Na Joyce Kasiki,Timesmajira online
KAMISHNA wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, Bw. Nyanda Shuli, ameipongeza Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria (OCPD) kwa juhudi zake za kufanyia kazi mapendekezo ya mabadiliko ya sheria mbalimbali yanayowasilishwa na wananchi kutoka maeneo mbalimbali nchini.
Kamishna Shuli alitoa pongezi hizo alipotembelea banda la Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea katika Viwanja vya Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, jijini Dar es Salaam.
“Ofisi hii inatoa huduma zinazofanana sana na kazi tunazozifanya sisi. Tunapokea mapendekezo kutoka kwa wananchi na wadau kuhusu sheria zinazohitaji marekebisho, ambapo hatimaye mapendekezo hayo hupitia kwenu kwa ajili ya kuyaandikia na kuyafanyia marekebisho kabla ya kupelekwa bungeni. Kwa hiyo, sisi ni wadau wakubwa katika kuhakikisha sheria zetu zinakwenda na wakati,” alieleza Kamishna Shuli.
Akitoa mfano halisi, Kamishna Shuli alieleza kuwa wakati walipotembelea mikoa ya kusini kwa shughuli ya uchunguzi, walikutana na Jaji Mfawidhi wa Kanda ya Kusini ambaye aliibua hoja kuhusu sheria ya uhujumu uchumi ambayo awali ilihusisha pia nyara kama kwato za swala na pembe za digidigi kuwa ni miongoni mwa vielelezo vya makosa ya uhujumu uchumi.
“Kwa kweli, mazingira ya sheria hiyo hayakuwa yanalingana tena na hali halisi ya sasa. Watu walikuwa wakikamatwa na kuhukumiwa bila dhamana kwa makosa ambayo awali sheria hiyo ililenga kuzuia ujangili wa wanyama wakubwa kama simba, tembo na faru – siyo swala na digidigi. Tunashukuru kwamba, baada ya mchakato wa kupokea maoni na mapitio ya sheria hiyo, ilifanyiwa marekebisho ili iweze kuendana na madhumuni halisi ya serikali na maslahi ya taifa kwa ujumla,” alifafanua.
Aidha, Kamishna Shuli alisisitiza umuhimu wa ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali za kisheria katika kuhakikisha haki za binadamu zinalindwa na sheria zinaendana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi.
Kwa upande wake, Mwandishi wa Sheria kutoka OCPD, Bi. Happyphania Luena, alitoa shukrani kwa Kamishna Shuli kwa kutembelea banda hilo na kuonesha nia ya kujifunza kuhusu kazi za ofisi hiyo. Alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya OCPD na Tume ya Haki za Binadamu ni wa msingi katika kuhakikisha haki na sheria vinazingatiwa katika jamii.
“Mbele yako ni Juzuu za Sheria zilizofanyiwa urekebishaji, Toleo la Mwaka 2023. Tumezileta hapa kwa lengo la kuwaelimisha wananchi kuhusu sababu za kufutwa kwa Toleo la Mwaka 2002 na umuhimu wa mabadiliko haya mapya ya sheria. Tunatumia nafasi hii kutoa elimu kuhusu kazi ya urekebishaji wa sheria na umuhimu wake katika kuimarisha utawala wa sheria,” alieleza Bi. Happyphania.
Maonesho ya SABASABA yameendelea kuwa jukwaa muhimu kwa taasisi mbalimbali za umma na binafsi kuonesha huduma na bidhaa zao huku pia zikitumia fursa hiyo kuelimisha umma kuhusu shughuli zao.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi