March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maboresho yalivyoleta tija katika mashirika ya umma

Na Mwandishi Wetu,Timesmajiraonline,Dar

JUNI 10, 2025 Ofisi ya Msajili wa Hazina iliandika historia mpya, pale ilipokabidhi Serikalini hundi yenye thamani ya sh. trilioni 1.028 ambazo ni gawio kutokana na faida iliyotengenezwa na baadhi ya mashirika ya umma.

Gawio hilo lilikabidhiwa kwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Msajili za Hazina, Nehemiah Mchechu, ambaye alisema;

“Gawio hili ni la kihistoria. Haikuwahi kutokea ofisi ya msajili wa
hazina kukusanya kiasi kama hiki kufikia Sh Trilioni 1.” Kiasi hicho ya fedha ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6 kutoka sh. bilioni
691.6 kilichotolewa na mashirika hayo mwaka 2021.

“Hili ni ongezeko kubwa la mapato yanayokusanywa kutoka taasisi za umma na kampuni ambazo serikali inamiliki hisa chache,” alisema Mchechu.

Kadhalika makusanyo hayo ya kihistoria tangu kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Hazina mwaka 1959, ni ongezeko la asilimia 68 ya kiasi kilichokabidhiwa kipindi kama hicho mwaka 2024, na asilimia 34 ya makusanyo yote ya mwaka 2023/24, ambayo yalikuwa ni sh767 bilioni.

Taarifa za Ofisi ya Msajili wa Hazina zinaonesha kuwa vyanzo vikuu vya mapato hayo kwa mwaka huu ni gawio ambalo limechangia asilimia 63.9 ya mapato yote, huku michango mingine ya mapato ghafi ikichangia asilimia 29.7.

Mapato mengineyo yanajumuisha ziada, marejesho ya mikopo na riba pamoja na Mawasilisho yatokanayo na mtambo wa kuhakiki na kuwezesha mawasiliano (TTMS) yamechangia asilimia 6.4 ya mapato yote.

Mchechu anasema fedha za gawio (Sh1.028 trilioni) kimekusanywa kutoka katika taasisi na mashirika 213 (195 ya umma na 18 kampuni zenye hisa chache), ikimaanisha kuwa mashirika 57 (sawa na asilimia 22) hayakuchangia.

Serikali, kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina, inasimamia Mashirika ya Umma na ya Kisheria 253 na kati ya hayo, 218 yanatoa huduma, huku 35 yakifanya shughuli za kibiashara, ikiwa ni fursa ya kimkakati ya kuchochea ukuaji wa uchumi na uzalishaji wa mapato yasiyo ya kikodi.

***Anachotamani Rais Samia

Itakumbukwa kuwa Agosti 2024, Rais Dkt. Samia alieleza matamanio yake ya kuongezeka kwa ukusanyaji wa mapato yasiyo ya kikodi (kutoka kwa Mashirika ya Umma na Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache), kuchangia hadi ya asilimia 10 ya bajeti ya Serikali ndani ya miaka mitano, kutoka kiwango cha asilimia tatu ambacho kilikuwa kimefikiwa wakati huo.

Rais akionesha kuridhishwa na mwenendo wa utendaji wa mashirika ya umma, alisema Serikali inaendelea kuchukua hatua kuhakikisha mashirika ya umma yanakuwa na tija kwa taifa kwa kuzalisha faida, huku akihimiza watendaji kuongeza ubunifu.

“Lengo letu ni kufikia angalau shilingi trilioni 1.5 kwa mwaka ujao (2025/26). Nina imani tunaweza, nikutake, msajili wa hazina, kuzipitia taasisi zote na kuweka malengo mahsusi ya mapato kwa kila moja, ili tuweze kufikia azma hiyo,”alisema Rais Samia na kuongeza:

“Mageuzi ni pamoja na kuwa wabunifu, tusisubiri Serikali itatue kila changamoto inayotukabili kama taasisi, tutumie fursa mbalimbali zinazotuzunguka katika kutatua changamoto hizo ikiwemo soko la mitaji.”

Baadhi ya wasomi wamenukuliwa na Jarida la Public Investment linalotolewa na Ofiai ya Msajili wa Hazina wakisema ili kuwezesha mashirika la umma kuchangia zaidi kwenye Mfuko Mkuu wa Serikali, lazima zifanywe hatua za makusudi za kupanua wigo wa vyanzo vya mapato.

Profesa Abel Kinyondo, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alinukuliwa akisema hatua ya Rais Samia kuwa na mtazamo baadhi ya taasisi za umma kufanyakazi kibiashara unaweza kuongeza wigo wa mapato na kwamba dalili zinaoneha kuwa umeanza kuzaa matunda.

“Uchumi wetu rasmi bado ni mdogo sana. Serikali inapaswa kuendelea kuimarisha mazingira rafiki kwa biashara ili kuwahamasisha walioko kwenye sekta isiyo rasmi kuingia kwenye mfumo rasmi wa uchumi,” alisema Profesa Kinyondo.

Naye Dkt. Daudi Ndaki, mchumi kutoka Chuo Kikuu cha Mzumbe, yeye anasema kuwa wataalamu wanapaswa kusaidia serikali kuchunguza vyanzo vipya vya ubunifu vya mapato yasiyo ya kodi ili kuongeza mapato bila kuwalemea wachache.

“Hili linaendana na dira ya Rais Dkt. Samia, mbaye amekuwa
akisisitiza mara kwa mara umuhimu wa mfumo rafiki wa ukusanyaji kodi ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na wa nje,” anashauri Dkt. Ndaki.

Dkt. Tobias Swai, Mkuu wa Idara ya Fedha katika Shule ya Biashara ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, alishauri mashirika ya umma yawekeze katika sekta zinazogusa maisha ya Watanzania wengi, huku akitaja maeneo muhimu ya kuwekeza kuwa ni huduma za kifedha, bima, sekta ya ardhi, utalii, usafirishaji na kilimo.

***Msajili wa Hazina

Akizungumza na Vyombo vya Habari Juni 2, 2025 katika mkutano uliokuwa na lengo la kutoa taarifa kwa umma kuhusu hafla ya kukabidhi gawio kwa serikali, Msajili wa Hazina, Mchechu alisema mwenendo wa utoaji michango kutoka kwenye Taasisi na Mashirika ya Umma umekuwa ukibadilika kila mwaka na kuwa usiotabirika.

“Mwenendo wa utoaji gawio, kwa wastani, umekuwa ukiongezeka kwa asilimia 50 kila mwaka,”anasema Mchechu na kuongeza: “Idadi ya Taasisi na Mashirika ya Umma ambayo yamekuwa yakichangia imekuwa ikibadilika kila mwaka kwa kupanda na kushuka.”

Kwa mujibu wa Msajili huyo wa Hazina, kwa kipindi cha miaka mitatu (2021/22 – 2023/24) wastani wa Taasisi na Mashirika ya Umma 146 ndiyo yamekuwa yakitoa michango sawa na asilimia 59 ya taasisi zote.

Kadhalika, Mchechu anasema serikali pia inamiliki hisa chache katika kampuni 56, hali inayothibitisha ushiriki wake katika sekta binafsi, Ofisi ya Msajili wa Hazina ikiwa ndiye msimamizi wa ushiriki huo.

“Kuwa na hisa chache kunamaanisha udhibiti mdogo, lakini uwezo wa kuwa na ushawishi, ambao unaweza kuwa na athari mbalimbali za kiuchumi, kijamii, na kisiasa kulingana na sekta na malengo ya uwekezaji,” anasema Mchechu na kuongeza;

“Pamoja na ongezeko hilo, idadi ya Kampuni ambazo zimekuwa zikilipa gawio ni chache ikilinganishwa na jumla ya Kampuni ambazo Serikali ina hisa chache. Mfano katika mwaka 2023/24, ni Kampuni 17 tu kati ya 56 sawa na asilimia 3.”

Mchechu anasema mafanikio yanayoonekana hivi sasa ni matokeo ya nguvu ambayo wamekuwa wakipewa na Rais Samia, ambaye mara kadhaa amekuwa akitoa maelekezo mahsusi kuhusu utendaji na utekelezaji wa mpango wa kuwezesha mashirika ya umma yanakuwa sehemu ya kukuza uchumi wa nchi.

Mchechu anasema katika muktadha huo, utekelezaji wa mkakati wa kuboresha utendaji taasisi za umma kupitia ofisi yake ambayo yanajumuisha kuimarishwa kwa utaratibu wa ufuatiliaji na matumizi ya Mifumo ya TEHAMA, pia umechangia mafanikio ya ukuaji wa mapato.

Kwa mujibu wa Mchechu, tayari Ofisi ya Msajili wa Hazina imeunganisha mifumo kadhaa ya kifedha (ambayo ni PlanRep, ERMS, e-Watumishi na MUSE), hatua ambayo imeongeza uwazi na uwajibikaji katika usimamizi wa fedha za Umma
kwa kuwezesha upatikanaji wa taarifa halisi za matumizi katika taasisi na mashirika husika.

“Maboresho haya yamewezesha mifumo kubadilishana taarifa ipasavyo ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa agizo la Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan aliyetaka kuona mifumo inasomana,”anasema.

Hatua hizo za maboresho zaweza kuwa ni utekelezaji wa mapendekezo ya tafiti na ripoti mbalimbali za kitaalamu ikiwa Ripoti ya mwaka 2018 ya Tume ya Umoja wa Mataifa ya masuala ya Uchumi kwa Afrika.

Ripoti hiyo iliyopewa jina la nafasi ya Mapato yasiyotokana na Kodi katika kugharimia maendeleo endelevu, ikibainisha kuwa kuwa Tanzania kwa zaidi ya miaka 10 (1997 – 2018), haikuwa ikifanya vizuri katika ukusanyaji wa mapato ya aina hiyo , licha ya kuwa uwanda mpana wa vyanzo vya mapato.

“Mwelekeo wa jumla unaonesha kushuka kwa mapato yasiyotokana na kodi, hali inayoonesha kuwa kuna haja ya mkazo mpya wa kisera katika kuboresha ukusanyaji na utofauti wa vyanzo vya mapato hayo,” insomuch sehemu ya taarifa hiyo ambayo inatoa
mapendekezo kadhaa ya kuboresha ukusanyaji wa mapato yasiyotokana na kodi.

Miongoni mwa mapendekezo hayo ni kuimarishwa kwa mazingira ya kisera na kiutendaji kutokana na Tanzania kutajawa kuwa moja ya nchi ambazo ambazo zilikuwa na mifumo dhaifu ya ukusanyaji wa mapato yasiyotokana na kodi, hasa katika eneo la kutambua
vyanzo vya mapato na kuhakikisha uratibu kati ya ngazi ya kitaifa na serikali za mitaa.

***Hatua za serikali

Chini ya badiliko ambayo Serikali imeyafanya kupitia Ofisi ya Msajili wa Hazina ni pamoja na baadhi ya taasisi ziliongezewa mtaji ili kuziwezesha kuimarisha utendaji wake, hatua ambayo imeziwezesha kutengeneza faida ambayo imechangia ongezeko la gawio lililotolewa mwaka huu kwenda serikalini.

Kwa mujibu wa taarifa za Ofisi ya Msajili wa Hazina, taasisi ambazo ziliongezewa mtaji ni pamoja na Benki ya TCB (Tanzania Commercial Bank) iliyoongezewa mtaji wa shilingi Bilioni 131, Shirila la Umeme Tanzania (Tanesco) lililopewa mtaji wa Sh. Trilioni 2.4 na Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC ambalo
liliongezewa mtaji wa Sh.Trilioni 2.7.

Taarifa zinaonyesha kuwa tayari taasisi hizo tatu zimeanza kupata faida ambapo mwaka 2024 TCB ilitengeneza faida shilingi bilioni 31.6. Kadhlika katika mwaka huo, faida ya Tanesco iliongezeka kutoka Sh. bilioni 8.9 hadi Sh. bilioni 22.8, wakati TPDC katika mwaka wa fedha 2023/24 faida yake iliongezeka kutoka Sh.
bilioni 159.6 hadi Sh. bilioni 306.

Mafanikio ya TPDC pia yanatajwa katika Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), ambayo inaeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2023/2024, shirika hilo lilipata faida ya Sh. bilioni 248.75.

Mashirika mengine yanayotajwa na ripoti hiyo ya CAG ni Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA) iliyopata faida ya Sh. bilioni 140.48 na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopata faida ya sh. bilioni 242.9.

Kwa upande mwingine mabadiliko yanayofanywa yamewezesha taasisi 57 kupewa uhuru wa kujiendesha ili kufikia ufanisi uliotarajiwa wakati wa uanzishwaji wake, huku taasisi 14 zikiuganishwa, kuundwa kwa tasisi sita mpya na kufutwa kwa taasisi tatu, uamuzi ambao ulitangazwa na serikali Desemba 15,
2023.

“Serikali iliunda timu ya wataalamu kwa ajili ya kufanya uchambuzi wa kina kuhusu utendaji wa mashirika ya umma kwa lengo la kubainisha changamoto za kiutendaji na kupendekeza hatua za kuchukua katika kuongeza tija ya maendeleo ya nchi,” alisema Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo.

***Changamoto za mashirika ya umma

Licha ya mafanikio haya, mashirika ya umma bado yanakabiliwa na changamoto kadhaa zinazohitaji kutatuliwa kwa haraka.

Kulingana na ripoti ya CAG ya mwaka 2023/2024, mashirika kama Kama Shirika la Ndege Tanzania (ATCL), Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) pamoja na Shirika la Posta Tanzania yameendelea kupata hasara za mabilioni ya shilingi.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, Kampuni ya ATCL imepata hasara ya Sh. bilioni 91.8, huku TTCL ikipata hasara ya Sh. bilioni 27.7.
Changamoto za kiutendaji, udhaifu wa usimamizi na madeni yanayofikia jumla ya Shilingi za Kitanzania trilioni 7.23
hadi kufikia Juni 2024, yamekuwa mzigo mkubwa kwa mashirika haya.

Kati ya mashirika 215 yaliyoteuliwa, mashirika 58 yamepata hasara kwa miaka miwili mfululizo, yaani 2021/2022 na 2022/2023, hali inayoonyesha kuwa licha ya mafanikio makubwa kwa mashirika kadhaa, bado juhudi zinahitajika ili kuhakikisha kuwa mashirika yote yanafanya kazi kwa ufanisi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Sabatho Nyamsenda amesema kuwa uongozi unapaswa kuimarishwa kwa kuleta watendaji mahiri na kujifunza kutoka kwa nchi kama China na Ethiopia, ambazo zinaendesha mashirika ya umma yenye faida.

Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Charles Kichere anapendekeza kuimarisha mifumo ya uwajibikaji, kupunguza gharama za uendeshaji, na kuhakikisha usimamizi bora wa mikopo na dhamana, hasa katika benki za umma.