March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

INEC yavitoa hofu vyama vya siasa

Na Allan Kitwe, Timesmajira Online-Tabora

TUME Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC),imesema itavitendea haki sawa vyama vya siasa vitakavyoshiriki uchaguzi mkuu Oktoba mwaka huu.

Hayo yamebainishwa na Kamishna wa Tume hiyo,Magdalena Rwebangira,wakati akifungua mafunzo ya siku 3 kwa waratibu,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka Mikoa ya Tabora na Kigoma yanayofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agoustino(SAUT),Mjini Tabora.

Kamishna wa Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) Magdalena Rwebangira akifungua mafunzo ya siku 3 kwa Waratibu, Wasimamizi na Wasimamizi Wasaidizi wa Uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka Mikoa ya Tabora na Kigoma katika ukumbi wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agostino (SAUT) Mjini Tabora

Amesema kuwa Tume imeleta mafunzo hayo ili kuwaandaa vyema,waratibu, wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi huo ili waweze kutekeleza majukumu yao ipasavyo.

Pia amesisitiza kuwa Tume imejipanga vizuri ili kuhakikisha taratibu zote za kikatiba na kisheria zinazingatiwa na kufuatwa, na wote waliopewa dhamana ya kusimamia uchaguzi huo ili kuhakikisha unakuwa na ufanisi.

Hata hivyo amewataka washiriki wa mafunzo hayo,kusoma kwa umakini katiba, sheria, kanuni, miongozo na melekezo yote yanayotolewa na Tume,ili kuwarahisishia utekelezaji jukumu hilo na kuepusha malalamiko na vurugu wakati wa mchakato wa uchaguzi.

‘Shirikisheni vyama vya siasa vyote vitakavyoshiriki uchaguzi katika hatua zote za mchakato wa uchaguzi huo, hakikisheni kanuni, taratibu, sheria, miongozo na maelekezo yote ya tume yanazingatiwa ili kuepusha malalamiko,” amesema.

Aidha amewataka kushirikisha wadau wanaostahili katika maeneo ambayo Tume imeelekeza na kufanya utambuzi wa vituo vya kupigia kura mapema na kubaini mahitaji maalumu vya vituo husika ili uchaguzi ufanyike kwa amani na utulivu.

Kuhusu ajira za watendaji wa vituo vya kupigia kura, Kamishna amewataka kutoingiza watu wasio na sifa kwa kigezo cha undugu au jamaa bali wazingatie weledi, uzalendo, uadilifu na uchapa kazi.

Baadhi ya waratibu,wasimamizi na wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya Jimbo kutoka Mikoa ya Tabora na Kigoma wakimsikiliza Kamishna wa INEC Magdalena Rwebangira,(hayupo pichani)

Amewataka kukagua na kuhakiki vifaa vya uchaguzi wanavyopokea na kuvisambaza katika maeneo husika kwa wakati, kutoa taarifa wakati wa kuapisha mawakala na kuhakikisha vyama vinapewa orodha ya vituo vya kupigia kura ili viweze kupanga mawakala wao vizuri.

Akiongea kwa niaba ya Washiriki wenzake, Msimamizi wa Uchaguzi wa Manispaa ya Tabora,Paschal Matagi,ameeleza kuwa mafunzo hayo ni muhimu na yatawasaidia kufanikisha jukumu hilo kwa ufanisi.