Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Imeelezwa kuwa umbali,ukosefu wa miundombinu rafiki katika shule za umma pamoja na walimu wenye uelewa juu ya watoto wenye changamoto ya kichwa kujaa maji kuliko kawaida(kichwa kikubwa) na mgongo wazi,kunachangia watoto hao kukosa hakinya msingi ikiwemo elimu.
Hivyo wito umetolewa kwa Serikali na wadau,kuwekeza nguvu zaidi kwa kuhakikisha miundombinu inaboreshwa pamoja na kuzalisha walimu wa mahitaji maalumu ambao watakuwa na uelewa wa kuwafundishia na kuwahudumia watoto hao.
Hayo yameelezwa na wadau mbalimbali wakati wa mafunzo ya kuwajengea uelewa wa pamoja waalimu wa watoto wenye mahitaji maalumu kutoka Wilaya mbili za Ilemela na Nyamagana mkoani Mwanza,yalioandaliwa na Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania(MWADETA).

Akizungumza na Timesmajira Majira Online mara baada ya mafunzo hayo,mmoja wa wazazi wenye watoto wenye changamoto hizo,Verediana Lugendo,amesema,watoto wenye ulemavu ikiwemo wenye mgongo wazi na kichwa kikubwa wana umuhimu na haki ya kupata elimu kama ilivyo watoto wengine huku umbali wa shule ni moja ya changamoto inayokwamisha watoto hao kupata elimu.
“Kwani watoto hawa miguu yao hawawezi kutembea umbali mrefu hivyo wanatakiwa kuwa na usafiri au visaidizi vya kuwasaidia kutembea kwa umbali huo au wawe na watu watakao wapeleka shuleni na kuwarudisha nyumbani,”.
Hivyo ameiomba Serikali kuwasaidia wazazi wenye watoto hao kwa kuwapatia bima na vifaa saidizi ikiwemo miguu bandia,shule za umma ziwe karibu pamoja na miundombinu yake kuboreshwa ili iwe rafiki kwa kundi hilo.
Salma Yusuph(mzazi),amesema suala la elimu kwa watoto wenye kichwa kikubwa na mgongo wazi,imekuwa changamoto hususani katika shule za Serikali,ambapo amedai kuwa wakiwapeleka walimu wamekuwa wakiwakataa,hivyo Serikali iwasaidie kuhusu jambo hilo hili watoto hao waweze kupata elimu kama wengine na haki nyingine za msingi.
Pia ameiomba Serikali kuwasaidia suala la bima kwa watoto hao ambayo ni changamoto kwani wanapowapeleka kwenye matibabu gharama zimekuwa kubwa huku wazazi wengi wao maisha yao ni duni,hivyo wanashindwa kumudu gharama.
Kwa upande wake Getruda Laizer(mwenye changamoto ya mgongo wazi),ameiomba Serikali erikali naomba iwekeze nguvu kwa watoto wenye changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa kwa sababu wengi wanakua lakini hawapati elimu hivyo kuwanyima fursa mbalimbali ikiwemo ajira na kubaki kuwa tegemezi wakati wote.
“Mfano mimi nilizaliwa na changamoto ya mgongo wazi kwa sasa ni mama wa watoto watatu nina miaka 37,nilipata fursa ya kusoma nina Diploma ya Maendeleo ya Jamii,ninafanya kazi ya kuhudumia watoto wanaozaliwa na changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa,je nisingepata elimu hii taifa lengepoteza nguvu kazi na kuongeza mzigo wa utegemezi,”.
Pia ameiomba Serikali iboreshe miundombinu upande wa shuleni na hospitalini, kwani shule nyingi zinakuwa na ngazi na watoto hao hawawezi kuzitumia kwa sababu wanatumia viti mwendo.
Sanjari na hayo amesema unyanyapaa katika Jami pia ni kikwazo huku akitolea mfano maisha yake ya utotoni kuwa aliishi kwa kunyanyapaliwa na jamii na ndugu na alikuwa mtoto asiye na rafiki wala kupata fursa ya kuchangamana na wenzie, lakini kilichompa nguvu mpaka ameweza kusoma na kufika hapo ni upendo wa wazazi wake ambao hawakumkatia tamaa wala kutelekeza.
Hivyo amewataka wazazi wenye watoto wa namna hiyo kuwapenda watoto wao na kuwapatia fursa za kielimu na nyingine kama walivyo wengine.
“Serikali ikilivalia njuga suala hili na kuonesha kuwa wanawaunga mkono watoto hawa kwa namna moja ama nyingine waweze kupata elimu naamini hata wazazi wao watapata moyo wa kuwasomesha watoto hao kwani watakuwa msaada baadae walipata elimu,”.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwanangu Development Tanzania(MWADETA),Walter Miya,amesema ukosefu wa miundombinu ya kuwasaidia watoto hao kupata huduma ikiwemo chumba maalumu cha kuwaondolea haja ndogo na kubwa wa wapi shuleni pamoja na walimu wenye utaalmu wa kujua muda gani mtoto huyo anahitaji huduma fulani ndio sababu ya wazazi hao kushindwa kuwapeleka watoto hao kwenye shule za umma.
Hivyo ndio sababu ya taasisi hiyo kutoa elimu hiyo kwa walimu wa mahitaji maalumu ambao kimsingi wamefundishwa kuhusu mahitaji maalumu lakini hawajafundishwa kuhusu namna ya kuwahudumia watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi.
“Sisi kama taasisi mwaka 2018 eneo la Vikindu Mkuranga mkoani Pwani, tukifanikiwa kuanzisha shule ya watoto wenye ulemavu mbalimbali lakini lengo kubwa ilikuwa ni watoto wenye vichwa vikubwa na mgongo wazi,hiyo ni baada ya kuona kuwa tunaokutana na watoto wengi hospitalini kwenye matibabu lakini hawawezi kuhudhuria shule,” amesema Miya na kuongeza:
“Kwa sasa ipo darasa la tano na ni shule shinikizi na jumuishi kati ya Serikali na binafsi ya bweni na kutwa ambayo inapokea watoto kutoka mikoa tofauti,ina jumla ya wanafunzi 106,na nusu kati yao ni wenye ulemavu na tunawachanganya wote wenye mahitaji maalumu na wa kawaida lengo ni kuleta usawa,”.

Naye Mwakilishi wa Ofisa Elimu Mkoa wa Mwanza,Mwalimu Jovither Mwombeki,amesema,mkakati wa Serikali ni kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata elimu sawa bila kujali hali zao.
“Madarasa yetu yote na shule zetu zote,zimeelekezwa kufundisha na kuwa na hali ya kuwa na madarasa jumuishi kwa maana ya kwamba watawekwa watoto wote wenye mahitaji maalumu na wasio na mahitaji maalumu,hasa wale ambao hawahitaji walimu,”amesema Mwalimu Jovither na kuongeza:
“Tunawatumia Maofisa Elimu Maalumu kutoka Halmashauri, kuhakikisha wanawabaini watoto wenye changamoto na ikifika kipindi cha kuwasajili wanafunzi wa darasa la awali na la kwanza, kuhakikisha watoto waliofikisha umri wa kwenda shule wanaandikishwa bila kujali tofauti zao,”.
Pia amesema,kwa sasa miundombinu shuleni inawaruhusu wanafunzi wote ikiwemo wenye hali ambazo siyo za kawaida waweze kufurahia kukaa katika madarasa na kupata fursa ya elimu huku walimu wakipatiwa semina za mara kwa mara za kuwahudumia wanafunzi wenye mahitaji maalumu.
Hata hivyo Daktari bingwa wa upasuaji wa ubongo na mgongo,kutoka Hospitali ya Rufaa ya Kanda Bugando,Dkt.Gerald Mayaya,amesema hospitali hiyo kwa mwaka wanapokea watoto wapya wenye changamoto ya mgongo wazi na kichwa kikubwa wastani wa 300-400.
Kwa miaka miwili iliopita walikuwa wanapokea watoto waliochelewa kuanza matibabu kwa asilimia 75, baada ya kufanya OUTETA kwa sasa wanapokea watoto waliochelewa kwa asilimia 50.
Pia amesema,umbali na hali ya kiuchumi ndio sababu ya watoto hao kukosa matibabu huku akidai kuwa wakipatiwa matibabu mapema wanaweza kufanya vitu kama watu wengine ikiwemo elimu.

“Mtoto wa kichwa kikubwa na mgongo wazi,akiibiwa vizuri,ataweza kusoma na kufanya shughuli za kijamii na kiuchumi hivyo kuwa na mchango katika taifa na kuanzisha familia na kuzaa watoto ambao hawana changamoto,mfano mama mmoja ambaye alipata matibabu akiwa na miezi mitatu na sasa amefanikiwa kupata mtoto mwenye umri wa miezi sita ambaye ni nzima,”amesema Dkt.Mayaya na kuongeza:
“Lakini wasipopata matibabu taifa linapoteza nguvu kazi ikiwemo ulemavu wa kudumu ambao hatashindwa kufanya jambo lolote na kuwa mzigo kwa familia na taifa pamoja na vifo,”.


More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina