Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, kupitia huduma yake ya kifedha Mixx by Yas, imeendeleza kampeni ya “Vuna na Mixx” kwa kuwazawadia wakulima wa Kanda ya Ziwa wanaotumia huduma za Mixx by Yas kupokea na kufanya malipo ya shughuli zao za kilimo.
Zawadi zilizokabidhiwa ni pamoja na pikipiki, baiskeli, simu, fedha taslimu, na pembejeo za kilimo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, ameupongeza mchango wa Yas na Mixx by Yas katika kuimarisha sekta ya kilimo nchini.

“Huduma za kifedha kama hizi ni nyenzo muhimu katika kumuinua mkulima kutoka kipato cha kujikimu hadi kipato cha kimaendeleo.
“Natoa wito kwa wakulima wote kujiunga na AMCOS na kuhakikisha malipo yao yanafanyika kupitia Mixx by Yas ili kunufaika na fursa hizi,” amesema Mtanda.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Ziwa, Joseph Mutalemwa, amesema zaidi ya miaka sita, Mixx by Yas imekuwa mshirika wa karibu wa AMCOS katika kuhakikisha malipo ya wakulima yanafanyika kwa usalama, uharaka na ufanisi.
“Kwa Kanda ya Ziwa pekee, tumefanikisha malipo ya takribani shilingi bilioni 1.8 kwa wakulima kupitia mfumo wa kidijitali wa Mixx.
” Kampeni ya Vuna na Mixx inalenga sio tu kutoa zawadi, bali pia kuimarisha maisha ya wakulima kwa kuwapatia huduma muhimu kama mikopo nafuu kupitia KilimoPesa na bima ya afya kupitia Afya Mkulima,” amesema Mutalemwa.
Kampeni ya mwaka huu inalenga kuwazawadia wakulima takribani 2,000 zawadi mbalimbali ikiwemo pikipiki, fedha taslimu, simu, friji, TV na pembejeo za kilimo, huku wakulima 1,050 wakipata bima ya afya ya mwaka mzima kupitia mpango wa Afya Mkulima.
Mutalemwa ameongeza kuwa, kampuni inapanua huduma zake kwa kuanzisha hivi karibuni bima ya mazao, ikilenga kupunguza hatari za kifedha kwa wakulima kutokana na changamoto za mabadiliko ya hali ya hewa na majanga ya asili.
Baadhi ya wakulima wanaotumia huduma ya kutuma na kupokea pesa kupitia Mixx by Yas wameishukuru kampuni ya Yas kwa kutambua mchango wa wateja wake na kuwazawadia vifaa vya thamani katika maonesho ya Nanenane yaliyofanyika kwenye viwanja vya Nyamhongolo jijini Mwanza.
Katika hafla hiyo, Philipo Kahigwa, mkulima kutoka Muleba, alipokea simu janja; Mageme Gimbuya, mkulima wa Itilima – Simiyu, alijinyakulia pikipiki; Innocent Lazaro, mkulima kutoka Kagera, alizawadiwa baiskeli; na Sekundakokugonza Audax, mkulima mama kutoka Kagera, alipata pikipiki.

Wakulima hao wamesema, zawadi walizopata zitakuwa msaada mkubwa katika shughuli zao za kilimo na biashara, kwani simu janja itawawezesha kupata taarifa za bei za mazao na kuwasiliana na wateja kwa urahisi, huku baiskeli na pikipiki zikirahisisha usafirishaji wa mazao kutoka shambani hadi sokoni kwa haraka na gharama nafuu.
Aidha, wameeleza kuwa hatua ya Yas kuwazawadia ni uthibitisho kwamba kampuni hiyo inathamini wateja wake, jambo linalowapa sababu ya kuendelea kuamini na kutumia huduma za Mixx by Yas kwa kutuma na kupokea pesa kwa usalama, haraka na kwa gharama nafuu.
Kwa mujibu wa takwimu za FinScope Tanzania 2023, ni asilimia 4 tu ya wakulima wadogo nchini wanaopata huduma rasmi za kifedha kama mikopo na bima. Yas kupitia Mixx by Yas inalenga kuziba pengo hilo kwa kutoa huduma nafuu, salama na zinazolenga moja kwa moja mahitaji ya mkulima.

More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro