March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Wadau watakiwa kuchangamkia fursa za mkonge

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma

MKUU  wa Sehemu ya Maendeleo ya Mkonge kutoka Bodi ya Mkonge Tanzania  Simon Kibasa amewataka wananchi na wadau mbalimbali kuchangamkia fursa lukuki zinazopatikana katika sekta ya mkonge nchini, hasa katika hatua ya uchakataji na masoko ya bidhaa zinazotokana na zao hilo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma katika maonyesho ya Kimataifa ya Wakulima kwenye banda la Bodi ya Mkonge, Kibasa o amesema kuwa sekta ya mkonge imeendelea kukua kwa kasi kufuatia kampeni ya serikali ya kuhamasisha kilimo cha mkonge iliyoanza rasmi mwaka 2020, ambapo wakulima wengi wameitikia wito huo.

 “Kwa sasa mkonge upo kwenye hatua za mwisho za uzalishaji, na hivyo tunawakaribisha wadau kushiriki katika hatua ya uchakataji wa mkonge kwa kuwekeza kwenye mashine za kuchakata na kuchaji huduma hiyo,” amesema.

Amebainisha kuwa Bodi ya Mkonge Tanzania imekuwa ikitoa mbegu bora kwa wakulima wapya pamoja na kutoa mafunzo, jambo linalowezesha kila Mtanzania anayetaka kuingia katika tasnia hiyo kufanya hivyo kwa urahisi.

Mbali na uchakataji, alieleza kuwa fursa nyingine zinazopatikana ni pamoja na kuuza singa zitakazozalishwa baada ya uchakataji wa mkonge. Aidha, alisisitiza kuwa bidhaa za mkonge zina soko kubwa ndani na nje ya nchi, hasa kwenye masoko ya kimataifa ambako mahitaji ya bidhaa asilia yanaendelea kuongezeka.

 “Hii ni nafasi adhimu kwa sekta binafsi, vijana na wanawake kuwekeza kwenye mnyororo wa thamani wa mkonge  kuanzia uzalishaji, uchakataji hadi usambazaji wa bidhaa,” ameongeza.

Amesema, lengo ni kuhakikisha Tanzania inarejea katika nafasi yake kama mmoja wa wazalishaji wakubwa wa mkonge duniani, huku ikiwa imejipanga kuhakikisha mazingira bora ya uwekezaji, elimu kwa wakulima na upatikanaji wa pembejeo bora.