*Ni kwa kuendeleza uchumi wa buluu
*Zaidi ya hekta 90 za mikoko zarejeshwa Tanga na Pemba
Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online-Tanga
Wadau wa mazingira nchini hapa wameonesha dhamira ya dhati katika kutekeleza Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, kwa kuhimiza ukuaji wa uchumi wa buluu kupitia miradi ya urejeshaji wa mazingira ya pwani na baharini.
Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, zaidi ya hekta 90 za mikoko zimepandwa upya katika mikoa ya Tanga na Pemba, hatua ambayo inalenga kulinda bioanuwai ya pwani, kuimarisha uthabiti wa fukwe dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, pamoja na kuinua uchumi wa jamii za maeneo hayo.

Mradi huu unaotekelezwa chini ya usimamizi wa Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kwa kushirikiana na Shirika la Kimataifa la Uhifadhi wa Mazingira na Uasili (IUCN) kupitia mradi wa Bahari Mali.
Akizungumza na katika mafunzo ya waandishi wa habari kuhusu masuala ya uchumi wa buluu, yaliyoandaliwa kwa ushirikiano wa JET na IUCN, kupitia mradi ya Bahari Mali, Meneja wa Miradi ya Uhifadhi wa Bahari , Joseph Olila,amesema urejeshwaji huo ni sehemu ya mradi ya mradi huo unaolenga kutumia fursa ya uchumi wa buluu kwa njia jumuishi na endelevu kwa lengo la kulinda bayoanuwai ya pwani na baharini.
Amesema urejeshaji wa mikoko unaongozwa moja kwa moja na jamii za maeneo husika kwani ndio wanafahamu maeneo yalio athirika zaidi,pia wanaofanya kazi kwa kushirikiana na taasisi za Serikali kama Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) na idara za misitu za halmashauri.
“Hadi sasa jumla ya hekta 90.4, zimeisharejeshewa uoto wa asili,tuna lengo la kufikia hekta 100 kufikia mwishoni mwa mwaka huu. IUCN hutoa msaada wa kifedha na mafunzo ya kiufundi kwa mwaka mmoja, na baadaye jamii huendelea kusimamia urejeshaji huu kwa kujitegemea, chini ya ushauri wa maofisa ugani,”amesema Olila.
Pamoja na upandaji mikoko, mradi pia unawawezesha wananchi kushiriki kwenye shughuli mbadala za kiuchumi kama ufugaji wa nyuki, ambazo huchangia si tu kwenye hifadhi ya mazingira, bali pia kuongeza kipato cha kaya.
Mradi unatekelezwa kwenye wilaya za Mkinga na Pangani (Tanga), pamoja na Mkoani na Micheweni (Pemba), ambapo wananchi wamejengewa uwezo wa kushiriki kwenye uzalishaji wa mazao ya baharini kama mwani, majongoo bahari, kaa, na ufugaji wa samaki.
“Mpaka sasa tumewafikia zaidi ya wananchi 400, ambao wamepata mafunzo, msaada wa kiufundi na kifedha kupitia Bahari Mali. Hii imewawezesha kufanya shughuli endelevu, zenye tija na rafiki kwa mazingira,”.
Kwa upande wake, Mtafiti Mwandamizi kutoka Taasisi ya Utafiti wa Uvuvi Tanzania (TAFIRI), Rushingisha George,amesema tafiti zinaonesha ongezeko la asidi baharini, hali inayotishia viumbe na mazingira ya bahari.
“Kupitia tafiti hizi, tunahitaji kutoa elimu kwa jamii juu ya namna ya kukabiliana na changamoto kama hizi. Lakini pia ni muhimu kuwahusisha waandishi wa habari kwa kuwa wao ndiyo daraja kati ya watafiti, jamii na watunga sera,”amesema.
Pia amesema,upatikanaji wa taarifa sahihi kwa wakati ni nguzo muhimu katika kufanya maamuzi bora ya kimkakati kwenye masuala ya uhifadhi wa bahari.

Mkurugenzi Mtendaji wa JET, John Chikomo, amesema kuwa chama chake kimeona umuhimu wa kuwajengea uwezo waandishi wa habari,ili waweze kuielewa vyema dhana ya uchumi wa buluu na kuifikisha kwa jamii kwa usahihi.
“Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050 inaweka mkazo kwenye uchumi wa buluu. Tunataka waandishi wa habari za mazingira wajifunze kwa vitendo kuhusu miradi ya pwani na bahari, ili wawe mabalozi wa kuhamasisha hifadhi na maendeleo endelevu,”amesema Chikomo.
Katika mafunzo hayo ya siku nne, waandishi wa habari kutoka maeneo mbalimbali ya Tanzania walipata nafasi ya kutembelea miradi ya Bahari Mali, kushuhudia shughuli za urejeshaji wa mikoko, kilimo cha mwani, ufugaji wa nyasibahari na uhifadhi wa matumbawe kwenye vijiji vya Mkinga na Pangani.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako