Mixx yazinduliwa Dodoma
Na Mwandishi Wetu Timesmajira Online
KAMPUNI ya huduma za kifedha kwa njia ya simu, Mixx, imeendelea na mpango wake wa kusogeza karibu huduma za kifedha za kidigitali kwa kuzindua kampeni ya Kila Hatua Mixx jijini Dodoma.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha wakazi wa Kanda ya Kati wanapata nafasi sawa ya kushiriki katika uchumi wa kidigitali na kunufaika na huduma rasmi za kifedha.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Biashara wa Mixx, James Sumari amesema Safari ya Mixx ilianza mwaka 2010 ikiwa na ndoto moja kubwa, kuhakikisha kila Mtanzania anapata fursa ya kushiriki kikamilifu katika huduma za kifedha.
“Miaka 15 baadaye, ndoto hii imekua na kuleta suluhisho kubwa la kifedha linalowaongoza mamilioni ya Watanzania kuelekea kwenye uchumi wa kidigitali.

“Kupitia Dodoma na Kanda ya Kati, tunataka kuhakikisha ndoto hii inamgusa kila kijana, kila mfanyabiashara na kila familia,” amesema Sumari.
Amesema, kwa sasa, zaidi ya Watanzania milioni 20 hutumia huduma za Mixx kila mwezi, wakifanya miamala yenye thamani ya takribani shilingi trilioni 6.
Aidha, amesema mtandao wa mawakala 200,000 umefungua fursa za ajira na kipato kwa maelfu ya vijana nchini.
Hata hivyo amesema kwa Kanda ya Kati, Mixx tayari inahudumia maelfu ya wateja na mamia ya wafanyabiashara wadogo kwa wakubwa, huku ikilenga kuongeza ushirikishwaji wa kifedha hata katika maeneo ya pembezoni na vijijini.

Kupitia kampeni ya Kila Hatua Mixx, kampuni inaleta suluhisho bunifu na rafiki zinazowawezesha Watanzania kusimamia maisha yao ya kifedha kwa urahisi zaidi. Miongoni mwa bidhaa hizo ni:
• Bustisha – Mkopo wa muda mfupi kuhakikisha miamala inakamilika pale salio linapokosekana.
• Nivushe Plus – Mkopo wa papo kwa hapo kusaidia dharura, biashara au malengo binafsi.
• Kibubu – Zana ya kidigitali ya kuweka akiba kwa urahisi ili kufanikisha mipango ya kifedha.
• Lipa kwa Simu – Huduma ya malipo ya kielektroniki kwa wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Kati, Bw. Said Idd, amesema uzinduzi wa Dodoma unaashiria dhamira ya kweli ya Mixx kuhakikisha kila Mtanzania anaguswa na mageuzi ya kifedha ya kidigitali.

“Kupitia kampeni ya Kila Hatua Mixx, tunaleta suluhisho la kifedha litakalowawezesha vijana, wanawake na wafanyabiashara wadogo wa Kanda ya Kati kusonga mbele. Hii ni fursa ya kukuza uchumi shirikishi unaoangazia wananchi wote bila kubagua,” amesema Idd.
Mbali na uzinduzi huo, hafla hiyo ilihusisha pia majadiliano ya kitaalam kuhusu ‘Nafasi ya huduma za kifedha kidigitali katika kujenga taifa lenye uchumi imara na shirikishi’.
Mixx imesisitiza kujenga ushirikiano na taasisi za kifedha, wafanyabiashara na jamii za Kanda ya Kati ili kuhakikisha kampeni hii inaleta matokeo chanya ya muda mrefu.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako