
Na Joyce Kasiki,Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kutoa elimu kwa wananchi katika Maonesho ya Nanenane yanayoendelea Jijini Dodoma ikiwemo madhara ya utumikishwaji wa watoto nchini.
Aidha, wananchi wamepata fursa ya kuelezwa kuhusu kazi hatarishi wanazofanya watoto ambazo husababisha ukosefu wa haki zao za msingi kama vile kupata elimu, afya, kulindwa dhidi ya unyanyasaji, kushiriki michezo na haki ya malezi bora.
Akizungumza, Afisa Kazi Mwandamizi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu, Bw. Oddo Hekela amesema “Tumeendelea kuelimisha umma kupitia maonesho haya kwa kukumbusha jamii kuwa ajira ya mtoto chini ya miaka 14 ni kosa kisheria, hivyo ni wajibu wa kila mmoja katika jamii kuhakikisha watoto wanalelewa katika mazingira salama na yanayowapa fursa ya kukua vizuri kiafya, kielimu na kimaadili.”
Amesema, Kifungu cha 5 cha Sheria ya Ajira na Mahusiano Kazini Sura 366 kinakataza Mtoto chini ya Miaka Kumi na Nne kufanya kazi zisizo rasmi ikiwemo upakuaji mizigo, usafirishaji wa magari pamoja kazi za viwandani.
Vile vile, amesema kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu imeendelea kuwahimiza wananchi wote kutoruhusu wala kushiriki katika vitendo vya kuajiri watoto, huku ikiendelea kusisitiza wajibu wa ulinzi wa mtoto ni jukumu la kila mwananchi.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi