Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya Bia Tanzania (TBL) inayoongoza kwa utengenezaji wa vinywaji hapa nchini, pamoja na kampuni zake tanzu imetangaza matokeo yake ya mwaka wa fedha ulioishia Desemba 31,2024.
Matokeo hayo yametangazwa leo kwenye Mkutano wake na wadau uliofanyikia katika ukumbi wa kimataifa wa mikutano wa Julius nyerere (JNICC), jijini Dar es Salaam.
Akitangaza matokeo hayo, Mwenyekiti wa Bodi Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL Plc), Leonard Mususa amesema Kampuni hiyo iliendelea kufanikisha ukuaji imara wa mapato na faida katika mwaka wa 2024.
Amesema, mapato yaliongezeka kwa asilimia 15, yakichochewa na nguvu ya bidhaa za Kampuni hiyo pamoja na biashara ya vinywaji vikali.
“Usimamizi madhubuti wa mapato, ufanisi katika uzalishaji na usambazaji, pamoja na nidhamu ya matumizi ya mapato, umechangia ongezeko la faida ya uendeshaji kwa asilimia 23.
“Lakini pia, kuongezeka kwa kiwango cha faida ya uendeshaji kwa alama 1.2. Sekta ya vinywaji vyenye kilevi nchini Tanzania ilionesha maendeleo makubwa katika mwaka 2024,” amesema Leonard Mususa, Mwenyekiti wa Bodi (TBL).
Aidha, amesema kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali pamoja na ongezeko la matumizi ya serikali kuliwezesha wananchi kuwa na kipato cha ziada, jambo lililoinufaisha sekta pamoja na kampuni.
“Mwaka 2024 tulishuhudia uwiano mzuri wa ununuzi wa bidhaa katika ujazo tofauti.
Mikakati yetu iliendelea kulenga utekelezaji wa malengo yetu ya kibiashara, ambayo ni kuongoza na kukuza sekta ya vinywaji vyenye kileo nchini.

“Kuendelea kuboresha ufanisi wa biashara yetu na kuongeza kasi kwenye mabadiliko ya kidijitali. Tuliendelea kuzingatia na kuwekeza katika mauzo na masoko ya bia zetu, pamoja na ubunifu kupitia matangazo, ushirikiano wa kimkakati na kujitangaza kwenye matamasha na majukwaa mbalimbali,” amesema.
Vilevile, amesema mwaka 2024, waliendelea kudhibiti zaidi ya theluthi mbili ya soko la bia nchini kupitia mkusanyiko wa chapa zao bora na maarufu.
Pia, waliendelea kuwekeza katika ubunifu ili kuongeza fursa za matumizi na kukidhi mabadiliko ya mahitaji ya walaji.
Hata hivyo, Mwenyekiti huyi wa Bodi amesema ufanisi na ubunifu wao katika masoko ulitambuliwa rasmi kwa timu yao kutangwazwa kuwa timu Bora ya Masoko ya mwaka na Tanzania Marketing Science Association TMSA, huku bia ya Safari Lager na Konyagi zikitambuliwa kimataifa.
Mususa amesema, mwaka 2024 kupitia majukwaa ya BEES na KUJA, waliwaunganisha wasambazaji zaidi ya 120 moja kwa moja na wateja wa mwisho. Matokeo yake, bidhaa zao zilifikia takriban wauzaji wa bia rejareja 22,000 kote nchini.
Amesema, waliendelea kutenga rasilimali kwa ajili ya kuboresha miundombinu ya uzalishaji na usambazaji, huku wakiweka mkazo katika vifungashio vinavyorejeshwa na kuhakikisha viwanda vyao vinaendeleza kasi ya ukuaji.
“Mwaka 2024, tulitumia jumla ya Shilingi bilioni 88.4 za Tanzania katika uwekezaji ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha Kilimanjaro Malting kilichokamilika na kuanza kufanya kazi katika robo ya mwisho ya mwaka 2024, chenye uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za kimea cha shayiri kwa mwaka,” amesema.
Ameongeza kuwa, “Tuliendelea kutekeleza vipaumbele vyetu vya maendeleo endelevu kupitia programu za kilimo cha kisasa, vifungashio vinavyohifadhi mazingira, mipango ya kuhifadhi hali ya hewa na maji, pamoja na uwezeshaji wa ujasiriamali,”.

Pia, mwaka 2024, TBL Plc ilizindua mpango wa kuendeleza wauzaji wa bidhaa zao (Retailers Development Programme) kwa lengo la kuboresha ujuzi wa biashara, uendelevu, na ufanisi wa kiutendaji kwa wafanyabiashara 22,000 wa rejareja kote nchini, ambapo wafanyabiashara 1,700 walipata mafunzo hayo ndani ya mwaka huo.
Amesema kuwa, ufanisi wao wa miaka minne mfululizo hadi kufikia mwaka 2024 uliwapa matumaini makubwa wanapoelekea mwaka 2025.
Licha ya mazingira ya biashara yenye mabadiliko ya mara kwa mara lakini alisema, waliendelea kuwa imara na wana imani katika uwezo wa timu yao kutekeleza mikakati yao ya kibiashara na kufikia malengo ya ukuaji endelevu.
Amewashukuru wanahisa wao wote kwa msaada wao wa kudumu, na Bodi kwa kuendeleza viwango vya juu vya uongozi na utawala bora wa kampuni.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi