March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Watatu wapoteza maisha Sengerema matukio mawili tofauti

Na Daud Magesa, Timesmajira Online-Mwanza

Watu watatu wamefariki katika matukio mawili tofauti mkoani Mwanza likiwemo la kijana mmoja kuuwawa kwa tuhuma za kufumaniwa akiwa na mke wa mtu pamoja na watoto wawili kufungua na moto.

Akizungumza matukioa hayo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Wilbrod Mutafungwa,amesema katika tukio la kwanza lililotokea Julai 29,2025, majira ya saa 7 usiku kijiji cha Lumeya, Kata ya Nyakaliro, Wilaya ya Sengerema mkoani hapa,amesema,mtuhumiwa anayefahamika kwa jina la Bagandosa Silas Menelo anadaiwa kumuua Elias Martine Mshaki (23) kwa kumpiga tumboni na kitu butu baada ya kumfumania akiwa na mke wake, Neema Sylvester Thobias (20), mkazi wa kijiji hicho.

Kwa mujibu wa taarifa ya Jeshi la Polisi, siku ya tukio mtuhumiwa na marehemu walikuwa wakinywa pombe pamoja, kabla ya Elias kuondoka na kwenda nyumbani kwa Bagandosa ambako alikutwa na mke wa mtuhumiwa.

Ghasia zilipozuka, mtuhumiwa alimpiga Elias kwa kutumia kitu butu hadi kufariki dunia, kisha kumgeukia mke wake na kumshambulia, akimsababishia majeraha kichwani.

Mutafungwa, amesema,chanzo cha tukio hilo ni wivu wa mapenzi, mwili wa marehemu umefanyiwa uchunguzi na kukabidhiwa kwa familia kwa maziko, huku majeruhi akiendelea kupokea matibabu katika Hospitali ya Halmashauri ya Buchosa.


“Tunamsaka mtuhumiwa na tunatoa wito kwa wanandoa na wapenzi kuwa wavumilivu wanapokumbwa na migogoro ya uhusiano, badala ya kujichukulia sheria mkononi,”Mutafungwa.

Katika tukio jinginge Mutafungwa,amesema
limetokea siku hiyo hiyo saa 11 alfajiri, eneo la Kijiweni, Kata ya Chifunfu wilayani Sengerema,ambapo watoto wawili wamefariki dunia baada ya kuungua kwa moto uliotokana na mlipuko wa mtungi wa gesi.

Watoto hao ni Efraim William (3) na Justa Msomi (3), wote wakazi wa Kijiweni ambapo inadaiwa kuwa William Simeo (23), mkulima na mkazi wa eneo hilo, aliwasha jiko la gesi kwa ajili ya kuwaandalia mayai watoto hao ndani ya chumba kilichokuwa na mitungi ya gesi, bila kuchukua tahadhari, na kusababisha uvujaji wa gesi uliopelekea mlipuko wa moto.

Mutafungwa amesema,wanendelea na uchunguzi wa tukio hilo, huku mtuhumiwa akishikiliwa kwa mahojiano.

“Tunatoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha usalama wa watoto wao kwa kuchukua tahadhari wakati wa matumizi ya gesi na vifaa vya moto,”amesema Mutafungwa.