Ashura Jumapili,TimesMajira Online-Bukoba,
Jitihada za Mbunge wa Jimbo la Bukoba Mjini Wakili Stephen Byabato,zimewezesha miradi mbalimbali ya maendeleo yenye thamani ya bilioni 40 iliokuwa imekwama kwa muda mrefu kutokana na changamoto za kisiasa kutekelezwa.
Miradi hiyo ni ya ujenzi wa soko kuu la Bukoba,stendi ya mabasi,kingo za mto Kanoni na upanuzi wa barabara,ambayo ilikuwa kilio cha muda mrefu kwa wananchi wa Bukoba.

Wakili Byabato,amesema katika ahadi za Chama Cha Mapinduzi(CCM) mwaka 2020 walihaidi kujenga soko la kisasa na stendi.
“Wakati napambania utekelezaji wa miradi hiyo baadhi ya watu walinizuia na kunieleza kuwa nikifuatilia hiyo miradi nitakosa Ubunge,nikawajibu soko litajengwa na mimi sio wa kwanza kuwa Mbunge hapa wala sitakuwa wa mwisho lazima miradi itekelezwe,”amesema Byabato.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera,Fatma Mwassa, amesema wakandarasi wamekabidhiwa maeneo ya ujenzi wa soko jipya,stendi ya mabasi Kyakailabwa,kingo za mto Kanoni zenye urefu wa kilometa 7.3 na barabara yenye urefu wa kilometa 10.75 ikiambatana na usimikaji wa taa za barabarani 423.
Amesema miradi hiyo imegawanywa katika makundi mawili ambapo Mkandarasi mzawa M/s Dimetoclasa Realhope Limited atajenga soko na stendi ya mabasi Kyakailabwa kwa gharama ya bilioni 18.9.
Huku Mkandarasi wa kigeni M/s Shandon Luqiao Group Company Limited atajenga barabara kilometa 10.75, kingo za Mto Kanoni kilometa 7.3 na kuweka taa za barabarani 423 kwa gharama ya bilioni 21.3.
Amesema matarajio yake ni kuona miradi hiyo inakamilishwa kwa wakati kulingana na mkataba ambapo wamepewa kipindi cha miezi 15 kuanzia Julai 15, 2025 hadi Oktoba 14, 2026.

Pia amesema miradi hiyo inatarajia kuwa kichocheo cha uchumi wa Manispaa hiyo na Mkoa wa Kagera,kwa kutengeneza ajira kwa vijana na kuwa kivutio hivyo amewataka wananchi kuhakikisha wanailinda miradi na kutoa ushirikiano kwa wakandarasi kufanya kazi yao bila vikwazo vyovyote.
Halmashauri ya Manispaa ya Bukoba ni miongoni mwa miji 15 ya awamu ya pili zinazotekeleza miradi ya TACTICS, lengo likiwa ni kupendezesha miji na kuongeza mapato ya ndani.


More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako