*Ni wakati wakienda kuonesha Askari Polisi walipoficha kichwa cha marehemu
*Askari wawili wajeruhiwa katika tukio hilo wakijaribu kuwazuia wananchi
Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Watuhumiwa wa mauaji ya kijana mmoja ambaye hakutambulika jina kwa wakati huo ambaye aliuwawa na kiwiliwili chake kikiwa kimetenganishwa na kutelekezwa
bila kichwa chake,wameuwawa na wananchi wenye hasira kali.
Tukio hilo la kuuwawa watuhumiwa hao lilitokea wakati wakienda kuwaonesha Askari wa Jeshi la Polisi,kichwa cha marehemu huyo pamoja na mali zake walizompora,ndio kundi la wananchi waliopata taarifa waliwavamia na kuanzia kuwashambulia.
Akizungumza jijini hapa Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza,Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP),Gideon Msuya, Agosti 9,2025,jeshi hilo lilitoa
taarifa ya kuanza uchunguzi na kuwasaka watu waliohusika na mauaji ya kijana mmoja, jinsia ya kiume ambaye wakati huo hukuweza kutambuliwa jina wala anuani ya makazi yake, ambaye alikutwa akiwa ameuawa huku kiwiliwili chake kikiwa kimetenganishwa na kichwa chake kwa kukatwa na kitu chenye ncha kali (panga).
Ambapo kiwiliwili hicho kilitelekezwa mtaa wa Malimbe, Kata ya Luchelele, Wilaya ya Nyamagana, kando ya barabara ya Luchelele huku kichwa cha mwili huo hakikujulikana kwa wakati huo kilipo na sababu za mauaji hayo hazikufahamimka.
SACP.Msuya, amesema,baada ya ufuatiliaji wa kina, kijana huyo aliweza kutambuliwa kuwa ni Dickson Yusuph(24), dereva bodaboda, na mkazi wa mtaa wa Shadi, kata ya Luchelele.
Hivyo kupitia msako wa jeshi hilo kwa kushirikiana na wananchi lilifanikiwa kuwakamata watuhumiwa wawili ambao ni Oscar Emmanuel(20) na Edwin Bujuel(22),wote wakazi wa Shadi, Kata ya Luchelele.
Amesema baada ya mahojiano walikiri kuhusika na mauaji ya kijana huyo na kulisaidia Jeshi la Polisi kuonesha mahali walipoficha kichwa pamoja na mali nyingine za marehemu ambazo ni pikipiki yenye namba za usajili MC 715 ENN aina ya TVS rangi vyeusi na simu ya mkononi aina ya INFINIX HOT 10,mali za walizokuwa wamempora marehemu kabla na baada ya kutekeleza mauaji hayo.
“Baada ya mahojiano ya kina imethibitika kuwa chanzo cha mauaji ya Dickson,ni wivu wa mapenzi kwa watuhumiwa kumtuhumu marehemu kuwa na uhusiano wa kimapenzi na mke wa Oscar Emmanuel aitwaye Neema Marwa, (17), na mkazi wa mtaa wa Shadi, kata ya Luchelele,”.
Sanjari na hayo SACP.Msuya, amesema wakati watuhumiwa wanaonesha mali za marehemu Dickson ndani ya msitu wa Nsumba, lilijitokeza kundi la wananchi waliopata taarifa ya kukamatwa kwa watuhumiwa hao na kuanza kuwashambulia Askari Polisi pamoja na watuhumiwa hao.
Ambapo amedai kuwa askari walijitahidi kuzuia wananchi wasiwashambulie watuhumiwa huku wakiepusha kutokea kwa madhara makubwa kwa watu wengi walikuwa wamekusanyika kushuhudia tukio hilo, endapo wangetumia nguvu kubwa ya silaha za moto walizokuwa nazo.
Amesema katika purukushani hizo watuhumiwa wote wawili waliuawa na wananchi wenye hasira na waliojichukulia sheria mikononi.
“Na askari wetu wawili walijeruhiwa na kukimbizwa Hospitali kwa matibabu. Miili ya marehemu hao imehifadhiwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa ajili ya kutambuliwa na kufanyiwa uchunguzi,”amesema SACP.Msuya na kuongeza:
“Kichwa cha marehemu Dickson pia kimehifadhiwa chumba cha kuhifadhia maiti kilichopo hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando kwa ajili ya uchunguzi na utambuzi na mali za marehemu zikiwemo pikipiki MC 715 ENN aina ya TVS rangi vyeusi na simu ya mkononi aina ya INFINIX HOT 10 vimepetikana na tunaendelea na taratibu za kisheria,”.
Hata hivyo amesema chanzo cha tukio hilo ni wananchi kujichukulia sheria mikononi na jeshi hilo linawasaka wahalifu waliojichukulia sheria mikononi kwa kuwaua watuhumiwa hao na kuwajeruhi Askari Polisi wawili ili waweze kuchukuliwa hatua za kisheria.
 “Tunatoa onyo kali na hatutasita kuchukua hatua za kisheria kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kujichukulia sheria mikononi, ikiwemo kuwaadhibu na hata kuwaua watu wanaowatuhumu kutenda makosa badala ya kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,”.

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro