Na Yusuph Mussa,Timesmajiraonline,Lushoto
WAKATI zoezi la kuchukua fomu kwa ajili ya mchakato wa ubunge ndani ya Chama Cha Mapinduzi ukikamilika Julai 2, 2025, Mwanadiplomasia Jasmine Shekalaghe amechukua fomu kumkabili Mbunge wa sasa Jimbo la Bumbuli, January Makamba.
Shekalaghe kutoka Kijiji cha Kihitu, Kata ya Vuga, Tarafa ya Soni, alichukua na kurudisha fomu kwenye Ofisi ya CCM Wilaya ya Lushoto, huku akijinasibu kuwa ni mtu mwenye maono kwa ajili ya maendeleo ya wananchi wa Bumbuli.
“Mimi ni mwenye maono ya kweli kwa wana Bumbuli. Na nataka kuleta mabadiliko mapya kwa ajili ya kusogeza mbele maendeleo ya wana Bumbuli. Najua kuna jitihada kubwa zimefanywa na Rais wetu Mama Dkt. Samia Suluhu Hassan, lakini bado jitihada zinahitajika ili kufikia matarajio ya wana Bumbuli” amesema Shekalaghe.
Katika majimbo matatu ya Wilaya ya Lushoto, ya Mlalo, Bumbuli na Lushoto, mchuano mkali unatarajiwa kuonekana Jimbo la Lushoto kati ya aliyekuwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo, Profesa Riziki Shemdoe, aliyekuwa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Lushoto Mathew Mbaruku, na Mbunge wa sasa Shaaban Shekilindi.
Wakati kwa Jimbo la Mlalo, kinyang’anyiro kinaonekana ni kati ya Mbunge wa sasa Rashid Shangazi, Amiri Mkufya na Gao Ngwilizi ambaye ni mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Mlalo, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi.
Baadhi ya watia nia wengine waliochukua fomu Jimbo la Lushoto ni Dkt. Wemael Chamshama, Wakili msomi Remigius Mainde na Hellen Mushi. Wakati Jimbo la Bumbuli ni Hussein Mshangama.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako