Na Hadija Bagasha,TimesMajira Online, Tabora
MGOMBEA urais kwa tiketi ya Chama cha Wananchi (CUF) Profesa Ibrahim Lipumba, amesema iwapo atapata ridhaa ya kuongoza nchi atahakikisha anasimamia soko la tumbaku nje ya nchi, kwani raia wa chini zaidi ya milioni 400 wanavuta tumbaku.
Akihutubia wananchi wa Kijiji cha Igalula Station Kata ya Igalula, wilayani Uyui mkoani Tabora, Prof. Lupumba, alisema mkoa huo wa Tabora unasifika kwa kulima zao la tumbaku lakini Serikali imewasahau wakulima wake.
Profesa Lipumba alisema wanahitaji wapate Serikali itakayosimamia maendeleo ya uchumi na itakayowekeza kwenye sekta ya kilimo kwa kujenga mazingira mazuri ya biashara ili viwanda vya tumbaku viendelee kuwepo pamoja na kukuza soko lake.
“Ndugu zangu tumbaku ina madhara yake, lakini wavutaji bado wapo wengi zaidi ya Wachina milioni 400 wanavuta sigara, Tanzania watu wote tupo kama milioni 58, wavuta sigara Uchina ni Mara saba ya wananchi wote waliopo Tanzania pana soko la tumbaku, lazima tuwe na Serikali itakayochangamkia soko hilo la wakulima wapate bei inayopatikana kwenye soko la tumbaku,” alisisitiza Profesa Lipumba.
“Wakulima wa tumbaku wameharibiwa soko lao la tumbaku, tumbaku haina soko mwaka jana kuna watu wameshinda na tumbaku zao kwenye mabanda, bei mbovu kwa sababu soko la tumbaku limeharibiwa na Serikali ya CCM,”alisema
Aliongeza kuwa kampuni iliyokuwa na tumbaku imetozwa kodi na ushuru mpaka ikashindwa kujiendesha wakafunga viwanda, nimefika Morogoro juzi watu wanalalamika hawana ajira viwanda vilivyokuwa vikichambua na kusindika tumbaku vimefungwa.
Alisema makampuni yaliyokuwa yakinunua tumbaku hivi sasa hayana soko kwa kuwa walikuwa wakipeleka kwenye makampuni yaliyokuwa na viwanda vya tumbaku ambavyo hivi sasa vimefungwa na hatimaye wanashindwa kununua tumbaku.
“Wakulima wapo hoi pamoja na suruba ya kilimo, lakini tumbaku haina soko biashara yake haitoki unaweza kuona Igalula hapa, lakini njaa tupu mzunguko wa pesa hakuna vijana hawana hela wanaweza kuona vitumbua vinauzwa mate yakawatoka wanaishia tu kuangalia pesa hawana,” alisema Profesa Lipumba.
Alisema Serikali isijikite kuendeleza tu zao la tumbaku, lakini pia wapate mazao mbadala kama korosho ambazo zinakubali kwenye ardhi ya Tabora hivyo kuwe na utaratibu wa kuwa na kilimo cha korosho kwa kuwa na soko la uhakika lipo.
“Korosho ni zao ambalo wenzetu wa Ulaya na Marekani wanatumia sana kwenye shughuli za sherehe kipindi cha pasaka, Krismasi, mwaka mpya na nyingine anapokunywa vinywaji vyao wanapenda pia wawe na vitafunio ambavyo ni korosho nchi za Africa Mashariki korosho wanaitumia katika mapishi yao na hata Wachina pia,” alisema.
Kwa upande wake mgombea ubunge Jimbo la Kaliua na Naibu Katibu Mkuu wa wa CUF, Magdalena Sakaya alisema anaishangaa nchi ya Tanzania kwa kuwa ina maprofesa wa fani mbalimbali, ikiwemo wa uchumi lakini inashindwa kuwatumia kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania.
Sakaya alisema vijana wanahangaika mitaani wanasoma na kumaliza digrii zao, lakini ajira hakuna hivyo wanahitaji kutumia hekima na busara kufanya mabadiliko na kuacha kuishi kwa mazoea.
”CCM wamezoea viongozi wote wanajua kabisa ukishamchagua mbunge, au diwani shida yenu nyie ni ubwabwa na vipande vya nyama, hamtoi nafasi kwa malengo, hamtoi ubunge kwa malengo, wala hamtoi urais kwa malengo, mnatoa nafasi kwa kutegemea mtapewa vyakula,”alisema.
More Stories
Watakaokwamisha mapato Kaliua kukiona cha moto
Dkt.Gwajima aagiza kuundwa kamati za ulinzi wa watoto
Kilo 673.2,dawa za kulevya zakamatwa Bahari ya Hindi