Na Daud Magesa, Timesmajira Online-Mwanza
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mwanza,kimevitaka vikao vya uteuzi wa wagombea wa nafasi za ubunge na udiwani kuhakikisha vinatenda haki kwa maslahi ya chama hicho.
Pia,wagombea wahakikishe wanaheshimu na kufuata katiba,kanuni,taratibu na miongozo ya CCM wakati wakisubiri kura za maoni.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mwanza, Omar Mtuwa, amesema hayo Julai 3,2025, wakati akizungumza na waandishi wa habari jijini hapa, amesema mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu umekamilika vizuri na orodha ya wagombea iko tayari.
“Tunashukuru mchakato wa kuchukua na kurejesha fomu umekwenda vizuri na hakuna malalamiko.Kimebaki kipindi cha mchujo na kura za maoni, ambapo vikao husika vitapitia majina ya wagombea wote ili kuwapata watakaostahili kupeperusha bendera ya CCM,” amesema .
Mtuwa amesema msisimko mkubwa wa wanachama kujitokeza kuchukua fomu za ubunge na udiwani umetokana na hamasa ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Dk. Samia Suluhu Hassan, na Katibu Mkuu wa chama, Dkt. Emmanuel Nchimbi, hali iliyowafanya vijana wengi kujitokeza kuwania nafasi mbalimbali.
Mtuwa amefafanua kuwa kwa mujibu wa kanuni za CCM, watapendekezwa wagombea watatu kutoka kila eneo, ambapo mmoja mwenye sifa bora zaidi ataptishwa na Chama kugombea katika uchaguzi mkuu ujao.
CCM Mkoa wa Mwanza imesisitiza mchakato wa ndani uendeshwe kwa haki, umoja na kuzingatia misingi ya Chama, huku wagombea wakitakiwa kuwa na subira na heshima kwa taratibu zinazoongoza uchaguzi wa ndani wa chama.
Hata hivyo, duru za kisiasa zinaonesha majimbo yanayotarajiwa kuwa na ushindani ni Nyamagana, Stanslaus Mabula anatarajiwa kuchuana na Lawrence Masha (Mbunge wa zamani na Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani),Balozi Prof. Adelardus Kilangi (Mwanasheria Mkuu wa Serikali wa zamani) na Abuu Seif (Mwenyekiti wa Mtaa wa Nera)
Huku Jimbo la Ilemela, Dkt. Angeline Mabula (Mbunge aliyemaliza muda wake) anakabiliana na Leonard Qwihaya ‘Manguzo’ na William Kafiti, huku Sengerema, Hamis Mwagao ‘Tabasamu’akitajwa kuchuana vikali na William Ngeleja (Waziri wa zamani wa Nishati na Madini).
Katika Jimbo la Misungwi, Mbunge wa sasa Alexander Mnyeti anatajwa kumenyana vikali na Charles Kitangwa ‘Mawe Matatu’ (Waziri wa zamani wa Mambo ya Ndani) ambapo Buchosa, Eric Shigongo atakabiliana na Dkt.Charles Tizeba (Mbunge wa zamani wa jimbo hilo).

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako