Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Waandishi wa Habari nchini,wametakiwa kuzingatia maadili,miiko na kufuata sheria,kanuni na miongozo katika kuandika na kuripoti habari za uchaguzi mkuu unaotarajia kufanyika Oktoba mwaka huu.
Huku wakihimizwa kuzingatia usawa kwa vyama vyote vya siasa,kuepuka rushwa na kuzingatia sheria ya ulinzi wa taarifa binafsi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika na kumalizika salama bila ya kuvuruga amani ya nchi.

Wito huo umetolewa Agosti 7,2025,na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza,Said Mtanda,katika semina ya siku moja kwa waandishi wa habari,watangazaji na Askari wa Jeshi la Polisi kuelekea uchaguzi mkuu kutoka mikoa ya Mwanza, Simiyu, Shinyanga,Kagera,Mara,Geita na Kigoma,iliofanyika jijini Mwanza.
Mtanda amesema, vyombo vya habari vilisaidia katika harakati za Tanganyika kudai uhuru,hivyo ni muhimu hasa katika kipindi hiki cha kuelekea kwenye uchaguzi,hivyo waandishi wa habari wakitumia kalamu vizuri itakuwa na manufaa kwa taifa lakini wakitumia vibaya ni hatari.
“Wakati wa kampeni na uchaguzi, waandishi mnawajibu wa kulinda usalama wenu,wa vyombo vyenu na jamii kwa ujumla kwa kuripoti taarifa sahihi na kuepuka rushwa na kuhakikisha mnafuata sheria, miongozo na maadili ili msiingie kwenye matatizo,”amesema Mtanda.
Meneja wa Huduma za Utangazaji kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA),Mhandisi Andrew Kisaka,amesema waandishi wa habari wana wajibu wa kutoa elimu kuhusu uchaguzi pamoja na kuelimisha umma mwenendo wa kampeni huku akionya kuwa hawapaswi kujumlisha matokeo na kuyatangaza ambayo hayajatolewa na mhusika kwa mujibu wa sheria.
Mhandisi Kisaka,amewaasa,waandishi kutoweka maoni binafsi wakati anachapisha au kutangaza uchaguzi huku katika midahalo wahakikishe wadau wa vyama vyote wanatendewa haki kwa kupewa fursa na muda sawa.
“Waandishi zingatieni katika kipindi cha kampeni na uchaguzi mjikite kutangaza na kuhabarisha umma juu ya sera za vyama vya siasa na wagombea na siyo umbea,kashfa na matusi.Someni na kuzingatia sheria,kanuni na miongozo ya uchaguzi,”.
Pia amesema, vyombo vya habari vya mtandaoni vimekuwa chanzo kikuu cha upotoshaji kutokana na mashindano ya kupata watazamaji wengi hivyo amewahimiza waandishi wa habari kuhakiki taarifa kabla ya kuzitangaza au kuchapisha.

Kwa upande wake Msemaji wa Jeshi la Polisi DCP.David Misime amesema,ni wajibu wa waandishi wa habari na Polisi wa kulinda usalama wakati wa uchaguzi kwa kuheshimu na kuthamini taaluma ya kila mmoja,kutambua na kuheshimu mipaka ya majukumu ya kila mmoja wakati wa kutekeleza wajibu wao.
“Waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kutunza na kuhamasisha amani,utulivu na usalama katika kipindi cha uchaguzi,kujiepusha kuandika au kuchapisha taarifa za uongo na uchochezi na sisi Jeshi la Polisi tutatekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia misingi ya haki, sheria na weledi ili kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa amani na utulivu,”amesema DCP.Misime.
Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano wa Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi(PDPC),
Inocent Mungy, amewataka waandishi wa habari kuhakikisha katika kipindi cha uchaguzi wanazingatia ulinzi wa taarifa binafsi na faragha za wagombe na wajikite katika mambo ya msingi na siyo binafsi pamoja na kuwa makini na matumizi ya Akili Unde(AI).
Haya hivyo katika semina hiyo iliondaliwa na Idara ya Habari Maelezo,,Bodi ya Ithibati ya Waandishi wa Habari,TCRS na Jeshi la Polisi.
Huku mada mbalimbali ziliwasilishwa ikiwemo mwongozo wa waandishi wa habari katika uandishi wa habari za uchaguzi na wajibu wa waandishi wa habari na Jeshi la Polisi katika kulinda usalama.




More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi