March 8, 2026

Timesmajira

Gazeti Huru La Kila Siku

Rais Samia azindua kiwanda cha mbolea INTERACOM,asisitiza elimu matumizi ya mbolea

Na Zena Mohamed,Timesmajiraonline,Dodoma

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan amezitaka Mamlaka za Mikoa na Serikali za Mitaa kutoa elimu ya kina kwa wakulima juu ya matumizi sahihi na vipimo vya mbolea ya FOMI katika uzalishaji wa mazao mbalimbali.

Amesema kuwa wakulima wanaweza kufikiwa na mbolea hiyo lakini wasiwe na maelekezo sahihi ya namna ya kuitumia.

Dkt.Samia amesema hayo jijini hapa Juni 28,2025 wakati wakati akizindua na kufungua Kiwanda cha Mbolea cha ITRACOM  kilichopo Nala,akishirikiana na mgeni wake Rais wa Jamuhuri ya Burundi Meja Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye.

Amesema kuwa elimu hiyo ni muhimu ili kuhakikisha mbolea inatumika kwa tija na kwa kuzingatia viwango vinavyofaa kwa kila aina ya zao na ardhi husika.

Hata hivyo ameongeza kuwa kwa kutoa elimu hiyo,kiwanda hicho kitakuwa kimechangia kwa kiasi kikubwa katika kuimarisha usalama wa chakula,kupunguza umasikini na kuongeza ajira kwa vijana na wanawake.

“Kiwango cha biashara kati ya Burundi na Tanzania kinaendelea kukua hivyo uwekezaji huu unaongeza fursa za ajira kwa vijana wetu, na kupitia mpango wa kuongeza vituo vya uuzaji wa pembejeo, wakulima sasa wanapata vifaa kwa gharama nafuu. Serikali imeanzisha pia mpango mkakati wa kujenga mabwawa ili kukabiliana na changamoto za ukosefu wa mvua.”amesema.

Vilevile amesisitiza uongozi wa kiwanda hicho kuhakikisha kuwa wanaimarisha mfumo wa usambazaji wa mbolea ili iweze kuwafikia wakulima waliopo vijijini.

Kwa upande wake Rais wa Jamhuri ya Burundi Meja Jenerali Mstaafu Evariste Ndayishimiye,amesema uzinduzi wa kiwanda hicho ni hatua muhimu ya kuchochea maendeleo katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Ndayishimiye,amesema kuwa kumekuwa na mabadiliko makubwa ya mahusiano kati ya Burundi na Tanzania.”Zamani tulikuwa tunakuja kama wakimbizi,sasa tunakuja kama wawekezaji.

“Naishukuru Serikali ya Tanzania na wananchi wake kwa moyo wa ukarimu na kwa kuunga mkono mradi huo mkubwa,amefafanua kuwa kiwanda cha ITRACOM hakitachochea tu maendeleo ya kilimo bali pia kitaimarisha mshikamano wa kikanda”amesema Rais Ndayishimiye

Naye  Waziri wa Kilimo Hussein Bashe,amesema kuwa Serikali ya awamu ya sita imetekeleza kwa kina zana ya maendeleo kupitia wizara ya kilimo. Milioni 700 zimetengwa kwa ajili ya kuwapa wananchi ruzuku ya mbolea, na zaidi ya bilioni 500 zimetumika kwa ajili ya kuwapa wakulima wa korosho.

“Tanzania kwa sasa tunazihudumia nchi za Kenya, Congo, Kuanzia tarehe 1 Septemba 2025, wananchi wataanza kununua mbolea kwa bei ya ruzuku.”amesema.

Awali Mkurugenzi Mtendaji wa Kiwanda cha ITRACOM Nduwimana Nazaire,amesema kuwa kiwanda hicho kina uwezo wa kuzalisha mbolea Tani Milioni moja kwa mwaka huku ajira zaidi 1800 za moja kwa moja tayari zimeshatolewa.

“Ilikuwa kama ndoto, leo tumetimiza Ujenzi  na kufungua kiwanda hiki kina uwezo wa kuzalisha mbolea tani milioni moja kwa mwaka. Mwaka 2020 mradi ulianza kutekelezwa, wewe ukiwa kama Makamu wa Rais. Kwa msimamo wako dhabiti ulihakikisha kiwanda hiki kinatekelezwa na kujengwa.”amesema Bw.Nazaire

Pia amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Burundi kwa kuruhusu uwekezaji huo wa mbolea hizo zinaboresha afya za udongo na zinaongeza mavuno, zimetengenezwa kwa mchanganyiko wa vitu mbalimbali.
“Kiwanda hiki kimetengeneza zaidi ya ajira 1,800 na kuna ajira zingine zisizo za moja  kwa moja ambazo ni 3,000.