Na Heri Shaaban, Timesmajira Online-Dar
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Hamza Johari, amemkabidhi Juzuu za Sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la Mwaka 2023 Jaji Mkuu wa Tanzania George Masaju.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Juzuu hizo, Johari,ameeleza kuwa kuanza kutumika kwa sheria kutairahisishia Mahakama wakati wa kutekeleza majukumu yake ya utendaji haki kwa wananchi.
” Jaji Mkuu baada ya kukamilika kwa zoezi la urekebu na Rais alizindua na alitoa tamko kwamba sheria hizi zianze kutumika kuanzia Julai 1,2025, hivyo tumekuja na timu yangu kukukabidhi rasmi Juzuu hizi zilizofanyiwa Urekebu,”amesema Johari.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa mradi wa urekebu wa sheria umefanyika kwa kutumia rasilimali za fedha za ndani na rasilimali watu wa ndani, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo mradi huo ulikuwa ukiendeshwa na wahisani.
Akipokea juzuu hizo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji George Masaju,ameeleza kuwa Mahakama ni mtumiaji mkubwa wa sheria hizo na zitasaidia katika utendaji kazi wake.
“Sisi kama Mahakama ni moja ya watumiaji wakuu kwa sababu mambo mengi yanaishia mahakamani hivyo tukiwa na hizi juzuu zitatusaidia,”amesema Masaju.
Katika hatua nyingine Jaji Mkuu wa Tanzania ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuukamilisha mradi wa urekebu wa sheria kwa kutumia rasimali fedha za ndani pamoja na kuzifanya sheria hizo kupatikana bure kwa njia ya mtandao na kuwasaidia watumiaji wengi kuzipata kwa urahisi.
Awali, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania kwa mchango wake katika kukamilisha zoezi hilo tangu akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo amesema wamekabidhi seti ya Juzuu za sheria za nchi 20 ambayo ina jumla ya sheria kuu 446.
Vilevile Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan,ya kuhakikisha Sheria hizi zinapatikana, ambapo sheria hizo zinapatikana katika mfumo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ujulikanao kama OAG-MIS.
“Kama alivyoelekeza,Rais wakati wa uzinduzi kuwa sheria hizi ziwe zinapatikana kwa urahisi na kwa njia ya kuuzwa na mchapishaji Mkuki na Nyoto pia zinapatikana katika mfumo wa OAG-MIS wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali,”.
Juzuu za Sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la mwaka 2023 zilisainiwa na kutolewa tamko na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan Aprili 23 , 2025 na zimeanza kutumika kuanzia tarehe Julai 1,2025.

More Stories
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI