November 23, 2024

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa (katikati) akipunga mkono kwa baadhi ya wakazi na mashuhuda wengine waliofika katika uzinduzi wa safari za treni za mizigo katika reli ya Dar-Tanga- Kilimanjaro uliofanyika mjini Moshi, Kilimanjaro.

JPM aweka historia reli ya Tanga

Na Eric Toroka, TimesMajira Online

MIAKA 30 iliyopita, usafiri wa treni wa abiria na mizigo ulikuwa ukitumiwa sana na wakazi wa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, lakini baadaye usafiri huo ulifutika na kuwa kadhia kubwa kwa wananchi wa kanda hiyo.

Kutokana na ukosefu wa usafirishaji wa bidhaa mbalimbali katika mikoa ya kaskazini, bidhaa nyingi zilikuwa zikipatikana kwa uchache, kwani usafiri wake ulikuwa wa kutumia magari ya mizigo yaani malori na mabasi.

Lakini katika uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano unaoongozwa na Dkt.John Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ulitafakari sana na kuamua kurejesha huduma za reli kanda ya kaskazini, ikianzia Dar es Salaam hadi mkoani Arusha na ile ya kutoka jijini Tanga hadi mkoani Arusha.

Waziri Mkuu,Kassim Majaliwa (katikati) akipunga mkono kwa baadhi ya wakazi na mashuhuda wengine waliofika katika uzinduzi wa safari za treni za mizigo katika reli ya Dar-Tanga- Kilimanjaro.

Julai 20,2020, ulifanyika uzinduzi wa safari ya treni ya abiria na mizigo kutoka Tanga hadi Moshi mkoani Kilimanjaro, lakini Agosti 24,2020 umefanyika uzinduzi mwingine wa treni ya abiria na mizigo kwa majaribio kutoka Tanga hadi Arusha.

Katika uzinduzi huo, treni ya mizigo iliyokuwa na mabehewa nane yaliyokuwa na saruji kutoka Kampuni ya Saruji Tanga (Tanga Cement), yenye uzito wa tani 320, iliwasili jijini Arusha, ikishuhudia na maelfu ya wakazi wa mikoa ya kanda ya kaskazini, wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Iddi Kimanta.

Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Idd Kimanta wakati akipokea treni ya abiria na mizigo, alisema kama saruji hiyo kutoka kampuni ya Tanga Cement ingesafirishwa kwa njia ya barabara, ingepakiwa kwenye malori 16, lakini usafirishaji kwa njia ya treni ni wa uhakika na gharama zake hazimuumizi mzalishaji.

Amesema usafiri huo utawarahisishia wananchi wa mikoa ya Arusha, Kilimanjaro na Manyara upatikanaji wa saruji kutoka Tanga Cement bila matatizo, hivyo watafannya shughuli zao za ujenzi na kukamilisha kwa wakati waliojipangia.

“Usafiri huu utarahisisha mambo mengi na utafungua fursa nyingi kwa wakazi wa Mkoa wa Arusha na hata majirani zetu, ninaomba tutunze miundombinu hii, ukiona dalili zozote za kuihujumu toa taarifa,” anasema Kimanta.

katika stesheni ya Krokon jijini Arusha ikiwa na shehena ya saruji tani 320 kutoka Kampuni ya Tanga Cement ya jijini Tanga. Treni hilo lililokuwa na mabehewa nane.

Wakati wa mapokezi na kukabidhiana saruji hiyo iliyofikishwa katika stesheni ya Krokon jijini Arusha, pia alikuwepo Mkuu wa Kilimanjaro, Anna Mgwira, Katibu wa Unezi na Itikadi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hamprey Polepole, wakuu wa wilaya za Arusha Mjini, Kenani Kihongosi na Jerry Muro wa Arumeru.

Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Kihongosi amesema kukamilika kwa ukarabati wa miundombinu ya reli kutoka Tanga hadi Arusha, kutaongeza ukuaji wa uchumi wa mkoa mikoa ya Kanda ya Kaskazini, kama walivyoanza kampuni ya Tanga Cement kupeleka saruji katika mikoa hiyo.

“Tunashukuru sana uongozi wetu wa Serikali ya Awamu ya Tano, umehakikisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inaboreshwa na kutoa fursa za kibiashara kwa wananchi wake.

Amesema watahakikisha wanalinda miundombinu ya reli kwa nguvu zao zote, akishirikiana na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru ambako inapita, Jerry Muro na wenzao wa Mkoa wa Kilimanjaro.

“Mimi kama Mkuu wa Wilaya ya Arusha, kwa kushirikiana na mwenzangu, Jerry Muro wa Arumeru, tutahakikisha tunalinda miundombinu ya reli hii usiku na mchana, wananchi mlio pembeni ya reli tunaomba ushirikiano wetu katika ulinzi,” anasema Kihongozi.

Kihongosi anawapongezi Tanga Cement kwa kuwa kampuni ya kwanza kusafirisha bidhaa yake kwa njia ya reli, akawataka kuhakikisha saruji wanayozalisha haikauki mkoani Arusha.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa, kwa upande wake amesema kuwa, gharama za kufufua reli ni Sh. bilioni 14, fedha ambazo ni kodi ya wananchi.

Amesema treni ya abiria ilisitishwa kufanya safari zake mwaka 1994, wakati ya mizigo kwa muda wa miaka 12, ilikuwa haifanyi kazi, lakini sasa huduma hizo zinarejeshwa, ambapo tayari safari za majaribio zimeonekana kupata mafanikio makubwa.

Kadogosa amesema kuwa, malengo makubwa ya shirika hilo ni kuhakikisha wanajenga treni ya kisasa kutoka Tanga-Arusha hadi Musoma mkoani Mara, ikiwa ni jitihada za Rais Dkt. John Pombe Magufuli.

Mtendaji Mkaazi wa Kampuni ya Tanga Cement, Mhandisi Ben Lemakiwanda chao ambacho ni wazalisha wa Simba Cement, wamefurahia uzinduzi wa treni hiyo kwani itawasaidia kufikisha bidhaa zao kwa wateja wakubwa na wadogo waliopo Kanda ya Kaskazini kwa haraka na uhakika zaidi.

“Uzinduzi huu wa treni ya mizigo tumeufurahia sana, saruji yetu hii tungetumia malori mengi kuifikisha Arusha tena kwa nyakati tofauti, badala yake imefika kwa wakati mmoja,” anasema Mhandisi Lema.

Mhandisi Lema ameipongeza serikali kwam kuboresha miundombinu ya usafirishaji ikiwemo treni ya abiria na mizigo na kwamba inawapa uhakika wa kulifikia soko lao kubwa, hasa katika mikoa ya Kilimanjaro, Arusha na Manyara.

“Uwepo wa treni ya kutoka Tanga kwenda Arusha ni fursa kubwa kwetu Tanga Cement katika uzalishaji wa bidhaa zetu hasa saruji chapa Simba na kuwafikia wateja wetu na watumiaji wa Simba Cement kwa urahisi zaidi,” anasema.

Anasema kwamba, zipo faida za kuwepo kwa treni ya mizigo na abiria, moja kubwa ni uhai wa barabara, kwani zinapunguza idadi ya magari ya mizigo mizito barabarani na wananchi kujipatia ajira na kujiingizia kipato.

Mhandisi Lema anawaomba Shirika la Reli Tanznaia (TRC), kufikiria kubeba mawe ya gypsum kutoka Makanya mkoani Kilimanjaro na kuipeleka Tanga, kwani mawe hayo ni moja ya malighafi muhimu zinazotumika katika utengenezaji wa saruji.

“Tunawaomba wenzetu wa TRC, wafikirie kubeba mawe ya gypsum kutoka Makanya mkoani Kilimanjaro hadi Tanga, ambako kuna kiwanda chetu cha Tanga Cement, mawe hayo ni muhimu sana kwenye uzalishaji wa saruji,” anasema.

Kwa upande wa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Hamphrey Polepole, amewaka wakazi wa Arusha na mikoa ya jirani kuhakikisha wanatumia usafiri huo kwani bei ya tiketi kwa abiria itakuwa ya chini.

Polepole anasema, kuwasili kwa treni ya mizigo, ajira nyingi zitafunguka, wakiwemo mama lishe watafanya biashara zao za chakula, vijana wao watapata ajira ya kushusha mizigo kama watakavyoshusha saruji kutoka Tanga Cement ilikuwa kwenye mabahewa nane yaliyopokelewa.

“Hii ni fursa kubwa sana, vijana changamkieni ajira zitakazotolewa hapa stesheni Krokon, kama ya kushusha saruji kwenye mabehewa. Nawapongeza sana Tanga Cement kwa kuamua kutumia usafiri wa treni kusafirisha saruji yenu,

“Pia, nawapongeza TRC kwa kukarabati miundombinu ya reli na hata kufanikiwa kufanya majaribio ya treni ya mizigo na abiria,” anasema Polepole.

Kukamilika kwa reli ya Tanga – Arusha na kuanza kutoa huduma ni mwendelezo wa utekelezaji wa dhamira ya Serikali ya Awamu ya Tano kuhakikisha miundombinu ya usafiri na usafirishaji inafaidika na fursa ya kijiografia iliyopo nchini kwa kutoa huduma za usafiri na uchukuzi wa reli kwa uhakika, usalama na kwa gharama nafuu.

Wataalamu wa masuala ya usafirishaji duniani wanaeleza kuwa, matumizi ya reli kwa ajili ya usafirishaji wa shehena, hupunguza gharama za bidhaa kwa asilimia kati ya 30 na 40.

Pia, matumizi ya reli huwa ni kichocheo kikubwa cha ukuaji wa uchumi kutokana na ukweli kwamba, kupitia usafiri wa reli unaweza kusafirisha mizigo mingi kwa haraka na kwa wakati mmoja kwenda kwa mlaji.