Na Heri Shaaban, Timesmajira Online-Dar-es- Salaam
OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, itaendelea kuboresha ushauri kwa taasisi za umma wakati wa kuingia mikataba mbalimbali ili iwe bora na kutimiza malengo ya Serikali,ambayo itanufaisha wananchi.
Hayo yamesemwa na Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali,Samwel Maneno, katika maonesho ya Kimataifa ya 49 ya Biashara ya Saba Saba yanayoendelea katika viwanja vya Saba Saba wilayani Temeke mkoani Dar-es-Salaam.

“Tunaendelea kuzipa ushauri taasisi za umma ili kuwa na ubora wa mikataba,pia kuhakikisha kwamba utekelezaji wa
mikataba hiyo inafanyika kwa mujibu wa makubaliano,”amesema Maneno .
Maneno amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali inayatumia maonesho hayo katika kutoa ushauri wa kisheria, kushughulikia malalamiko, utatuzi wa migogoro na elimu ya sheria hususani sheria zilizofanyiwa urekebu toleo la mwaka 2023 zilizoanza kutumika Julai Mosi mwaka huu.
“Sheria zilizofanyiwa urekebu zimezinduliwa na zimeanza kutumika na kitu kizuri ni kuwa kati ya sheria 446 sheria 300 zinapatikana kwa lugha ya kiswahili,”amesema .
Pia Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipata fursa kutembelea mabanda ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwandishi Mkuu wa Sheria pamoja na Taasisi ya Mafunzo ya uanasheria kwa vitendo, kuona shughuli zinazotekelezwa na taasisi hizo katika maonesho hayo.

Maonesho ya Sabasaba 2025 yamezinduliwa rasmi na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo yanatarajiwa kumalizika Julai 13,2025.

More Stories
Wanawake washauriwa kuchangamkia fursa za uchumi
Aida:Wanawake wakipata haki zote itapunguza migogoro
LGTI wanawake waadhimisha siku yao Ngorongoro