March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Aweso aagiza mradi wa maji Kiwira ukamilike haraka

Na Esther Macha, Timesmajira Online-Mbeya

WAZIRI Maji Jumaa Aweso,amemuagiza mkandarasi anayejenga mradi wa maji kutoka chanzo cha mto Kiwira mkoani Mbeya kampuni ya China Railway Construction Engineering Group kuharakisha utekelezaji wa mradi huo.

Mradi wa Kiwira unatarajia kuzalisha lita za maji milioni 117 kwa siku,zitakazowezesha Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mbeya kuzalisha lita milioni 190 kutoka lita milioni 74.2 za sasa.

Aweso amesema hayo Julai 23,2025,wakati wa ziara ya siku moja ya kukagua utekelezaji wa mradi huo,ambapo amesema chanzo cha maji mto Kiwira kitakua matumaini kwa wananchi wa Mbeya.

Amesema anaridhishwa na kasi ya utekelezaji katika eneo la chanzo lakini bado upo umuhimu wa kuongeza kasi ili mradi huo ukamilike Desemba 2025,kama ilivyoainishwa katika mkataba.

Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Jijini Mbeya, CPA Girbert Kayange, amesema kuwa mradi huo ukikamilika utaweza kukidhi mahitaji ya wananchi wa Mbeya na Mjini wa Mbalizi na viunga vya jirani kwa asilimia 100.

Amesema kuwa maji hayo yatatoka kwenye chanzo kwenda Jiji la Mbeya kwa njia ya mseleleko kutoka kwenye banio ambalo linaendelea kujengwa na kusafiri kwa umbali wa kilometa 37, kupitia kwenye bomba kubwa la chuma lenye kipenyo cha ukubwa wa milimita 200.

Hata hivyo amesema kuwa utekelezaji wa mradi huo mpaka sasa ni asilimia 45,na katika eneo hilo la mradi banio limeshatekelezwa kwa asilimia 95, na ulazaji wa bomba kuu la kusafirisha maji .

Katibu wa Chama cha Mapinduzi (CCM) mkoani Mbeya, Langael Akyoo,amesema chama hicho kinaridhishwa na jitihada zinazofanywa na Serikali kuhakikisha huduma ya maji inawafikia wananchi.

Amesema wataendelea kushirikiana kwa karibu na Wizara ya Maji ili kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati.

Waziri Aweso pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Maji Mhandisi Mwajuma Wazjiri wako katika ziara ya kukagua miradi ya maji katika mikoa ya Nyanda za Juu Kusini.