March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Maofisa Elimu watakiwa kuweka mipango ya kuwainua kiuchumi walimu

Na Esther Macha,Timesmajira Online-Rungwe

Mkuu wa Mkoa wa Mbeya,Beno Malisa,amewaagiza Maofisa Elimu Mikoa ya Nyanda za Juu Kusini,kuweka mipango maalumu ya kuwainua kiuchumi walimu kupitia semina mbalimbali za elimu ya fedha ili waepuke kutegemea mshahara tu.

Malisa,ametoa agizo hilo, Julai 15,2025 wakati akifungua mafunzo ya awamu ya tatu kwa walimu ,juu ya matumizi ya TEHAMA kwa shule za sekondari mikoa ya Iringa,Katavi,Mbeya,Njombe, Ruvuma, Rukwa na Songwe yanayoendelea katika Chuo cha Ualimu Msasani wilayani Rungwe.

Malisa amesema walimu wengi nchini,wamejikuta wanaingia katika madeni ya mikopo hali inayosababisha maisha yao kuwa magumu, hivyo amewaasa kuwa ni wakati sahihi wa kujinasua katika mtego huo na kuanza kujiimarisha kiuchumi nje ya kazi yao ya ualimu.

Pia amesema,ipo haja Serikali kuongeza idadi ya washiriki wa mafunzo ya TEHAMA kwa wanawake ambao idadi yao ni ndogo.

“Wengi mliopo hapa ni vijana,tumieni fursa vizuri kwa siku tano mtakazokaa, kwani tunaamini vijana wepesi kushika na kuelewa na Kazi haitakua nzito”amesema Mkuu huyo wa Mkoa wa Mbeya.

Sanjari na hayo Malisa,amewapongeza walimu kwa kazi wanayoifanya ya kuwalea na kuwafunza watoto huku akiwasihi kuweka mkazo katika kufundisha,kutunza na kulinda maadili ya Kitanzania kwani ulimwengu wa sasa umefikia pabaya.

“Kwa miaka ya hivi karibuni kesi nyingi zinazokuja wanaotuhumiwa ni walimu na hatutaki kusema kuwa walimu ndo chachu ya changamoto hii,hivyo sadieni kuwa sababu ya watoto kuwa na maadili mema,”.

Kwa upande wake Mratibu wa mradi wa kuimarisha ubora wa elimu ya sekondari kutoka ofisi ya Rais TAMISEMI (Sequip ),Robert Msigwa,amesema Wizara ya Elimu kwa kushirikiana na ofisi hiyo,imekuwa ikitekeleza majukumu mbalimbali,ambapo shule za sekondari 830 zimejengwa na kuna shule 26, za bweni za wasichana zimejengwa kila Mkoa.

Huku shule saba za wavulana zimejengwa katika Kanda saba ,shule 103 kwa ajili ya utekelezaji wa mkondo wa amali.

Mwalimu Zawadi Kasimu kutoka shule ya sekondari Matalawe mkoani Ruvuma, amesema kuwa baada ya mafunzo hayo watakuwa wamepata uelewa wa namna ya kutumia TEHAMA.

.