Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Kasulu
Wanafunzi zaidi ya 1200,wa shule ya msingi Buhoro,iliopo wilayani Kasulu mkoani Kigoma wamenufaika na kilimo cha kahawa kwa kuanza kupata huduma ya chakula shuleni kutokana na mauzo ya zao hilo.
Hayo ni matokeo ya Wilaya ya Kasulu, kuhamasisha wakazi wa wilaya hiyo, taasisi za elimu na wadau mbalimbali kuchangamkia fursa ya kilimo cha zao la kahawa ili kujikwamua kiuchumi.

Hayo yameelezwa na viongozi, watendaji na walimu wa shule ya msingi Buhoro iliyopo Kata ya Buhoro,wilayani humo wakati wakizungumza na mwandishi wa habari hii.
Akiongea kwa niaba ya Mwalimu Mkuu wa shule ya msingi Buhoro,Mwalimu wa Taaluma wa shule hiyo Stanslaus Petro,amesema walianza kulima zao hilo mwaka 2021 baada ya kuhamasishwa na Ofisa Kilimo wa halmashauri hiyo.
‘Tulipatiwa jumla ya miche 100 tukaipanda, na yote imekua vizuri na inazaa matunda mengi, huu ni mwaka wa pili sasa tunavuna mfululizo, tumeshapata zaidi ya kilo 800 na kuziuza, fedha tunayopata inatumika hapa hapa shuleni ikiwemo kutoa huduma ya chakula kwa wanafunzi wetu,”amesema.
Mwanafunzi wa darasa la pili katika shule ya msingi Buhoro,Neema Luhomwa, amekiri kuwa shamba lao la kahawa linawasaidia kupata mlo, uji asubuhi kwa kila siku, hali inayowafanya kupenda shule na kusoma kwa bidii.
Mwenyekiti wa Kijiji cha Buhoro,Fredrick Nyambo, amepongeza halmashauri ya Wilaya hiyo kwa kuhamasisha wananchi na shule zote kulima zao hilo na kugawa miche bure kwa watu wote, manufaa yake yameanza kuonekana.
‘Halmashauri imeotesha jumla ya miche 200,000 kati ya hiyo miche 6000 imegawiwa kwa wakazi wa kata hiyo na hekali 100 za zao hilo zimepandwa katika maeneo mbalimbali,”.
Katibu wa CCM wa Kata hiyo,Elias Daud, ameeleza kufurahishwa na juhudi zinazofanywa na serikali kupitia halmashauri hiyo, kwani zimesaidia kutatua kero ya utoro kwa wanafunzi wa shule hiyo, kupitia chakula kinachotolewa shuleni.

Naye Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho, Paskarin Clement, amesema kuwa kilimo cha zao hilo kimeleta neema katika shule hiyo na jamii kwa ujumla, na sasa wameanzisha Chama cha Msingi cha Ushirika (Amcos) ili kurahisisha soko la wakulima..

More Stories
TAMWA yakumbusha jamii kupinga ukatili wa kijinsia kuelekea siku ta wanawake Duniani
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro