Na Mwandishi Wetu, Timesmajiraonline,Tabora
MKUU wa Wilaya ya Tabora, Upendo Wella, amewataka wakulima wa tumbaku kwenda kutekeleza kwa vitendo moja ya nguzo muhimu iliyoainishwa kwenye Dira ya Taifa ya 2050 ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilifu wa mabadiliko ya tabia nchi.
DC Wella ametoa maagizo hayo wakati akikabidhi Pikipiki 60 zenye thamani ya zaidi ya sh. Milioni 178 zilizotolewa na Kampuni ya Alliance One kwa wakulima wake walioshinda bahati
nasibu iliyochezeshwa na Kampuni hiyo kwa wakulima wake.
Amesema Dira ya Taifa iliyozinduliwa na Rais Daktari Samia Suluhu Hassan imejikita katika misingi minne ya utawala bora, amani, usalama pamoja na utulivu na dira pia imezitaja nguzo tatu ikiwemo ya uhifadhi wa mazingira na ustahimilifu wa mabadiliko ya tabia nchi.

“Tusipokuwa na mazingira endelevu, tusiposhirikiana katika utunzaji wa mazingira, vyanzo vya maji na uhifadhi wa mazingira tunayofanyia kilimo, basi hata hiki kilimo tunachokitegemea
hakitakuwa endelevu,” alisema Upendo Wella.
Amesema Pikipiki hizo ni sehemu ya juhudi za Kampuni ya Alliance One katika kuwawezesha wakulima utii wa kanuni za kilimo bora kukuza ufanisi katika uzalishaji wa Tumbaku na amewataka wakulima kwenda kuongeza uzalishaji na kuhamasisha Wakulima wengine kuzingatia kanuni za kilimo.
Awali katika taarifa yake, Msemaji wa Alliance One, Wakili John Magoti, amesema wakulima 60 waliopata zawadi za Pikipiki ni wale waliokidhi vigezo vilivyowekwa na Kampuni hiyo, ambavyo ni usahihi wa uzani wa marobota pamoja ukubwa sahihi wa mafungu.
Amevitaja vigezo vingine kuwa ni matumizi ya vitambaa vya hessiani, Kamba ya pamba, Marobota yenye umbo la la mraba kulingana na vipimo vya bosi la kufungia, Tumbaku safi isiyo na
uchafu wowote, maji au vitu visivyo vya Tumbaku, Ubora wa Tumbaku kwa kuzingatia rangi, sehemu ya mmea, upangaji wa madaraja na ulinganifu wa Tumbaku ndani ya kila robota.
Amesema wakulima waliopewa Pikipiki wametekeleza hayo mambo saba aliyoyaelezea na kwamba wameonesha Nidhamu na juhudi katika uzalishaji na amewaomba wakulima wengine
wa Tumbaku kufanya bidii na kutekeleza hayo katika misimu ijayo.
Nao Wakulima waliobahatika kupata Pikipiki hizo wamelezea furaha yao, ambapo Benjamin Lugho kutoka Kaliua alisema Kampuni hiyo inawajali Wakulima wake maana mbali Pikipiki lakini
walitoa fedha ya ziada kwa Wakulima kama motisha katika kuzalisha tumbaku bora.

Oleni Kadyagenzi mkulima kutoka Kasulu Kigoma amesema Pikipiki hiyo inamsaidia kubeba mbolea na mazao mengine kutoka eneo moja hadi jingine na kumpunguzia gharama alizokuwa akizitumia katika usafiri wa kukodi huku Mkulima Dotto Maiti kutoka Sikonge ameipongeza Kampuni ya Alliance one kwa kuwajali wakulima wake.
Jumla ya Wakulima 60 kati ya zaidi ya 2,000 waliokidhi vigenzo wamepata zawadi za Pikipiki baada ya kushinda Bahati nasifu zilizochezeshwa na Kampuni ya Alliance one kwa lengo la
kuwahamasisha Wakulima kuzalisha Tumbaku bora na kuifikisha kwenye masoko kwa wakati.

More Stories
Kihenzile ahamasisha uwekezaji sekta ya anga
Wafanyabiashara watuliza wananchi hofu ya bei ya bidhaa
TISEZA kuanzisha madawati ya uwekezaji kila Halmashauri za Wilaya