Na Mwandishi Wetu, Timesmajira Online
KAMPUNI ya mawasiliano ya Yas, imezindua rasmi jukwaa la Anzia Ulipo Biashara Expo, katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara maarufu kama Sabasaba.
Lengo ni, kuwa jukwaa mahsusi kwa ajili ya kuwawezesha wajasiriamali chipukizi kuonyesha biashara zao na kupata ujuzi wa kukuza shughuli zao za kiuchumi.
Uzinduzi huo ulifanyika Julai 2, 2025 kwenye viwanja vya Mwalimu Nyerere, Dar es Salaam, ambapo jumla ya wajasiriamali 20 waliodhaminiwa na Yas.
Wajasiriamali hao walipata fursa ya kuonesha bidhaa na huduma wanazotoa, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo kuwaunga mkono Watanzania wanaoanza safari ya mafanikio.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Yas Kanda ya Dar es Salaam Kusini, Robert Kasulwa amesema jukwaa hilo ni sehemu ya kampeni ya kitaifa ya Anzia Ulipo, inayolenga kuwahamasisha Watanzania kuanza na kile walicho nacho huku wakisukumwa na ndoto kubwa.

“Wajasiriamali tuliowadhamini wamechaguliwa kwa misingi ya uthubutu, ubunifu na maono. Kupitia Sabasaba, wanapata fursa ya kujitangaza, kujifunza na kutengeneza mitandao ya kibiashara. Hii ni hatua muhimu ya kupeleka ndoto zao kwenye jukwaa la kitaifa,” amesema Kasulwa.
Kasulwa ameongeza kuwa Yas inaendelea kuwa mshirika wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia huduma zake za kidijitali kama Mixx by Yas, pamoja na miundombinu ya kisasa ya intaneti kupitia teknolojia ya 4G na 5G, inayowawezesha Watanzania kufanya kazi na kuendesha biashara kwa ufanisi zaidi.
“Tunaamini mafanikio yanaweza kuanza popote pale mtu alipo, ilimradi tu awe na ndoto, uthubutu na mshirika sahihi. Yas tunatoa hayo yote – huduma, nyenzo na jukwaa la kuonyesha uwezo wa Watanzania,” ameongeza.

Akiwataka wananchi kutembelea banda hilo maalum, Kasulwa amesema:
“Tunawaalika Watanzania wote wanaotembelea Maonesho ya Sabasaba kufika katika banda la ‘Anzia Ulipo Biashara Expo’, kushuhudia ubunifu na bidhaa kutoka kwa wajasiriamali wetu. Hii ni fursa ya kuunga mkono ndoto za Watanzania wenzetu waliothubutu kuanza.”


More Stories
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako
TTCL yaadhimisha siku ya Wanawake kwa kutoa msaada JKCI
Wananchi Dodoma washauri TBA kujenga nyumba za kupangisha watu binafsi