Na Judith Ferdinand, Timesmajira Online-Mwanza
Katika kipindi cha kuanzia Machi 2024 hadi Aprili 2025, Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela kupitia Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii stendi ya mabasi Nyamhongolo,imefanikiwa kuwahudumia watoto 146.
Kati yao wasichana ni 81 na wavulana ni 65,ambapo asilimia 68 ya watoto waliopatiwa huduma katika dawati hilo ni wenye umri kati ya miaka 7- 14 huku asilimia 31 ni watoto wenye umri wa miaka 15 -17 na asilimia moja ni watoto wenye umri wa miaka 7.
Hayo yamebainishwa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Halmashauri ya Manispaa ya Ilemela,anaeshughulika na Dawati la Huduma za Ustawi wa Jamii katika stendi hiyo,
Lucy Katonkola, amesema,uanzishwaji wa dawati hilo katika vituo vya usafiri ni maelekezo ya Serikali kupitia Ofisi ya Rais TAMISEMI,juu ya uwepo wa Maofisa Ustawi wa Jamii katika maeneo ya bandari na stendi kuu za mabasi yaendayo mikoani tangu Juni 2022.
Lucy amesema,lengo kuu la uanzishwaji wa madawati hayo ni kuimarisha utoaji wa huduma kwa makundi maalumu hususani kuzuia watoto kuingia mtaani pamoja na usafirishaji haramu wa binadamu (human trafficking),kubaini na kuzuia watoto wanaosafirishwa kinyemela na kusaidia watu waliopo katika mazingira hatarishi maeneo ya stendi.
Sanjari na hayo,Lucy ametoa rai kwa wazazi na walezi kuachana tabia ya kusafirisha watoto wadogo peke yao bila usimamizi wa mtu mzima, huku akiwataka wananchi wanaozunguka maeneo ya stendi kuhakikisha wanatoa kipaumbele katika suala la ulinzi na usalama wa watoto katika maeneo hayo.
Kwa upande wake Ofisa Mradi wa shirika la Railway Children Africa (RCA),Anitha Joseph,amsema wamekuwa wakijishughulisha na watoto na vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi pamoja na familia zao.
Huku wakilenga kuimarisha muitikio wa jamii juu ya watoto na vijana walio katika mazingira hatarishi hasa waliopo mitaani kwa kutoa elimu kwa jamii,namna ya kuzuia na kudhibiti wimbi la watoto mitaani kwa kushirikiana na serikali kuzitafsiri sheria na miongozo inayolenga kuwasaidia watoto na vijana hao.

More Stories
Bilioni 7 kuwainua vijana 308 sekta ya uvuvi
Clara:Miaka 50 ya Sabasaba fursa mpya za Biashara na Uwekezaji
Usajili wa Laini za Simu: Jilinde Dhidi ya Kutumiwa Vibaya kwa Utambulisho Wako