March 7, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Mwanasheria Mkuu wa Serikali Aitaka OCPD kukamilisha ufasili wa Sheria za Uchaguzi kabla ya Uchaguzi Mkuu

Na Joyce Kasiki,Timesmajira online

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, ameihimiza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kuhakikisha inakamilisha zoezi la ufasili wa sheria zote muhimu kwa lugha ya Kiswahili, hususan zile zinazohusiana na uchaguzi mkuu na kanuni zake, kabla ya kufanyika kwa uchaguzi mkuu unaotarajiwa mwaka huu.

Johari alitoa wito huo alipotembelea banda la OCPD katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Dar es Salaam (SABASABA) yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam, ambapo pia alipata fursa ya kujifunza kuhusu huduma mbalimbali zinazotolewa na ofisi hiyo pamoja na changamoto na maoni ya wananchi wanaotembelea banda hilo.

“Nafikiri tuendelee kuongeza jitihada katika kazi yetu ya kufanya ufasili wa sheria. Kwa kufanya hivyo, tutawezesha wananchi kupata haki zao kwa urahisi zaidi, hasa kupitia sheria za uchaguzi na kanuni zake ambazo zinapaswa kupatikana kwa lugha ya Kiswahili,” alisisitiza Mhe. Johari.

Aidha, aliipongeza OCPD kwa kazi nzuri inayoifanya, hususan katika kutoa elimu kwa umma kupitia ushiriki wao kwenye maonesho hayo, pamoja na utekelezaji wa majukumu mengine ya kisheria waliyopewa kwa mujibu wa sheria.

Awali, Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD, Bi. Mariam Possi, alimweleza Mwanasheria Mkuu kuwa wananchi wengi wanaotembelea banda hilo huonesha shauku ya kufahamu mchakato mzima wa utungaji wa sheria, kuanzia hatua za awali hadi sheria kusainiwa na Rais. Pia wanataka kujua kuhusu urekebishaji wa sheria, umuhimu wake, na hatua zilizofikiwa katika ufasili wa sheria kutoka lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili.

“Katika kipindi chote cha maonesho haya, tumepokea wananchi na wadau mbalimbali wa sheria kutoka maeneo tofauti nchini. Wengi wanataka kuelewa majukumu ya Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria, jinsi wanavyoweza kupata sheria zilizorekebishwa – toleo la mwaka 2023 – pamoja na sheria ambazo kwa sasa zipo katika hatua za mwisho za kufanyiwa ufasili kwa Kiswahili,” alifafanua Bi. Possi.

Aliongeza kuwa ofisi yao inatoa elimu kwa wananchi kwa umakini na kwa kuzingatia sheria na miongozo rasmi, huku akisisitiza kuwa Serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kushirikiana na OCPD, inaendelea kutumia njia mbalimbali kuhakikisha sheria hizo zinafikika kwa wananchi wote, ili waweze kuzisoma, kuzitafsiri kwa uelewa wa kawaida, na kuzitumia katika kudai haki na kutekeleza wajibu wao kama raia.