March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Yas yadhamini mashindano ya Ndondo Cup 2025

Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online

KAMPUNI ya Mawasiliano hapa nchini, Yas
imetangaza rasmi kudhamini Mashindano ya Ndondo Cup kwa mwaka huu wa 2025.

Yas na Mixx, inajivunia kuwa sehemu ya mashindano hayo ya kihistoria yanayoshirikisha timu za vijana kutoka maeneo mbalimbali hapa nchini.

Akizungumza mara baada kutangaza rasmi udhamini huo, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Dar es Salaam, Robert Kasulwa amesema Ndondo cup imejijengea heshima si tu kwa ushindani mkali wa soka, bali pia kwa mchango wake mkubwa katika kuibua vipaji vya vijana na kuvifikisha kwenye viwango vya juu, kitaifa na kimataifa.

“Tunathibitisha dhamira yetu ya muda mrefu ya kuendeleza michezo, kuibua vipaji vipya na kubadilisha fikra na mitazamo ya vijana wa kitanzania ya kuanzia pale walipo kama kauli mbiu ya Kampeni yetu ya ‘Anzia Ulipo’ inavyosema,” amesema.

Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Dar es Salaam Kusini, Robert Kasulwa (katikati), akiwa na kurugenzi wa Yas Kanda ya Kaskazini, Aidan Komba (wa pili kulia), akizungumza wakati wa hafla ya kuitambulisha Yas kama mdhamini mpya wa michuano ya Ndondo Cup. Hafla ya tukio ili ilifanyika juzi jijini Dar es Salaam. Meneja Matukio na Udhamini Yas,David Maisori (kulia), Muasisi wa Michuano ya Ndondo Cup, Shaffih Dauda (wa pili kushoto) na Mratibu wa Michuano hiyo Yahya Mkazuzu (kushoto).

Amesema, mwezi uliopita Yas ilizindua Kampeni ya Anzia Ulipo. Kampeni inayotoa wito kwa kila Mtanzania mwenye ndoto na ari ya kubadilisha maisha yake afanye hivyo kwa kutumia teknolojia.

Aidha, amesema kila mmoja anayo picha ya mafanikio yake ila wengi hatuanzi kupiga hatua kwakuwa tunasubiria wakati sahihi au mtu fulani atushike mkono.

“Leo hii, kupitia ushirikiano huu na Ndondo Cup, tunajivunia kuendelea kuona kampeni yetu ikipata uhalisia.

“Ndondo Cup ni jukwaa halisi la “Anzia Ulipo”, vijana wanaanza pale walipo, wanatumia vipaji vyao, wanajituma, na hatimaye wanapata nafasi ya kutambulika katika ligi za kitaifa na kimataifa.

“Kama mtoa huduma kinara wa mawasiliano ya kidigitali nchini, Yas tunaamini kuwa teknolojia ndiyo daraja la mafanikio ya sasa.

“Kwa kutumia mtandao wetu bora wa 4G na 5G ulionea nchi nzima pamoja na bidhaa zetu zilizobuniwa kukidhi mahitaji ya kila Mtanzania, tunawapa vijana fursa ya kujiamini, kujitangaza, na kutimiza ndoto zao,” amesema.

Hata hivyo alisema, Ndondo Cup hayahusiani na soka tu bali pia yanahusu ustawi wa jamii zetu, yanahusu afya, elimu, ajira na ndoto za vijana wa kitanzania.

“Kwa niaba ya Yas na Mixx, nawahakikishia washiriki na mashabiki kuwa tutahakikisha msimu huu wa Ndondo Cup unakuwa wa kipekee, wa kidigitali, na wenye kuleta fursa halisi kwa maelfu ya vijana nchini,” amesema Kasulwa.

Kwa upande wake Muasisi wa Ndondo Cup Shaffih Dauda ameishukuru Kampuni ya Yas, kwa kukubali kudhamini mashindano hayo anaamini mwaka huu yatakuwa ya kipekee.

“Ndondo Cup, sio tu mpira ni uchumi , ni maisha na ni hatua mpya, hii si tu kuhusu nani anashinda kombe. Hii ni kuhusu nani anabadilika kimaisha kupitia mpira.

“Na huu ndio mpango wa Tanzania mpya na mitaa yenye ndoto hai ambayo Naiita THE FUTURE”

“Kwa timu shiriki zitapata nafasi ya kushiriki Mafunzo ya Uongozi na Biashara Kwa kushirikiana na SIDO, VETA na taasisi nyingine.

“Watapata kujua kuhusu uongozi, ujasiriamali, TEHAMA na menejimenti ya vikundi. Yote hii Tunawajenga vijana kuwa viongozi wa kweli wa uchumi,” amesema Dauda.