TCCA yatoa elimu kuhusu matumizi salama ya Drones katika kilimo maonyesho NaneNane
Na Joyce Kasiki,Timesmajira online, Dodoma
MAMLAKA ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) inaendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu matumizi salama na sahihi ya ndege nyuki (drones) katika shughuli za kilimo, ikiwa ni sehemu ya ushiriki wake katika Maonesho ya Wakulima Nanenane yanayoendelea kufanyika katika viwanja vya Nzuguni, jijini Dodoma.
Kwa mujibu wa wataalam kutoka TCAA, teknolojia ya ndege nyuki imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha kilimo cha kisasa, ambapo hutumika katika shughuli mbalimbali ikiwemo upuliziaji wa viuatilifu, ufuatiliaji wa afya ya mazao, uchambuzi wa udongo, na utunzaji wa kumbukumbu za mavuno kwa usahihi wa hali ya juu.
Akizungumza katika banda la TCAA lililopo kwenye maonesho hayo, Mkaguzi wa Ndege Nyuki kutoka TCAA, Bw. Ibrahim Abdalah, alisema kuwa pamoja na faida kubwa zinazotokana na matumizi ya teknolojia hiyo, ni muhimu kwa watumiaji kufuata sheria na kanuni zilizowekwa ili kulinda usalama wa anga.
“Matumizi ya ndege nyuki katika kilimo yameleta mapinduzi makubwa katika sekta ya kilimo, lakini ni muhimu yakazingatia usajili rasmi na kufuata kanuni za kiusalama. TCAA tunahakikisha matumizi haya yanafanyika kwa ufanisi bila kuhatarisha usalama wa anga na watumiaji wake,” amesema Bw. Abdalah.
Amesisitiza kuwa, kwa mujibu wa Sheria ya Usafiri wa Anga na miongozo ya matumizi ya ndege nyuki, kila drone inapaswa kusajiliwa rasmi kabla ya kutumika, na operesheni zake lazima zifanyike kwa kuzingatia masharti ya usalama na matumizi halali.
“Kwa kutambua mchango mkubwa wa teknolojia hii katika maendeleo ya kilimo na uchumi kwa ujumla, Mamlaka hiyo imeendelea kutoa wito kwa wakulima, watafiti, na watoa huduma za kilimo kuhakikisha wanatumia ndege nyuki kwa kufuata taratibu stahiki.”
Aidha,amewahimiza wadau hao kuwasiliana na ofisi zao kwa ajili ya kupata ushauri wa kitaalamu, msaada wa kiufundi, na maelekezo kuhusu upatikanaji wa vibali halali vya uendeshaji wa ndege nyuki nchini.

More Stories
Wanawake jumuia ya kikristo Tanzania CCT wafundana kuelekea siku ya Wanawake Duniani
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi