Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora
MKUU wa Mkoa wa Tabora, Paul Chacha ameahidi kukodi mabasi ya kutosha ili kupeleka mashabiki wa soka wa Mkoa huo jijini Dar-es-Salaam ili kushangilia timu ya taifa (Taifa Stars) kwenye ufunguzi wa michuano ya CHAN katika uwanja wa Benjamin Mkapa.
Chacha ametoa ahadi hiyo wakati akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake, ambapo ameeleza kuwa Tabora ni miongoni mwa Mikoa yenye hamasa na mashabiki wengi wa soka nchini hapa.
“Ni lazima tupeleke mashabiki wengi zaidi kuliko Mikoa mingine ili kuiongezea hamasa timu yetu ya taifa, nitakodi mabasi ya kutosh:a ya kupeleka mashabiki bure uwanjani jijini Dar na kuwarudisha,”amesema Chacha na kuongeza:
“Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan ameahidi kutoa zawadi nono kwa vijana wetu wakitwaa ubingwa, na sisi tutamuunga mkono kwa kuipa hamasa timu yetu ya taifa ili ifanye vizuri,”.
Ametoa wito kwa mashabiki wa soka kutoka Wilaya zote 7 za Mkoa huo walio tayari kwenda kushuhudia ufunguzi wa michuano hiyo kujitokeza kwa wingi.
Akizungumza kwa niaba ya mashabiki wenzake, Nico Joseph mkazi wa Halmashauri ya Manispaa ya Tabora,amesema wapo tayari kwenda uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao kwenye mtanange wa ufunguzi wa michuano hiyo.

More Stories
Dkt.Tulia,Mwalunenge waungana kutatua changamoto ya barabara
TUCASA yaomba kuanzishwa sheria malipo sekta ya ujenzi
Kihongosi:Uhai wa chama mashina