Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma
MKUU wa Mkoa wa Tabora Paulo Chacha amesema kuwa hali ya Uchumi ya Mkoa wa Tabora imeendelea kuimarika ambapo Pato halisi la Mkoa limekua kutoka Shilingi Trilioni 5.4 mwaka 2020 hadi Shilingi Trilioni 6.3 mwaka 2024 sawa na ukuaji wa asilimia 17.
Vilevile, pato la mtu mmoja mmoja limeongezeka kutoka shilingi milioni 1.77 mwaka 2020 hadi shilingi milioni 1.85 mwaka 2024 sawa na ongezeko la asilimia 4.5.
RC Chacha amesema hayo jijini hapa leo Julai 11,2025 wakati akizungumza waandishi wa habari kuhusu mafanikio ya Serikali ya awamu ya sita.

Amesema kuwa Uchumi wa Mkoa huo umekuwa kwa kutegemea kilimo, ufugaji, uchimbaji madini, uvunaji mazao ya maliasili, biashara, uzalishaji katika viwanda vidogo miundombinu, huduma za jamii na Utawala.
Ameeleza kuwa Kilimo na Ufugaji huchangia asilimia 70 ya pato la Mkoa ambapo mazao makuu yalimwayo kwa ajili ya chakula ni Mahindi, Mpunga, Mtama, Muhogo, Viazi vitamu, Uwele na jamii ya mikunde. Aidha, mazao ya biashara ni tumbaku, pamba, alizeti, karanga na mchikichi.
Amesema kuwa Sekta ya Kilimo ni sekta muhimu inayogusa wananchi wote wa Mkoa wa Tabora, Serikali ya awamu ya sita imewezesha Mkoa kusimamia sekta hiyo ili kuhakikisha uzalishaji unakuwa wenye tija na usalama wa chakula unaimarika.
“Serikali imekuwa ikitoa fedha nyingi kwa njia ya ruzuku ya mbolea na mbegu. Aidha, imetoa jumla ya Shilingi 52.8 bilioni kwa ajili ya ruzuku na miradi ya umwagiliaji.
“Skimu za umwagiliaji zimeongezeka kutoka skimu 25 mwaka 2020 hadi skimu 46 mwaka 2025 na Eneo la umwagiliaji limeongezeka kutoka ekari 16,453.25 mwaka 2020 hadi ekari 37,560.25 mwaka 2025,”amesema.
Vilevile Mkuu wa Mkoa wa huo amesema kuwa Mkoa huo umeendelea kupiga hatua kubwa katika sekta ya uzalishaji wa asali na uhifadhi wa mazingira, hali inayochochea maendeleo ya kiuchumi kwa wakulima na kuimarisha thamani ya asali ya Tabora kitaifa na kimataifa.
Ambapo amesema hadi kufikia mwaka 2025, viwanda vinne vya kisasa vya kuchakata na kufungasha asali vimejengwa katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo kwa lengo la kuongeza thamani ya zao hilo.
“Mwaka 2020 tulikuwa na uzalishaji wa asali tani 1,868.6, lakini sasa tumefikia tani 2,002.48 kwa mwaka 2025,hii ni hatua kubwa inayotokana na mikakati ya mkoa katika kuwajengea uwezo wafugaji wa nyuki na kuvutia uwekezaji kwenye sekta hii,” amesema Chacha.
Aidha, ameongeza kuwa mafanikio hayo yameenda sambamba na juhudi za uhifadhi wa mazingira, ambapo misitu ya hifadhi ya vijiji imeongezeka kutoka misitu 6 yenye ekari 11,952.5 mwaka 2020 hadi misitu 37 yenye ukubwa wa ekari 330,780.75 mwaka 2025.
“Kuongezeka kwa misitu ya hifadhi ya vijiji ni matokeo ya ushirikiano mzuri kati ya serikali, wananchi na wadau wa mazingira, hii inalinda vyanzo vya uzalishaji wa asali na kuongeza kipato kwa jamii,”amesema.
Mkuu huyo wa mkoa amehimiza wakazi wa Tabora kuendelea kutumia fursa ya sekta ya asali kwa njia endelevu na kuwataka wawekezaji zaidi kujitokeza, akisema Tabora iko tayari kwa ushirikiano wa kibiashara.


More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI