March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

CCM kufanya harambee kukusanya bilioni 100 za kampeni

Na Agnes Alcardo, Timesmajira
Online

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM), kesho kinatarajia kufanya harambee ya kitaifa, kwa ajili ya kuchangisha kiasi cha bilioni 100,zitakazo saidia kampeni za chama hicho, zinazotarajiwa kuanza Agosti 28,2025.

Harambee hiyo ya kitaifa iliyopangwa kufanyika Agosti 12,2025,majira ya jioni katika ukumbi wa mikutano wa Mlimani City jijini Dar-es-Salaam.

Hayo yameelezwa Agosti 11,2025,na Katibu Mkuu wa CCM, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, katika mkutano wake na Wahariri na Waandishi wa Habari waandamizi, huku akiwakaribisha wanachama wa CCM, wadau na wananchi wote wenye mapenzi na chama hicho kuweza kuchangia kiasi chochote.

“Tunaelekea katika uchaguzi mkuu na kabla ya uchaguzi kuna kampeni, hivyo kama tunavyojua kuwa kampeni huwa zinahitaji maandalizi ya hali ya juu ikiwemo kuandaa magari,tumeona kesho tufanye harambee ya kuchangisha fedha kutoka kwa watu mbali zitakazoenda kusaidia katika shughuli zote za kampeni,”amesema Nchimbi.

Balozi Nchimbi, ambaye pia ni Mgombea Mwenza wa CCM, amesema, mgeni rasmi katika harambee hiyo, atakua Mwenyekiti wa chama hicho Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.Samia Suluhu Hassan.

Amesema hadi sasa chama hicho kina zaidi ya wanachama milioni 13 waliosajiliwa kidigitali na kwamba harambee hiyo iko wazi hata kwa vyama vingine vya siasa kuchangia.

Aidha,amewatoa wasiwasi wananchi kuwa, chama hicho kitahakikisha kinapokea fedha za michango zenye kulenga kuunga mkono juhudi za chama na si vinginevyo.