Na Esther Macha,TimesmajiraOnline,Mbeya
ILI kuweka hali ya usalama wakati wa Maonesho ya wakulima Nane nane Halmashauri zote za Mkoa wa Mbeya pamoja na Taasisi zimevunja miundo mbinu ya majengo yao ili kupisha maboresho ya uwanja huo yanayoendelea kwa ajili ya Maonesho ya Kikanda ambayo yatafanyika katika viwanja vya John Mwakangale Jijini hapa.
Aidha imeelezwa kuwa samba samba na uvunjaji huo pia vitaundwa vijiji ili kuzuia watu kusambaa eneo kubwa la uwanja kama ilivyokuwa ikifanyika miaka iliyopita.
Hayo yamesemwa Julai,8,2025 na Katibu Tawala Msaidizi Uchumi na uzalishaji Mkoa wa Mbeya,Said Madito wakati wa kikao cha kamati ya maandalizi cha Maonyesho ya wakulima nane nane ambayo hufanya kila mwaka katika uwanja wa John Mwakangale Jijini Mbeya.
Hata hivyo Madito amesema, halmashauri na taasisi zote tayari zimevunja miundombinu ya majengo yao ndani ya uwanja huo pamoja na uzio hivyo wataunda vijiji ili kuzuia watu kusambaa eneo kubwa la uwanja kama ilivyokua ikifanyika miaka iliyopita.
“Lengo letu kuweka uwanja huu wa Maonyesho katika hali ya usalama ili shughuli zote za Maonyesho ziweze kwenda vizuri bila mwingiliano”amesema Madito.
Katika kikao cha maandalizi ya maonesho hayo msimamizi wa ujenzi wa uwanja kutoka Wizara ya kilimo Mhandisi, Elizabeth Mziray amesema maelekezo ya Wizara ilikua ni kuanza na lango kuu la kuingilia, Uzio na Maduka ya mbele ambavyo ujenzi unaendelea hadi sasa na umefikia zaidi ya asilimia 20 na kwamba vitakamilika ifikapo July 30 kwakua mkandarasi yupo eneo la kazi kuendelea na ujezi.
Nao baadhi ya wadau wa maonesho hayo wameiomba sekretalieti ya maandalizi kuangalia namna ya kuwepo kwa uzio wa muda ikiwemo wa mabati ili kuongeza usalama wakati wa maonesho huku baadhi ya wananchi wakieleza hali ya maandalizi na vipando ndani ya uwanja.
Wamesema kuwa uzio unapokuwa umewekwa mabati kwa muda ulinzi unakuwa wa kutosha kwa wakulima wakati wa shughuli za Maonyesho zikiendelea ili kuzuia vibaka ambao wanaweza kujitokeza ndani ya uwanja huo.
Neema Juma ni mjasiriamali mdogo anayefanya biashara za kuuza nafaka amesema kuwa uwepo wa Maonesho hayo unawapa fursa za kuuza bidhaa zao kwa wingi.

More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi