Na Raymond Mushumbusi
WATANZANIA wanahitaji mambo kadhaa kuhakikisha wanaishi maisha yanayoendana na haki, mazuri yenye staha sambamba na kuboresha afya ya mwili na akili.
Miongoni mwa mahitaji hayo ni pamoja na makazi bora ambayo kwa hali ya kawaida yanamwezesha binadamu kufurahia maisha na kujitofautisha na viumbe wengine wakiwemo wanyama.
Kwa mujibu wa Utafiti wa Mapato na Matumizi wa kaya Binafsi wa Mwaka 2017/2018 asilimia 15.9 ya kaya zote nchini bado zinaishi katika makazi duni yaliyojengwa kwa tembe na kuezekwa kwa nyasi (nyumba za nyasi na udongo).
Makazi haya yanatambulika kuwa ni makazi duni ambayo yamekuwa yakijengwa kwa matakwa ya kaya husika na nyumba hizi zimekuwa zikichukuliwa kuwa nyumba za asili.
Utafiti huo umebainisha moja ya sababu za kuwa na makazi ya aina hii kuwa ni uelewa mdogo ama kutokuwa na uelewa na umuhimu ama faida za makazi bora.
Sababu nyingine inayotajwa katika kusababisha uwepo wa nyumba duni ni kipato kidogo miongoni mwa wananchi wa maeneo ambayo yamebaki na makazi duni.
Elimu kuhusu umuhimu wa makazi bora pamoja na hamasa kwa wanajamii ni njia ambayo inahitajika ili kubadilisha mtazamo wa jamii kuhusu makazi sambamba na kujengeana uwezo kama wanajamii kuhusu umuhimu wa makazi bora sambamba na faida zake kwa jamii.
Hivi karibuni Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii ) imezindua Kampeni ya Kuboresha Makazi ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa majukumu yake ya msingi kwa kuiwezesha jamii kutatua mojawapo ya mahitaji ya msingi kwa binadamu kuwa na makazi bora kwa afya ya mwili na akili.
Kampeni hiyo inayobeba kauli mbiu ya ‘‘Piga Kazi: Boresha Makazi’’ ina umuhimu wa kipekee katika kuwezesha wananchi hususan wale wanaoishi katika makazi duni kujikomboa kimazingira, akili na fikra na kujenga nyumba bora ambazo mbali na kuwa na muonekano mzuri makazi hayo yanawaepusha wakazi hao dhidi ya magonjwa yanayoweza kuepukika.
Serikali ya Awamu ya Tano chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.John Pombe Magufuli iliweka bayana kwamba pamoja na mambo mengine, itawawezesha wananchi kuishi katika makazi bora ikiwa ni sehemu ya kuwaletea maendeleo na kampeni ya uboreshaji wa makazi ni sehemu ya utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya mwaka 2015-2020 Ibara ya 4 (c) iliyoahidi kuboresha makazi ya wananchi.
Aidha, uanzishaji wa kampeni hii unalenga kutekelewza Sera ya Maendeleo ya Jamii (1996) inayotaka mwananchi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na ubunifu ili kujiletea maendeleo kupitia utaratibu uliokuwa ukitumika miaka ya nyuma kama vile kusaidiana kufanya kazi za maendeleo miongoni mwa wanajamii wakilenga kutatua kero zao na kufikia malengo yao.
Utaratibu wa aina hii ulipewa majina mbalimbali katika jamii husika na kutafsiriwa kwa vitendo kulingana na mapokeo ya jamii hizo mfano; ‘Mgohe’ kwa Wahehe, ‘Msaragambo’ kwa Wapare, ‘Ireka’ kwa Wanyaturu, ‘Embesi’ kwa Wameru, ‘Saaragata’ kwa Wagogo na majina mengine mengi kulingana na tafsiri ya makabila hayo ambayo kwa umoja wake yalikusudia katika kujiletea maendeleo kupitia umoja wa kusaidiana.
Kaulimbiu ya Kampeni“Piga kazi, Boresha Makazi” inaendana na azma ya Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli chini ya Kaulimbiu ya Hapa Kazi Tu! inayosisitiza jamii kufanya kazi kwa bidii ili kusaidiana na Serikali katika kujiletea maendeleo.
Tafiti za maendeleo ya mipango miji katika nchi zilizoendelea duniani zikiwemo za China na Japan zinaonesha kuwa, mji hiyo iliendelea kutokana na juhudi za wananchi wenyewe kujitolea kwenye shughuli za ujenzi wa Taifa lao kwa kuchapa kazi kwa bidii.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Kampeni “Piga Kazi Boresha Makazi” iliofanyika wilayani Misungwi mkoani Mwanza Katibu Mkuu Wizara ya Afya- Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii, Dkt.John Jingu amesema, Serikali kwa kushirikiana na wananchi na wadau wa maendeleo itahakikisha utekelezaji wa kampeni hiyo unakuwa na manufaa makubwa kwa jamii kwa kuwahamasisha na kuijengea uwezo kisaiklojia ili wananchi katika makazi hayo waweze kujijengea nyumba kwa kutumia teknolojia rahisi na sahihi katika eneo husika.
Dkt.Jingu ameongeza kuwa, pamoja na mafanikio ya ukuaji wa uchumi, jamii bado inakabiliwa na changamoto ikiwemo makazi duni.
Aidha,takwimu za idadi ya kaya, zinaonesha kuwa Tanzania Bara ina jumla ya 9,276,997 ambapo asilimia 15.9 ya kaya hizo zinaishi katika nyumba duni zilizoezekwa kwa nyasi na udongo (Tembe). Idadi hii inamaanisha kuwa takribani kaya 56,772,232 zinaishi kwenye makazi duni.
Ameongeza kuwa, kampeni hii itakuwa chachu kwa jamii kujenga nyumba bora hasa kwa kutambua kuwa Tanzania imepiga hatua na kufikia kiwengo cha uchumi wa kati ikiwa ni miaka mitano iliyokuwa ikikusudiwa hivyo wananchi wanatakiwa kuishi maisha yanayoakisi uchumi wa kati.
“Kampeni ya Piga Kazi Boresha Makazi inalenga kufanya mageuzi ya kifikra na mtizamo wa jamii kuwa na moyo wa kujitegemea, uzalendo na kushika hatamu katika kujiletea maendeleo,”amesema.
“Katika kufikia azma hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano ya Mheshimiwa Rais Dkt.John Pombe Joseph Magufuli, Tanzania imedhamiria kuamsha ari ya jamii kusaidiana na kushirikiana katika shughuli za maendeleo ya jamii na ya mtu mmoja mmoja kwa kutumia mifumo ya asili iliyopo katika jamii,”amesema.
Dkt.Jingu amesisitiza kuwa, kampeni hii itachochea jamii kutumia mifumo, fursa na nguvu kazi iliyopo kama vile vikundi vya kijamii vya kusaidiana VICOBA, SACCOS, Benki za Kijamii, Vyama vya Ushirika wa Nyumba na Asasi za Kiraia katika kuboresha makazi yao.
Aidha, Dkt.Jingu amewataka Maafisa Maendeleo ya Jamii nchini kuzidi kuhamasisha jamii kujiunga katika vikundi vya kusaidiana ili kuwezesha kuondokana na makazi duni katika maeneo ambayo bado wananchi hawajapata mwamko wa kuboresha makazi.
Ameongeza kuwa, wataalamu wa Maendeleo ya Jamii ni kiungo muhimu katika kuhakikisha kampeni inatekelezeka ngazi ya jamii kuanzia ya ngazi ya kata mpaka Taifa na wana jukumu la kuelimisha na kuhamasisha jamii kuchukua hatua za kujiletea maendeleo.
“Hapa napenda kuvipongeza vikundi vyote nchini vilivyohamasika kwa kutambua umuhimu wa mifumo ya asili ya kusaidiana na kutumia fursa hii kuboresha makazi yao, endeleeni kuhamasisha na wengine wajiunge au kuanzisha vikundi vingine tuboreshe makazi yetu,”amesema.
Akizungumzia gharama nafuu zinazozungumziwa katika ujenzi wa nyumba bora, Dkt.Jingu amesema, kwa mujibu wa makadirio ya wasanifu majengo, nyumba bora ya gharama nafuu na teknolojia rahisi inagharimu kati ya shillingi 9,500,000 na 12,579,300 kwa nyumba ya vyumba vitatu, sebule, jiko na choo kutegemeana na upatikanaji wa vifaa vya ujenbzi katika eneo husika.
Katibu Mkuu, Dkt.Jingu ameongeza kuwa, Serikali inatambua kuwa zipo faida za kuishi katika makazi bora kama kuleta furaha, amani, uhakika wa maisha, heshima katika jamii na kujengeka kwa maadili mema kwa watoto kwani inakuwa na vyumba vinavyotosheleza familia yenye baba na mama, watoto wa kike na wa kiume.
“Kampeni itasaidia kuamsha ari ya jamii kuboresha makazi na kutatua changamoto ya mmomonyoko wa maadili katika jamii unaochangiwa kwa kiwango kikubwa na uduni wa makazi ya familia,”amesema.
“Niseme jitihada za Serikali katika kuhamsishaji jamii uboreshaji makazi inalenga kuondokana na athari zitokanazo na uduni wa makazi ikiwemo magonjwa ya mfumo wa hewa kama vile pumu, kifua kikuu, mafua, kikohozi na mengineyo,”amesema.
Dkt.Jingu amesema kuwa, Serikali inatambua kuwa utekelezaji wa kampeni unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali.
Aidha, ajenda ya makazi bora ni mtambuka na inahitaji ushirikiano wa dhati kutoka sekta mbalimbali, mashirika yasiyo ya kiserikali, wadau wa maendeleo, makampuni binafsi na wafanyabiashara wa vifaa vya ujenzi ili kufanikisha kampeni.
“Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wote katika kutekeleza kampeni. Hapa napenda kutoa wito kwa wadau kuendelea kushirikiana na Serikali katika kuwezesha wananchi kuboresha makazi yao kwa kuwapatia utaalamu, teknolojia rahisi na vifaa vya ujenzi kwa gharama nafuu,”amesisitiza.
Wananchi wa kata za Mondo na Koromije ni moja kati ya wananchi walioitikia wito wa kuboresha makazi yao kutoka katika nyumba za nyasi mpaka kuwa na nyumba za bati.
Joyce Lupemba mkazi wa Kata ya Koromoje ambaye anatoa ushuhuda wa maisha bora anayoishi baada kujenga nyumba ya kisasa, bora kwa gharama nafuu.
Amesema, kipindi wakati akiishi katika nyumba ya ya tembe iliyoezekwa kwa nyasi, pamoja na familia yake alikuwa akiishi maisha ya tabu wakikabiliwa na changamoto kadhaa ikiwa ni pamoja magonjwa ya mara kwa mara ambayo wakati mwingine yalitokana na kung’atwa na wadudu wanaoshambulia mifugo.
Joyce anasema nyumba hizo wakati wa mvua zilikuwa zikivuja na kusababisha adha kubwa na hivyo familia kukosa sehemu salama za kuishi.
“Niseme nyumba za nyasi zilikuwa sio salama kwa kuishi kwani vumbi na uchafu ulisababisha sana watoto wetu wapate magonjwa mara kwa mara na wakati mvua ilikuwa nishida sana kwetu ila kwa sasa tunaishi kwa raha sana,” amesema.
Naye Mzee Tano Kakunga mkazi wa Kata ya Mondo amesema kuwa, wananchi wamepata mwamko wa kujiunga katika vikundi na kusaidiana katika ujenzi wa nyumba bora kwani wameiona faida za kukaa katika nyumba za bati na matofali tofauti na mwanzo walipokuwa wakiishi katika nyumba za udongo na nyasi.
“Niombe tu Serikali ituunge mkono kwa kutuwezesha kupata mikopo yenye unafuu ili wananchi wengi waweze kuondokana na nyumba za udongo na nyasi na kuboresha nyumba zao,”amesema.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Shirika la Kivulini, Yassin Ally amesema,shirika lake linashirikiana na Serikali kuhakikisha linaacha alama jangwani kwa kuhamasisha wananchi kujiletea maendeleo na mabadiliko katika maisha.
“Sisi tuna msemo wa kuacha alama Jangwani, tunawawezesha wananchi wa maeneo haya kujenga moyo wa kusaidiana na kuwezeshana kuondokana na makazi duni na kujenga nyumba bora kwa kutumia gharama kidogo. Nishukuru tu, kwamba wananchi wametuelewa na mabadiliko ni kama invyoonekana,”amesema.
Ameongeza kuwa, katika kuhakikisha kwamba wananchi wanabadili fikra kuhusu makazi, walihamasisha utunzi wa nyimbo zinazohamasisha wakazi kuishi katika makazi bora huku nyimbo hizo zikiwakatisha tamaa ya kuishi katika nyumba za nyasi na kusema kuwa nyasi ni kwa ajili ya mifugo na siyo kwa ajili ya makazi.
Akizungumzia kazi za Kivulini kama Shirika Lisilo la Kiserikali, Yasin anasema mashirika hayo yanawajibika kufanya kazi kwa uwazi na kuwawezesha wananchi kujiletea maendeleo na kufanya na hivyo kuendana na kasi ya serikali ambayo kwa ujumla wake imeweza kuingia katika uchumi wa kati.
“Sisi kama mashirika na asasi za kiraia tunashukuru Serikali kutujengea mazingira bora ya kazi ya kuwawezesha wananchi kufanya kazi za maendeleo, kazi yetu ni kusaidia majukumu ambayo tumekabidhiwa na Serikali na tunashukuru pale tunapokuwa tumefanikiwa kufanya jambo linalothibitika kwa macho,”anafafanua.
“Mpaka sasa Kampeni ya ”Piga Kazi Boresha Makazi” kwa Wilaya ya Misungwi imefikia tarafa nne, kata 27, vijiji 144 na vitongoji 724 kwa kutumia njia mbalimbali za kuhamasisha jamii kuondokana na makazi duni na kuboresha makazi yao.
“Niseme tu hatutoishi katika Wilaya ya Misungwi Mkoa wa Mwanza, bali tunaenda katika mikoa mingine na tumeshaanza kutoa elimu ya kuborehsa makazi katika mikoa ya Shinyanga, Geita, Mara na Kigoma ili kuwahamasisha wananchi wa maeneo hayo kuboresha makazi,”anasema.
Serikali kwa kushirikiana na mashirka yasiyo ya kiserikali inaendelea kutoa elimu kwa wananchi kupitia mwongozo wa uhamasishaji ujenzi wa nyumba bora ngazi ya jamii ili kuhakikisha wananchi wanahamsika kuboresha makazi yao na kuishi katika nyumba bora.
Mwandishi wa makala haya,Raymond Mushumbusi ni Afisa Habari Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii).
More Stories
Ushiriki wa watoto, vijana katika vita ya mabadiliko ya tabianchi
Ubunifu wa Rais Samia kupitia Royal Tour unavyozindi kunufaisha Tanzania
Rais Samia anavyojenga taasisi imara za haki jinai kukabilina na rushwa nchini