
Na Joyce Kasiki, TimesMajira Online
KATIKA hatua kubwa ya kuimarisha sekta ya kilimo cha mboga mboga nchini, Kituo cha Utafiti wa Kilimo TARI Tengeru kupitia kwa Mtafiti Mwandamizi Emmanuel Laswai, kimetambulisha aina mpya 22 za mbegu bora za mbogamboga zenye uwezo wa kukidhi mahitaji ya wakulima wa sasa na wadau wote walioko kwenye mnyororo wa thamani wa mazao hayo.
Mbegu hizo mpya ni pamoja na nyanya, pilipili (ikiwemo pilipili hoho na abanero), pamoja na ngogwe maarufu kama nyanyachungu. Kila mbegu imeboreshwa kisayansi ili kuwa na uwezo wa kutoa mazao mengi, kustahimili magonjwa na changamoto za mabadiliko ya tabianchi, huku zikilenga pia mahitaji ya soko la kitaifa na kimataifa.
Kurudi kwa vinyanya vya asili
Akizungumza kwa msisimko mkubwa, Laswai alieleza kuhusu mafanikio makubwa katika kurejesha nyanya aina ya cheri vinyanya vidogovidogo vilivyokuwa vimepotea sokoni kwa muda mrefu.
Amesema ,kwa sasa, TARI imefanikiwa si tu kuzirudisha, bali pia kuziboresha ili ziwe na virutubisho vingi, uzalishaji wa juu, na upinzani mkubwa dhidi ya magonjwa huku akisema,aina hii inalenga soko la watalii na mahoteli, hasa jijini Arusha na Dar es Salaam, ambako vinatumika sana katika maandalizi ya salad.
Vile vile amesema,Mbegu mpya za hoho nazo zimechukua nafasi yake. “Kwa mara ya kwanza tunazindua mbegu za pilipili hoho za rangi nyekundu na njano ambazo zinaweza kulimwa hata kwenye mashamba ya kawaida, si lazima vitalunyumba kama ilivyokuwa zamani,” alisema Kaswai.
Hii ni habari njema kwa wakulima wadogo wanaotaka kuingia kwenye kilimo cha thamani kubwa bila gharama kubwa za miundombinu.
Pia amesema zipo mbegu mpya ya pilipili kali aina ya abanero, maarufu kwa ladha yake kali na harufu ya kipekee ambapo amesema,mbegu hizi zina kinga dhidi ya magonjwa ya virusi na bakteria, huku zikiwa na rangi mbalimbali kama njano, machungwa na nyekundu , kitu kinachoongeza mvuto wake sokoni, hasa kwa soko la bidhaa za viwandani na chakula cha haraka .
Katika hatua ya kurudisha urithi wa chakula cha Kiafrika, TARI Tengeru imetoa mbegu tatu mpya za ngogwe (nyanyachungu). Moja kati ya hizo ni ile ya zamani yenye uchungu wa asili, aina ya mshumaa, ambayo imekuwa ikiuliziwa sana na wakulima na walaji. Kaswai alieleza kuwa ladha ya uchungu imeboreshwa ili kukidhi mahitaji ya walaji wa sasa wanaopenda ladha hiyo ya kipekee ambayo ndiyo hulka halisi ya nyanyachungu.
Ametumia nafasi hiyo kuwaalika wakulima wote nchini, wawe ni wakubwa au wadogo, kuja kuchukua mbegu hizi bora.
“Tumezifanyia kazi miaka mingi na sasa tuko tayari kuona kilimo cha mbogamboga kikibadilika kwa tija, faida na kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi,” alisema mtafiti huyo mwandamizi.
Kwa mbegu hizi 22 mpya, TARI Tengeru inatoa mchango mkubwa si tu katika kuimarisha kilimo cha bustani, bali pia kuinua kipato cha wakulima, kuimarisha lishe bora na kusukuma mbele ajenda ya usalama wa chakula .

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi